ASKOFU KARDINALI PENGO AUWASHA MOTO
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar
es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo, akifafanua jambo wakati akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.
Katika kauli yake, Pengo amesema kuwa kinachoendelea ni kama mbinu ya kutaka suala hilo lisahaulike au liishe hivi hivi tu bila wahusika kukamatwa.
“Hata Askofu wa Zanzibar hajui kitu, mimi sijui kitu na haijulikani ni watu wangapi waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo la kinyama, jambo ambalo linaonyesha kuwa suala hili linataka kufa kimya kimya,” alisema Kardinali Pengo alipozungumza na waandishi wa habari wakati akitoa salaam za Pasaka mwaka huu.
Moto aliouamsha Pengo unaongeza nguvu katika malalamiko ya umma juu ya kushindwa kwa vyombo vya dola kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wahalifu waliohusika katika matukio ya kuteka, kuwajeruhi na kuwaua baadhi ya watu wakiwamo viongozi wa dini kumeendelea kulalamikiwa.
Katika matukio hayo yaliyofanyika mwaka jana na mwaka huu, hakuna watuhumiwa waliokamatwa na kufikishwa mahakamani.
Mbali na Padri Mushi, viongozi wengine wa dini waliouawa ni Mchungaji wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God, Mathayo Kachila, mkoani Geita na Imamu wa Msikiti wa Mwakaje, eneo la Kitope, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Sheikh Ali Khamis Ali.
Wapo pia waliojeruhiwa akiwamo Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae mjini Zanzibar, aliyejeruhiwa kwa risasi na Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleimani Soraga, aliyemwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.
Wengine waliojeruhiwa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka na Mwenyekiti wa Jukwa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda.
Watu binasi na makundi mbalimbali wamekuwa wakihoji kasi ndogo ya vyombo vya dola ya uchunguzi wa matukio hayo na kuwafikisha mahakamani wahalifu hao.
Kutokana na hali hiyo, Kanisa Katoliki Tanzania nalo limehoji kasi hiyo ndogo na kueleza kuwa linasikitishwa na usiri ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama nchini katika uchunguzi wa kifo cha aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Minara Miwili Mtoni visiwani Zanzibar, Evaristus Mushi.
Kanisa hilo limesema kuwa mpaka sasa vyombo hivyo vimeshindwa kuwekwa wazi kwa Watanzania kuhusu uchunguzi huo ili wajue kilichobainika.
Kardinali Pengo alisema ni jambo la kusikitisha kwa vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini kufanya uchunguzi wa tukio kubwa kama lile, lakini vikashindwa kutoa matokeo yake kwa Watanzania.
Alitoa kauli hiyo baada ya waandishi wa habari kutaka maoni yake juu ya uchunguzi uliofanywa kuhusu tukio hilo ambalo yeye aliliita kuwa lilikuwa la kinyama.
“Nilitegemea baada ya mauaji yale, tungeambiwa ni nani aliyeua na vyombo vya dola vilivyokuwa vinafanya uchunguzi huo vingeweka wazi kila kitu, lakini hilo halikutokea,” alisema Kardinali Pengo.
Kuhusu amani na utulivu nchini, Pengo aliitaka serikali kushiriki kikamilifu kuitafuta kwa kuwa jukumu hilo ni la kwake na haiwezi kulikwepa na kwamba Wakristo wapo tayari kushirikiana nayo.
Alisema njia pekee ya kupata suluhu ya amani nchini ni pande zote yaani serikali, Wakristo na Waislamu kukaa meza moja ya mazungumzo ili kuangalia kiini cha tatizo na kupata ufumbuzi wake.
Alifafanua kuwa Wakristo wameshaanza vikao vyao kwa ajili ya kujadili namna ya kuitunza amani, lakini kwa upande wa serikali na Waislamu hajui kama wameishaanza kufanya hivyo.
“Vyovyote vile itakavyokuwa katika suala la kusaka amani, serikali haiwezi kukwepa, ni lazima ihusike kufanya mazungumzo na pande mbili za dini nchini,” alisema Kardinali Pengo.
Alisema ili mazungumzo ya kweli yaweze kufanyika, ni lazima kila upande uwe tayari kupokea ukweli na kusema ukweli bila kuongeza kitu kingine chochote ambacho siyo ukweli.
