Anayedaiwa kuua watu watatu kujeruhi saba kortini
Stanford Richaed
Watu hao ni Rudia Manase, Ezema Lazaro na Sebastian Julius, ambao waliuawa Machi, 8 mwaka huu kwa kuwacharanga mapanga na nondo vichwani.
Mshtakiwa huyo alifikishwa nahakamani jana mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Obadia Bwegoge, kwa kosa la kuwaua watu hao katika kijiji cha Bitale majira ya usiku.
Mshtakiwa wakati anasomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka, Inspekta wa Polisi Amina Kahando, alipiga kelele kwa kusema: “Sitaki kusomewa makesi makesi hapa mnataka kuninyonya damu, niacheni niacheni, mimi makesi makesi ya nini.”
Inspekta Kahando alidai kuwa Machi 8, mwaka huu saa 2:30 usiku katika Kijiji cha Bitale, mshtakiwa aliwaua Rudia Manase, Ezema Lazaro na Sebestian Julius kwa kuwacharanga na mapanga na nondo vichwani, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo ambaye inadaiwa kuwa ana matatizo ya akili, hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji hadi hapo itakapopangwa nas kusikilizwa na Mahakama Kuu.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Bwegoge alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 26, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena na kuamuru mshtakiwa apelekwe mahabusu katika gereza la Bangwe.
Katika hatua nyingine, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk. Leonard Subi, alisema majeruhi wote wanane waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa Maweni wodi namba tano na saba hali zao zinaendelea vizuri.

Comments
Post a Comment