hatimaye mfanyabiashara mwingine maarufu amwagiwa tindikali jijini arusha


Kamanda, Liberatus Sabas.
Mfanyabiashara wa madirisha ya alluminium jijini Arusha, Japhet  Minja (30), amelazwa katika Hospitali ya Selian jijini hapa, baada ya kumwagiwa kimiminika kinachodaiwa kuwa ni tindikali usoni na watu wasiojulikana.


Tukio hilo la kusikitisha limetokea jana saa 12:15 alfajiri katika eneo la Shamsi, wakati mfanyabiashara huyo akitoka nyumbani kwake kwenda kazini.

Akisimulia tukio hilo, mmoja wa ndugu zake ambaye hakutaja jina lake, alisema kuwa Minja alikumbwa na mkasa huo wakati akienda kwenye   shughuli zake za kila siku.


Alisema baada ya kufika eneo la Shamsi, Minja alikutana na vijana wanne wakiwa wamesimama barabarani kisha walimsimamisha kama vile walikuwa wakitaka kumuomba msaada.

“Baada ya ndugu yangu kusimama, alishusha kioo cha gari upande wake na hapo wale vijana wakafungua mlango kwa nguvu na kumchomoa ndani ya gari na kumtoa nje, kisha kumshambulia kwa kumpiga na baadaye  kumwagia tindikali usoni,” alisema.

Alisema kuwa baada ya kumwagia tindikali wakati watu waliokuwa karibu na  eneo hilo wakikusanyika vijana hao walikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Alisema watu hao walimchukua Minja na kumkimbiza hospitalini hapo kwa matibabu waandishi wa habari walipofika hospitalini hapo kufuatilia tukio hilo, walizuiwa na  uongozi  kutokana na majeruhi huyo kulazwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU)Mganga wa Hospitali hiyo, Dk. Godbless Massawe,


 Aliyempokea Minja hospitalini hapo kwa matibabu,    alithibitisha  kuwa alimwagiwa kitu ambacho mpaka sasa hawajaweza kukibaini kwa kuwa  vipimo vya kubaini tindikali kwa nchini, vinapatikana Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Dk. Massawe alisema  kitu alichomwagiwa Minja kilikuwa kinamsababishia macho yake kukosa nguvu ya kuona, kadri muda ulivyokuwa ukienda huku kikimsababishia apate maumivu makali kwenye ngozi ya uso.

Alisema wakati akiendelea kupatia huduma ya kwanza, alilalamika kuwa anapata shida kuhema, wakamwekea hewa ya oksijeni na baada yamuda alishindwa kuzungumza, lakini alianza kupata nafuu baada ya kuendelea kumhudumia.

 Dk. Massawe alisema baada ya kupata nafuu aliweza kusema kuna wateja walikwenda nyumbani kwake na kumuomba awauzie madirisha kwa Sh. milioni 4, lakini walimpatia Sh. milioni 3.

Alisema baada ya kumapatia fedha hizo waliongozana hadi barabarani na wakiwa njiani kuna watu wakazuia gari la wateja wake na alipoamua kushuka, ndipo alipovamiwa na baadhi yao wakaingia kwenye gari lake na kuchukua fedha zake kisha kummwagia ‘spray’ kwenye macho.

Alisema  Minja aliendesha gari mwenyewe hadi duka moja la dawa nao wakamshauri anawe uso na aliponawa aliambiwa aende hospitalini.

Alisema alikwenda zahanati moja ambayo hakuitaja na kushauriwa kwenda  hospitali kubwa na alipofika Selian, akaanza kujisikia vibaya na kupoteza fahamu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusisitiza kwamba wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini kitu alichomwagiwa mfanyabiashara huyo.

“Kitu kinachotupa mashaka ni kimoja kuwa yule mtu aliendesha gari mwenyewe, sasa kama tindikali utaweza kuendesha gari kweli, hivyo vitakuwa visa tu,” alisema Sabas.

Matukio ya watu kumwagiwa tindikali yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka nchini.

Masoud Mohamed Shambi, mkazi wa kisiwa cha Pemba, alikumbwa na mkasa huo mwaka 2000.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Zanzibar, Rashid Ali Juma (45) naye, alimwagiwa tindikali Februari 18, 2011, saa 2:30 usiku, nje ya msikiti wa Amaan.


Novemba 5, 2012, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, alimwagiwa tindikali na mtu asiyefahamika wakati akifanya mazoezi ya viungo kwenye Uwanja wa Mwanakwerekwe.

Mwaka 2012 mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia mjini Zanzibar, Chandurali Chunilai Asawala alimwagiwa tindikali.

Mei 23, 2013, Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Mkoa Mjini Magharibi, Mohamed Said Omar maarufu kwa jina la Kidevu, pia alimwagiwa tindikali.

Agosti 7, 2013,  saa 1:15 usiku, watu wawili waliokuwa katika pikipiki kwenye eneo la Mji Mkongwe, Mtaa wa Shangani, waliwamwagia tindikali mabinti wawili, raia wa Uingereza,  Katie Gee (18) na Kirstie Trup (18) waliokuwa Zanzibar wakifanya kazi ya ualimu kwa kujitolea.

Septemba 14, 2013, Padri Ancelmo Mwang'amba wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Cheju, alimwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana katika maeneo ya Mlandege.  
 
Mwaka 1995, aliyewahi kuwa Mbunge wa Mwanza Mjini, Said Shomari alimwagiwa tindikali na kujeruhiwa vibaya mwilini, hasa sehemu za shingoni.

Usiku wa kuamkia Julai 13, Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Said Juma Makamba alimwagiwa tindikali wakati akiwa nyumbani kwake eneo la Kwamrombo, Arusha.

Mwingine ni mmiliki wa maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohamed Saad aliyemwagiwa tindikali Julai 19, 2013, usiku wakati akiwa kwenye jengo kubwa la biashara la Msasani City Mall. Mwingine ni Saeed Kubenea, Mkurugenzi wa Hali Halisi Publishers ambao huchapisha gazeti lililofungiwa la Mwanahalisi aliyepatwa na mkasa huo Januari 7, 2008.

Comments