DPP agoma kuzungumzia maendeleo ya kesi ya wasambazaji dawa za kupunguza virusi vya ukimwi ARVs feki


Uwezekano wa kuwashitaki mahakamani wanaohusika na kashfa ya kusambaza Dawa bandia za Kupunguza Makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs), umegubikwa na giza.


Hiyo ni kutokana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kushikwa ghafla na kigugumizi kuzungumzia hatima ya jalada la uchunguzi wa tuhuma hizo.

Ofisi ya DPP imekumbwa na hali hiyo ikiwa imepita miezi mitatu tangu Mkurugenzi mstaafu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, kumwambia mwandishi wa habari hizi kuwa jalada hilo limerejeshwa kwa DPP.

 Manumba alisema jalada hilo limerejeshwa kwa DPP ili kupata ushauri ama wahusika wa kashfa hiyo washitakiwe mahakamani au la.

 Hata hivyo, wakati Manumba akisema hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi, akizungumza na mwandishi wa habri hizi ofisini kwake, jijini Dar es Salaam jana, amegoma kuzungumzia jalada hilo.

 Feleshi alisema hawezi kuzungumzia jalada hilo kwa kuwa lipo ngazi za juu za utekelezaji.
Hata hivyo, Feleshi hakufafanua anaposema ngazi za juu anamaanisha nini. Badala yake, alisema zipo taratibu za kutoa taarifa za serikali baada ya taratibu za kisheria na kiusalama kukamilika.


 “Lazima ifahamike kuwa utoaji wa taarifa za siri na nzito unapaswa kuwa na umakini. Subirini taarifa rasmi itatolewa. Haiwezekani chakula kinapikwa jikoni na kuchunguliwa kila wakati. Kusubiri ni jambo la busara ili kipakuliwe kikiwa kimeiva,” alisema Feleshi.

 Agosti 23, mwaka huu Ofisi ya DPP ilisema imeshindwa kuamua kuwashtaki mahakamani wanaohusika na kashfa hiyo, baada ya kubaini upungufu katika uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi kuhusiana na tuhuma hizo.

Feleshi alisema kutokana na hali hiyo, jalada la uchunguzi wa tuhuma hizo lilirejeshwa kwa DCI ili lifanyiwe marekebisho dhidi ya upungufu uliobainika.

Kashfa kuhusu ARVs bandia, iliibuliwa na vyombo vya habari Septemba mwaka jana, baada ya toleo mojawapo la dawa hizo la Machi, 2011 kubainika kuwa ni bandia Kiwango kikubwa cha dawa hizo, ambazo hutolewa bure na serikali katika hospitali zake, ziliripotiwa kusambazwa na maelfu ya wagonjwa walishazitumia kwa kiasi kikubwa.

ARV hizo ‘feki’ zinazodaiwa kutoka nchini India, ziliingizwa kwenye mfumo, Mei, mwaka jana.
 Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Seleman Rashid, alikaririwa na vyombo vya habari akisema serikali ndiyo iliyogundua kuingizwa kwa ARV hizo ‘feki’ nchini.

Taarifa nyingine zilimkariri mmiliki wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPIL) kinachotengeneza ARV, Zarina Madabida, akisema kiwanda chake ndicho kilichogundua kuwapo kwa dawa hizo.

Zarina, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) alisema baada ya kugundua ARV hizo ‘feki’, alitoa taarifa kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na kuiomba iingilie kati ili kuziondoa kwenye mzunguko.Aidha, kashfa hiyo ilisababisha Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Joseph Mgaya, na vigogo wengine wa MSD, kusimamishwa kazi.

Wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora, Daud Maselo na Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora wa Dawa, Sadick Materu.
Waziri Mwinyi alikaririwa akisema viongozi hao walisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kwa kuruhusu kusambazwa kwa ARV bandia aina ya TT-VIR 30 toleo Na.0C.01.85.

Kwa mujibu wa Waziri Mwinyi, dawa hizo zilisambazwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya nchini. Mbali na viongozi na watendaji hao kusimamishwa kazi, serikali kupitia wizara hiyo pia ilisitisha Kiwanda cha TPIL kuzalisha dawa hizo.


chanzo:NIPASHE

Comments