Jukwaa la Wahariri lapinga hukumu ya serikali kufungia gazeti la MWANANCHI, Mtanzani


Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limepinga kufungiwa magazeti ya MWANANCHI na Mtanzania,  kwa madai kwamba sheria ya mwaka 1976 iliyotumiwa na serikali kutoa adhabu hiyo ni kandamizi na imekuwa ikilalamikiwa na wadau kwa miaka mingi sasa.


Taarifa ya TEF iliyosainiwa na Katibu wake, Neville Meena, ilieleza jana kuwa sheria hiyo ni moja ya zile ambazo Tume ya Jaji Francis Nyalali ilipendekeza ifutwe.Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sababu za Tume hiyo kupendekeza sheria hiyo ifutwe ni pamoja na kukiuka misingi ya haki za binadamu, utawala bora na kwenda kinyume cha Katiba ya nchi pamoja na maazimio ya kimataifa ya haki za binadamu.“Hivyo, tunaungana na taasisi nyingine kupinga adhabu hii kwa magazeti ya Mwananchi, Mtanzania na wakati huo huo tukikumbushia kifungo cha gazeti la Mwanahalisi kwa sababu sheria hiyo iliyotumika haifai,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.TEF pia imelaani adhabu hiyo kwa madai kwamba utaratibu uliotumiwa na serikali katika kuitoa, umekiuka ule wa kutoa haki ya asili, kwa kuwa imejigeuza kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka na mtoa adhabu, ambao haukubaliki katika jamii yoyote iliyostaarabika.“Hili si jambo la kuendelea kufumbiwa macho na jamii, ambayo inafuata misingi ya kidemokrasia na utawala bora,” ilieleza taarifa hiyo.Aidha, TEF ilieleza masikitiko yake kutokana na kesi ya kupinga sheria hiyo kutoanza kusikilizwa mahakamani kwa miaka minne sasa kutokana na kutopangiwa jaji wa kuisikiliza.Hivyo, imeitaka Mahakama kurekebisha kasoro hiyo ili kuhakikisha si tu haki inatendeka, bali ionekane inatendeka.Ilieleza kuwa TEF inasikitishwa zaidi na kitendo cha serikali kuendelea kuitumia sheria hiyo, huku ikiwa imekalia kwa miaka mingi sasa miswada miwili ya sheria ya haki za habari bila ya kuipeleka bungeni, hivyo, imeitaka iyafungulie magazeti hayo.Wakati huo huo, Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha MWANANCHI, imefafanua sababu zilizotumiwa na serikali kulifungia gazeti hilo na kusema habari kuhusu mishahara mipya iliandikwa baada ya mwandishi wao kupata taarifa ya kina kutoka kwa mtu waliyemwamini sana serikalini.Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Tido Mhando, pia ilifafanua kuwa hakuna sehemu yoyote katika habari kuhusu Waislamu kusali chini ya ulinzi mkali wa polisi iliyosema Jeshi la Polisi lilipeleka mbwa msikitini.Hivyo, MCL imewaomba radhi wasomaji, watangazaji, wasambazaji na wadau wake wote  watakaokosa habari na kuathirika kwa kipindi cha siku 14 cha adhabu hiyo hadi Oktoba 10, mwaka huu.

Comments