Ikulu ya rais Somalia yashambuliwa na kundi la Al-Shabab

Kundi la kigaidi la ash-Shabab nchini Somalia, limetekeleza shambulizi dhidi ya ikulu ya rais wa nchi hiyo na kupelekea mtu mmoja kuuawa.


 Mbali na kuthibitisha habari hiyo, afisa usalama wa nchi hiyo Abdur Rahman Muhammad amesema kuwa makombora manne yaliipata ikulu hiyo ya rais huyo wa Somalia mapema leo.

 Kundi la ash-Shabab limetangaza kuhusika na shambulizi hilo. Taarifa iliyotolewa na kundi hilo imesema kama ninavyonukuu: “Tumeshambulia ikulu, na baadhi ya makombora yamefanikiwa kuipata ikulu hiyo.”

 Mwisho wa kunukuu. Polisi imethibitisha tukio hilo na kuahidi kuwachukulia hatua kali wahusika. Hivi karibuni kundi la ash Shabab la Somalia lilisambaza mkanda wa video likitishia kufanya mashambulizi mengine ya kigaidi katika nchi kadhaa ikiwemo Kenya.

 Weledi wa mambo wanasema hatua hiyo kuwa imetokana na hasira za kundi hilo kufuatia kupoteza maeneo mengi liliyokuwa likiyadhibiti yakiwemo yale ya kistratijia nchini Somalia. Kwa hivyo shambulizi la mjini Mogadishu dhidi ya ikulu ya Rais Hassan Sheikh Mohamed, linatoa ujumbe kwamba kundi hilo bado lingali na uwezo nchini Somalia.

Comments