Wafungwa wa walio hukumiwa adhabu ya kifo wagoma kula kwa siku 8. soma habari kamili hapa

Kamishna Mkuu wa Magereza, John Minja
Wafungwa  22 wa gereza ya Maweni mkoani Tanga waliohukumiwa kunyongwa kutokana na kukutwa na hatia ya makosa ya mauaji, wamegoma kula kwa siku nane sasa baada ya kuondolewa baadhi ya vyakula na kulishwa chakula cha aina moja ambacho wanadai ni kibovu.


Wafungwa hao wanadai kuwa chakula wanachopewa hakifai ikiwamo maharage yaliyooza na ugali.

Kwa mujibu wa barua kutoka kwa wafungwa hao ambayo mwandishi wetu ameiona, Oktoba 10, mwaka huu Mkuu wa Magereza mkoani humo (RPO), aliwatangazia kwamba serikali haina fedha na kwamba ratiba ya chakula itabadilika.

Barua hiyo imeendelea kueleza kwamba bosi huyo wa magareza aliwatangazia kwamba Serikali (Hazina) haina fedha na fungu la chakula limepungua hivyo kuanzia siku hiyo watapikiwa chakula cha aina moja ugali na maharage.

Aidha, wafungwa hao wakiwamo wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi, walikuwa wakipikiwa chakula tofauti kama vile wali, ugali, nyama, maharage, dagaa, mboga za majani, mayai na maziwa, lakini baada ya tangazo hilo chakula wanachopikiwa ni cha aina moja tu.

“Mkuu huyo alitutangazia kwamba Hazina imetoa theluthi moja kwa hiyo bajeti ni ndogo haitoshi na jeshi linalazimika kubadilisha ratiba ya chakula...Mabadiliko hayo hayakujali wale wanaotumia dawa kali za kurefusha maisha kupata chakula chao maalum chakula kibovu maharage yameoza tumeamua kugoma kula ni siku ya saba leo (jana),” ilisema sehemu ya barua ya wafungwa hao ambayo mwandishi wetu ameiona.

Ikifafanua sehemu ya barua hiyo ilisema kutokana na mgomo huo baadhi yao wamefungiwa kwenye chumba maalum huku wakipigwa na kulazimishwa kusitisha mgomo huo.

“Tunaomba utusaidie kuichapisha taarifa yetu tunanyanyasika sana na tunaiomba serikali kufuatilia ili tupate chakula tunachostahili badala ya kula chakula kibovu,” ilisema sehemu ya barua hiyo kutoka kwa wafungwa hao ambao majina na namba zao mwandishi wetu aliziona lakini kwa sasa inayasitiri.

Hata hivyo, akizungumza na mwandishi wa blogu hii kwa njia ya simu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, Editha Mallya, alithibitisha kuwapo kwa mgomo huo, lakini akasema ni wa siku mbili na siyo nane kama wanavyodai wafungwa hao. “Siku za nyuma walikuwa wanatishia kugoma, lakini walikula chakula kama kawaida,” alisema.


  Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya mwandishi wetu na Mkuu wa magereza wa mkoa wa Tanga:

NIPASHE:  Habari za Jumapili afande, NIPASHE imeona barua ya wafungwa 22 katika gereza la Maweni ambao wanadai kuwa wamegoma kula siku ya nane leo, ni kweli?


Kamishna: Nzuri, Ni kweli kuna wafungwa wamegoma kula, lakini siyo kwa siku nane leo (jana) ni siku ya pili, wasingekuwa hai kama wangegoma kula siku nane.

 Mwandishi wetu: Je, ni kweli kwamba ratiba ya chakula ya awali imebadilishwa na wanakula chakula kibovu?Kamishna: Ni kweli mwandishi, ratiba ya chakula imebadilika kutokana na kupungua fungu la fedha tumepunguza ratiba ya kula wali na nyama kutoka siku nne kwa mwezi hadi siku mbili kwa mwezi, lakini siyo kweli kwamba wanakula chakula kibovu

.Kuna wafungwa kutoka mikoa ya Mwanza, Arusha, Kilimanjaro na Kagera walihamishiwa kwenye gereza hilo wakiwa dhaifu kwa hiyo wakawekewa ratiba ya chakula maalumu kama maziwa, wali, nyama, mayai na viazi kwa muda wa mwezi mmoja hali ilipotengemaa tumewachanganya na wenzao kula chakula cha kawaida ndiyo wameanzisha mgomo wanataka ratiba hiyo iendelee moja kwa moja kwa sababu wao wamehukumiwa kunyongwa.

 Akifafanua zaidi alisema siyo haki wapewe chakula cha daraja la kwanza kwa muwa wao wote wa maisha yao jela wakati wana uwezo wa kula chakula cha kawaida kama wenzao, lakini wameamua kugoma.“Tumewatenga na wenzao tangu waanzishe mgomo huo kwa sababu hata sheria hairuhusu wao peke yao kula chakula cha daraja la kwanza kwa muda wote wa kutumikia adhabu yao,” alisema Mallya kwa msisitizo kwamba wafungwa wote wana haki sawa, lakini bajeti imepungua kwa sasa.

Comments