UGOMVI WA JAJI WEREMA NA DAVID KAFULILA WACHUKUA SURA MPYA BAADA YA WAWILI HAO KUKATAA KUPATANISHWA

Mvutano kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila umechukua sura mpya baada ya mwanasheria huyo kugoma kupatanishwa huku akitishia ‘kumshughulikia’ mbunge huyo. 

 
Ugomvi baina yao uliendelea jana asubuhi nje ya Ukumbi wa Bunge muda mfupi baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuahirisha kikao cha Bunge hadi leo.
 
Licha ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kumwita Jaji Werema na Kafulila akiwataka kupeana mikono kama ishara ya kuzika tofauti zao, Jaji Werema alikataa na nusura amvamie mbunge huyo. 
Wakati akizungumza na mwandishi mara baada ya Bunge kuahirishwa jana, Jaji Werema alikutana uso kwa uso na Kafulila katika Viwanja vya Bunge na kuanza kumlalamikia mbunge huyo kwa kitendo chake cha kumwita mwizi.
 
“Unamuona huyo jana (juzi), aliniita mimi mwizi. Yaani mtu mzima kama mimi naitwa mwizi, kwa kweli sikupendezwa kabisa na kauli yake,” alisema Jaji Werema huku akimfuata Kafulila ambaye alitembea harakaharaka kumkwepa mwanasheria huyo.
 
Jaji Werema alisema juzi alishikwa na jazba baada ya kuitwa mwizi lakini akasema hakuwa na nia ya kumpiga ndani ya Ukumbi wa Bunge.
 
Wakati Jaji Werema akiendelea kumlalamikia Kafulila, alitokea Zungu na kumtaka mwanasheria huyo kumsamehe mbunge huyo...“Mheshimiwa naomba mpeane tu mikono kama ishara ya kusameheana, yale mambo ya jana (juzi) yamekwisha.”
 
Lakini badala ya kukubaliana na ombi la Zungu, Jaji Werema alihamaki huku akitaka tena kumvamia Kafulila... “Mimi nakwambia Kafulila nitakukata kichwa, we subiri tu labda ukiniomba msamaha.”
 
Kafulila naye alijibu mapigo... “Huwezi kunikata kichwa Werema, huwezi, yaani uniue, hapana huwezi tena nakwambia huwezi.” 
Wakati wakiendelea kurushiana maneno, Zungu alikuwa katikati yao, huku akiwasihi wapeane mkono na kusameheana bila mafanikio...“Haya mambo yamekwisha jamani, malizeni tofauti hizi.”
 
Kama vile alijua kuwa kauli ya kuua ilimchanganya Kafulila, Jaji Werema huku akitembea kuelekea katika Jengo la Utawala la Bunge alisema: “Siwezi kukuua kwa maana hiyo unayodhani, maana kufa utakufa kwa mapenzi ya Mungu, ila tutapambana tu, nitakuonyesha.”
 
 Kauli ya Kafulila
Akizungumza baadaye, Kafulila alisema: “Kutokana na hali ilivyo sasa, nimeandika barua Ofisi ya Spika juu ya vitisho nilivyopewa na Jaji Werema, kwanza jana (juzi) alitaka kunivamia pale bungeni na kunipiga, leo (jana) asubuhi amenitishia kuwa atanikata kichwa.”
 
Kafulila alisema barua hiyo pia ataipeleka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa maelezo kuwa siku za hivi karibuni yamekuwa yakitokea matukio ya watu kutekwa, kuteswa na kutupwa porini... “Kwa nafasi yake, Werema anaweza kufanya lolote, hivyo barua hizo zinalenga kueleza alichokusudia kunifanyia.”
 
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alipoulizwa kuhusu mvutano uliotokea juzi bungeni na barua za Kafulila alisema Ofisi ya Bunge haijapata malalamiko yoyote.
 
“Jana sikuwapo bungeni lakini mpaka sasa hakuna malalamiko yoyote yaliyoletwa katika Ofisi ya Bunge. Kama wangeshikana mashati ndani ya Bunge  hilo lingekuwa kosa la kufanya fujo bungeni na adhabu zake zipo wazi,” alisema Joel.

