Dawa za kulevya zawatokea puani maofisa wa polisi

  Watatu wasimamishwa kazi, wapo wengine watatu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi
Kwa zaidi ya miaka miwili baada ya blogu hii jamiileotz  kuripoti kuwako kwa mchezo mchafu ndani ya Jeshi la Polisi kwa baadhi ya maofisa kuchakachua shehena ya dawa za kulevya aina ya cocaine iliyokamatwa katika mpaka wa Tunduma kati ya Tanzania na Zambia, hatimaye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, ameamua kuchukua hatua baada ya kubainika kwa ‘uharamia’ wa kutisha unaofanywa na maofisa wa polisi mkoani Mbeya
.

Maambuzi ya Dk. Nchimbi aliyotangza jana ni sehemu ya kuwawajibisha maofisa wa polisi waandamizi sita ambao wamehusika katika kashfa nzito za kudai rushwa, kubambika wananchi kesi, kudai fedha ili kutoa ajira na kuiba dawa za kulevya ambazo zilikuwa ni kilelezo katika kesi ya kusafirisha dawa hizo nchini.

  JAMIILEOTZkwa mara ya kwanza Januari 17, 2011 iliripoti tukio la kutatanisha la kuwako kwa udanganyifu wa kutisha ndani ya Jeshi la Polisi kwa baadhi ya maofisa kula njama za kuiba kiasi cha kilo nane cha dawa za kulevya kati ya kilo 42.5 ambazo zilikamatwa mpakani Tunduma zikisafirishwa kwenda Afrika Kusini.

Dawa hizo zikiwa kwenye gari aina ya Nissan Hard Board pick up lenye namba za usajili CA 508-650 likiendeshwa na Vuyo Jack (29) akiwa na mwanamke mwenye asili ya Asia, Anastacia Cloete (25) wakitoka Dar es Salaam.

Watuhumiwa hao walikamatwa Novemba 18 mwaka 2010, wakati wa upimaji wa mzigo huo ilibainika kuwapo kwa cocaine paketi 26 zenye uzito wa kilo 28.5, Heroin paketi 3 za uzito wa kilo 3.5 na Morphine paketi 8 za uzito wa kilo 10.75. Dawa hizo zilikuwa zimefichwa kwenye sehemu ya ndani ya gari hilo baada ya kufuguliwa bodi.

Waliosimamishwa kazi ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Mkoa wa Mbeya, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Elias Mwita na Msaidizi wake, Mrakibu wa Polisi (SP) Jacob Kiango.

Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa huo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Kinyongo na aliyekuwa RCO Mkoa wa Kagera, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Peter Matagi.

Yumo pia Ofisa aliyekuwa anasimamia ajira ya jeshi hilo, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP) Renatus Chalamila; na aliyekuwa Mkuu wa Polisi (OCD) Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Paul Mng’ong’o. Mng’ong’o na wenzake wamekwisha kufikishwa mahakamani.

Dk. Nchimbi alitangaza uamuzi huo, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, baada ya timu kadhaa zilizoundwa mwaka jana kuchunguza tuhuma zinazowakabili maofisa hao waaandamizi wa jeshi hilo.

Alisema utekelezaji wa hatua hiyo ulianza rasmi jana na kwamba tayari amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, kuwafungulia maofisa hao mashtaka ya kijeshi kabla ya kufikishwa kwenye mahakama ya kiraia kujibu tuhuma zinazowakabili.

Waziri Nchimbi alisema kati ya maofisa hao wa Polisi, watatu wamesimamishwa kazi kwa tuhuma ya kuhusika na upotevu wa kilo 1.9 ya dawa za kulevya aina ya “Cocaine” katika mazingira ya kutatanisha.

Alisema mwingine amesimamishwa kazi kwa tuhuma ya kupiga na kuwabambikia wananchi kesi zisizo na dhamana kutokana na rushwa na mwingine kwa tuhuma za kudai na kujipatia fedha kutokana na ajira ya Polisi.

Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, ofisa mwingine amesimamishwa kazi kwa tuhuma ya kuingia kwenye hifadhi za mbunga ya wanyama ya Serengeti na kupanga njama ya kuchimba madini aina ya dhahabu ndani ya hifadhi hiyo.

Aliwataja wanaotuhumiwa kuhusika na upotevu wa dawa hizo katika mazingira ya kutatanisha kuwa ni SSP Mwita, SP Kiango na ASP Kinyongo. 

Anayetuhumiwa kupiga na kuwabambikia wananchi kesi zisizo na dhamana kutokana na rushwa, alimtaja kuwa ni SSP Matagi.

Pia anayetuhumiwa kudai na kujipatia fedha kutokana na ajira ya Polisi, alimtaja kuwa ni SACP Chalamila.

Anayetuhumiwa kuingia kwenye hifadhi za mbuga ya wanyama Serengeti na kupanga njama ya kuchimba madini aina ya dhahabu ndani ya hifadhi hiyo, alimtaja kuwa ni SSP Mng’ong’o.
Dk. Nchimbi alisema dawa hizo ambazo zilipotea baada ya kufikishwa Polisi mjini Mbeya, zilikamatwa na askari wadogo wa jeshi hilo katika mpaka wa Tunduma mkoani humo, mwaka jana.