Aidha, alisema katika mazungumzo ya kutafuta amani kwa pande zote, lazima kila upande uwe na nia njema na kwamba yakiwapo hayo majadiliano yatakuwa na manufaa kwa taifa na wananchi wake.
Alisema dini zote mbili zimekuwapo nchini kwa muda mrefu bila waumini wake kugombana na kwamba anashindwa kuelewa amani inataka kutoweka kwa sababu gani hivi sasa na kusisitiza kuwa mazungumzo ndiyo njia pekee ya kuirejesha.
Alisisitiza kuwa serikali haipaswi kuacha nchi itawaliwe na wahuni wachache wanaoleta vurugu kwa kisingizio cha dini na kusema kuwa lazima hatua madhubuti zichukuliwe ili kuhakikisha amani inadumishwa.
“Mpaka watu wagombane na mali zao kuharibiwa?” alihoji na kuongeza: “Hatuwezi kuliacha suala hili kwa kuliangalia tu, ni lazima serikali ihusike kikamilifu kupata ufumbuzi wake.”
“Kuna watu wanalihusisha suala hili la ukosefu wa amani na mgogoro wa kidini, ni kwa nini wahusishe na mgogoro wa kidini wakati jambo hili ni la wahuni tu wachache ambao wanalitekeleza kwa maslahi yao au ya wale waliowatuma, hivyo siyo vyema kulihusisha na dini,” alisema Kardinali Pengo ikiwa ni kauli yake ya kwanza baada ya kurejea nchini kutoka Vatican alikokuwa kushiriki mchakato wa uchaguzi wa Papa mpya, Francis I. Akizungumzia madai ya baadhi ya watu kwamba vyombo vya usalama vinahusika kuwadhuru watu, Kardinali Pengo alisema kama suala hilo lipo ni hatari kubwa kwa kuwa jukumu la kulinda amani ni la kwao.
“Kama suala hili likigeuka na kuwa hivi linavyodaiwa kwamba vyombo hivyo vinahusika kuwadhuru watu litakuwa jambo hatari sana,” alisema Kardinali Pengo.
Kuhusu kuwapo tishio la kulipua makanisa katika kipindi cha sikukuu ya Pasaka, Pengo aliitaka serikali kuimarisha ulinzi kwa kuwa hiyo ndiyo kazi yake na kwamba kwa upande wake haogopi hilo badala yake atakwenda kusali kama kawaida na kwamba ni bora afie kanisani kuliko kuogopa kwenda kusali siku hiyo.
Misa ya Pasaka kitaifa mwaka huu itafanyika mkoani Dodoma na mkesha wake katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam utafanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph.
Padri Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi Februari 17, mwaka huu wakati akiwa ndani ya gari lake kwenda kanisani kuongoza misa.
Siku chache baada ya mauaji hayo serikali ilituma timu ya watalaamu kutoka jijini Dar es Salam kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo na Machi 1, mwaka huu kikosi maalum cha upelelezi cha FBI cha Marekani kiliwasili nchini kwa ajili kusaidia kazi hiyo.
Wakati utata wa mauaji hayo ukiwa umegubika taifa, Machi 5, mwaka huu Kibanda akiwa getini kwake Mbezi Juu jijini Dar es Salaam akisubiri kufunguliwa geti, alivamiwa na watu wasiojulikana, wakamteka na kupigwa vibaya, kutobolewa jicho la kushoto na kumjeruhi kichwani. Pia walimwaribu meno yake yote ya mbele; kumkata kidole na jeraha jingine mguuni.
Kibanda kwa sasa anapatiwa matibabu nchini Afrika Kusini, lakini zikiwa zimepita siku 21 tangu wahalifu hao wafanye unyama huo ambao hawakuchukua chochote kwake, huku polisi wakiwa wameunda kikosi cha wapelelezi 12 waliobobea kufanya kazi ya kuwasaka, hakuna kauli yoyote ya polisi juu ya wahusika wa janga hilo.
Kutekwa na kupigwa kwa Kibanda kunafanana kwa karibu sana na alivyofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Steven Ulimboka, mwaka jana. Hadi sasa ameshitakiwa mtu mmoja ambaye anaelezwa kuwa ni raia wa Kenya, huku umma ukiwa na hisia kali ya usanii katika mashitaka hayo
Comments
Post a Comment