Chanzo  za Ugomvi
Juzi kabla ya kutoa kauli hiyo, Werema alikuwa akitoa ufafanuzi wa muongozo ulioombwa na Kafulila kuhusu fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow iliyokuwa Benki Kuu (BoT), ambazo zimelipwa kampuni ya PAP, inayomiliki mitambo ya Kampuni ya Independent Power limited(IPTL).
 
Werema alisema fedha hizo si za Serikali kama inavyodaiwa na Kafulila kwa kuwa fedha za Serikali hazikai katika akaunti hiyo.
 
Aliendelea kufafanua kuwa taarifa zinazotolewa zinapotosha umma kuwa serikali imetoa fedha kuilipa IPTL, wakati ukweli ni kuwa fedha hizo ziliwekwa katika akaunti hiyo kutokana na misuguano baina ya wanahisa wawili waliokuwa wamiliki wa IPTL. 
 
Werema alibainisha kuwa mmoja wa wanahisa hao, alikuwa akitaka IPTL ifilisiwe huku mwingine akipinga juu ya jambo hilo mpaka walipouza hisa zao na kumaliza mgogoro huo, ambapo Mahakama iliruhusu mali za kampuni hizo zipewe kwa mwanahisa mpya, PAP.
 
Werema alisema kuna watu walileta bungeni  vipeperushi wakidai ni ushahidi kuhusu utoaji wa fedha hizo za akaunti ya Escrow na kuhusisha na rushwa.
 
"Kafulila ni miongoni mwa  wanaoeneza taarifa potofu…, kama ni tuhuma au kuna rushwa itakuja kujulikana, tusubiri uchunguzi wa vyombo husika,” alisema.
 
Wakati akizungumza, Werema alitumia mfano wa kabila la Wanyankole, aliosema kuwa wana usemi unaosema kwamba tumbili hawezi kuamua kesi ya msituni.
 
Kabla ya kufafanua maana ya msemo huo, Kafulila bila kuwasha kipaza sauti alikuwa akipiga kelele kumuita Werema kuwa ni mtuhumiwa hivyo atangaze maslahi yake.
 
“Naomba nisikilize hata kama ni mtuhumiwa nina fursa ya kusikilizwa …nisikilize  wewe tumbili,” alijikuta akisema Werema.
 
Baada ya kusema hivyo, Kafulila hakukubali na yeye bila kuwasha kipaza sauti alisema: “wewe (Werema) ni mwizi tu.”
 
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Zungu alimuomba Jaji Werema kukaa chini ili atoe ufafanuzi, huku Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) na Kafulila wakitaka kuzungumza.
 


Zungu alisema kwa kuwa Bunge lilishaamua kuwa suala hilo lipelekwe Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ni vyema kama Kafulila ana ushahidi wowote, apeleke huko.
 
Baada ya kutoa muongozo huo, ambao ulisitisha malumbano, Mwenyekiti Zungu alisitisha shughuli za Bunge mpaka jioni na kuondoka huku akisindikizwa na makatibu wa Bunge na wapambe kama kawaida.
 
Hatua ya Mwenyekiti wa Bunge kuondoka katika ukumbi baada ya kusitisha shughuli za Bunge, ilimpa fursa Jaji Werema kuweka sawa makabrasha yake na kutoka katika kiti chake, ambapo alionekana kama vile anakwenda kumkabili Kafulila.
 
Wakati hilo likitokea, Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbai (Chadema), alihama katika kiti chake na kukimbilia alipokuwa amekaa Kafulila.
 
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya mawaziri  walimzunguka Jaji Werema kabla hajamfikia Kafulila na Kasulumbai.
 
Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro,  Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Abdullah Juma Saadalla na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene.
 
Nje ya Bunge, Kafulila na Mnyika waliitisha mkutano na waandishi wa habari, ambapo walidai kuwa na ushahidi wa kutuhumu baadhi ya mawaziri kusema uongo bungeni kuhusu fedha hizo za Escrow.

Comments