Alisema baada ya kukamatwa zilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, jijini Dar es Salaam ili kuthibitisha kama ni dawa halisi za kulevya au la.

Hata hivyo, alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida, mzigo ulipofikishwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, ikabainika kilichopelekwa na askari wadogo kwa mabosi wao sicho kilichokamatwa.

“Walipeleka (kwa Mkemia Mkuu wa Serikali) sukari na chumvi, badala ya dawa zilizokamatwa,” alisema Dk. Nchimbi.

Kutokana na utata huo, Dk. Nchimbi alisema serikali iliunda timu kwa ajili ya kuchunguza sakata hilo.

Alisema katika uchunguzi huo, ilibainika kuwa kulikuwa na mchezo mchafu uliofanywa na maofisa hao wa ngazi za juu wa Polisi.

Dk. Nchimbi alisema katika ripoti yake, timu hiyo ilisema kilichofanywa na maofisa hao waandamizi wa Polisi kililenga kuwapunguzia askari hao wadogo ari ya kufanya kazi.

Kutokana na hilo, alisema katika ripoti yake, timu hiyo ya uchunguzi pamoja na mambo mengine ikapendekeza vigogo hao wa jeshi hilo wasimamishwe kazi.

Kuhusu aliyesimamishwa kazi kwa tuhuma ya kupiga na kuwabambikia wananchi kesi zisizo na dhamana kutokana na rushwa, Dk. Nchimbi alisema afisa huyo alikumbwa na tuhuma hiyo baada ya kuwapo mtu aliyekuwa akimiliki ekari 4,000 za shamba mkoani Kagera.

Alisema kwa mujibu wa sheria, hairuhusiwi mtu kumiliki ekari nyingi za shamba kiasi hicho peke yake, lazima awe amepewa na Rais.

Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, kutokana na hali hiyo, wananchi walianza kumlalamikia mtu huyo kumiliki eneo hilo peke yake na bila kuliendeleza huku wengi wao wakiachwa wakiwa na shida ya ardhi.

Alisema malalamiko ya wananchi hao yalikwenda mbali zaidi hadi walipoamua kuvamia eneo hilo na kulitwaa kwa nguvu.

Dk. Nchimbi alisema kuona hivyo, ofisa huyo wa Polisi aliwakamata vijana 14 na kuwafungulia kesi ya ujambazi sugu, huku akidai kwamba ni watu waliokuwa wakitafutwa muda mrefu kwa tuhuma hizo.

Alisema vijana hao walishikiliwa mahabusu kwa miezi miwili mfululizo bila ya kupewa dhamana licha ya kesi yao kufutwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Dk. Nchimbni alisema alipopata habari, alifuatilia suala hilo na kugundua kuwa vijana hao hawakuwa majambazi, bali walibambikiwa kesi hiyo.

Alisema pia aligundua na kujiridhisha kuwa vijana hao waliponzwa kutokana na kugombea eneo hilo, hivyo, akaifuta kesi ya ujambazi waliyofunguliwa.

Dk. Nchimbi alisema baadaye iligundulika kuwa ofisa huyo wa Polisi alikuwa amekula njama na mtu huyo aliyekuwa akimiliki eneo hilo ili awafungulie kesi wananchi hao.
Dk. Nchimbi lisema ofisa huyo wa Polisi na mtu huyo walikula njama hizo ili kuwaziba midomo wananchi hao wasiendelee kupigia kelele dhidi ya umiliki wa eneo hilo.

Kuhusu ofisa wa Polisi anayetuhumiwa kudai na kujipatia fedha kutokana na ajira ya Polisi, alisema kuwa alikuwa anawaambia watu kuwa anao uwezo wa kuwaingiza kwenye jeshi.

Dk. Nchimbi alisema baada ya kuwa anawaambia hivyo, alikuwa pia akiwataka wampe fedha kwa ajili hiyo.

Alisema vijana wengi wamekuwa wakilalamika na wengine wakimfuata hadi wizarani wakidai kuwa kazi hawajapata licha ya baadhi yao kumpa ofisa huyo wa Polisi Sh. milioni moja ili awape ajira jeshini.

Kutokana na malalamiko hayo kukithiri, Dk. Nchimbi alisema serikali haiwezi kuendelea kuvumilia, hivyo kutokana na uzito wa jambo hilo, kwa mamlaka aliyonayo ameamua kumsimamisha kazi.

Alisema zaidi ya hivyo, angependa kumwajibisha, lakini kutokana na ngazi aliyonayo ofisa huyo, mamlaka yake (Waziri Nchimbi) hayamruhusu kufanya hivyo.

Hata hivyo, alisema tayari amekwisha kumwandikia Rais Jakaya Kikwete barua kumshauri amwajibishe na kwamba, amesimamishwa kwa mwezi mmoja wakati yakisubiriwa majibu ya Rais.

Comments

Popular Posts