Bilal ataka wezi wa maji washughulikiwe
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal
Dk. Bilal, alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam, wakati wa
ziara yake katika Mamlaka ya Majisafi na Majitaka jijini humo (Dawasa).
“Ni wajibu wetu kuhakikisha wale wote wanaotumia maji wanatumia
kwa njia ya halali. Tujitahidi kuwadhibiti hao wagemaji njiani
(wanaojiunganishia maji kwa njia zisizo halali) ili yafike mahali
yanakotakiwa kufika,” alisema Dk. Bilal.
Alisema ni vizuri kuhakikisha miundombinu ya huduma hiyo inatunzwa na kwamba maji yanayopatikana yanakuwa safi na salama.
Pia aliagiza kuharakishwa kwa miradi ya maji ya Kidunda, Mpiji na Mpera kwa kuwa ni ya muhimu.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe,
alimthibitishia Makamu wa Rais, kuwa wizara yake imeshachukua hatua za
kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba mpaka sasa tayari kiasi
cha fedha kimeshapatikana.
Alisema Sh. takribani bilioni 27 zinahitajika hadi kukamilika kwa miradi hiyo mitatu ya maji.
Akizungumzia hali ya rasilimali ya maji nchini, Profesa Maghembe,
alisema kuwa kiasi cha rasilimali kimepungua kutokana na kiwango kidogo
cha mvua zilizonyesha kati ya Novemba mwaka jana hadi mwaka huu.
Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na hali hiyo ni mabonde ya maji ya
mito Wami/Ruvu, maziwa ya Tanganyika na Nyasa huku mabonde ya Ziwa
Viktoria na Bwawa la Mtera vikibaki katika hali ya kawaida.

Comments
Post a Comment