Abiria wa treni 1,200 wakwama
Waziri wa uchukuzi, Harrison Mwakyembe.
Abiria hao ambao walikuwa wakitokea Kigoma kuelekea Dar es Salaam
walifikia mkoani hapa jana saa 5:30 asubuhi jana baada ya kuondoka
Kigoma Jumapili.
Jamiileotz ilishuhudia abiria hao wakiwa katika kituo cha stesheni ya
Dodoma wakirandaranda huku wengine wakitafuta magari kwa ajili ya
kuendelea na safari.
Baadhi yao walisema safari yao ilikuwa na mashaka kutokana na injini ya treni hiyo kuharibika.
Issa Kikolwa alisema: “Leo ni siku ya tatu mpaka sasa tupo Dodoma
wakati tumezoea siku kama ya leo tunakuwa Dar es Salaam…na hapa tulipo
hatujui tutafika lini kwa hali ilivyo”
“Tumeambiwa kuwa tunaweza kuondoka muda ya saa moja…kama hali
itakuwa nzuri, lakini hatuna uhakika na hilo…ila muda mfupi
tumetangaziwa kuwa tuje tujipange kwenye dirisha la kukatia tiketi
tukiwa na tiketi na vitambulisho vyetu na hatujui wanataka kutuambia
nini,” alisema.
Hassan Ayoub, alisema tatizo lilianza kuonekana juzi kati ya maeneo ya Tabora na Igoma baada ya injini za treni kuzima.
“Ilibidi tulale maeneo hayo kuanzia saa saba usiku hadi saa 11
alfajili na kuanza safari hadi kufika hapa, pia tumeambiwa hatuwezi
kuendelea na safari kutokana na reli kujaa maji,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, wamejikuta wakimaliza fedha za kujikimu njiani huku wakilipia huduma za choo na kununua maji.
Saada Ferouz alisema wamepata matatizo makubwa wakiwa njiani kwani
walifika eneo la Isinge treni hiyo iliharibika ikawalazimu kulala eneo
hilo.
Mkuu wa Kituo cha Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) cha Dodoma, Selsus
Roman, aalithibitisha kutokea kwa tatizo hilo na kudai kuwa abiria hao
walitarajia kuondoka jana jioni iwapo eneo hilo litatengamaa.
Alisema abiria hao waliingia jana saa 5:30 asubuhi wakitokea Kigoma
na kuwa walishindwa kuendelea na safari kutokana na maji kujaa kwenye
eneo la Gulwe na Godegode.
“Mvua zilinyesha sana kuanzia Jumapili hadi juzi usiku na eneo hilo
limejaa maji kwa hiyo mafundi wapo huko kwa ajili ya kufanya
matengenezo, hivyo yakikamilika abiria wataendelea na safari leo (jana)
jioni,” alisema.
Roman alisema walipeleka taarifa makao makuu kutokana na suala hilo
na kutakiwa kuwasaidia posho kwa ajili ya chakula ambayo ni Sh. 2,500
kwa kila mmoja.
“Tumewaambia wapange fedha za kujikimu na tumemtaka kila abiria
alete tiketi na kitambulisho chake ndiyo tuwape fedha za kujikimu,”
alisema.

Comments
Post a Comment