DK.SHEIN AWACHANA WAISLAMU LAIVU KWENYE MAULIDI

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema hatavumilia kuona baadhi ya watu wanafanya vitendo vya chokochoko za kidini kwa nia ya kutaka kugawanya Watanzania.
Akizungumza kwenye Maulidi ya kuzaliwa Mtume Mohamad (SAW) katika Msikiti wa Majumuiyat wa Temeke jijini Dar es Salaam juzi, Dk Shein alisema mgawanyiko kati ya Watanzania ni kitu kisichokubalika daima.
Kwenye sherehe hiyo iliyoandaliwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum, ilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na viongozi mbalimbali.
Dk. Shein alisema msingi wa dini ya kiislamu ni usawa wa binadamu kwa kila mmoja kumpenda mwenzake, ni kosa kubwa kutumia dini kwa kudhulumu maisha ya mtu au mali zake.
Aliwasisitizia waumini hao warudi kwenye dini na kuangalia misingi yake pamoja na hadithi za Mtume (SAW).
Alisema Zanzibar ina historia kubwa ya watu wa dini zote kuishi kwa pamoja kama ndugu na yaliyotokea kwa viongozi wa dini kuuawa ni matukio mageni yanayotakiwa kuondolewa haraka.
Awali mlezi wa msikiti huo, Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi alisema lazima Watanzania walinde amani yao iliyodumu kwa miaka mingi.
Alitahadharisha endapo waumini wa kiislamu wakitaka kuwadhuru wakristo kwa namna yoyote, na wakristo nao wakawa na nia kama hiyo, nchi haitakuwa salama na hakuna atakayefurahia maisha.
"Tanzania ni ya sisi sote, ndani tupo wa dini na makabila mbalimbali, hivyo inatulazimu tupendane na kuishi kwa pamoja kulinda utamaduni wetu wa upendo," alisisitiza mzee Mwinyi.
Kwa upande wa Sheikh Majid Salehe, alisema wanasiasa waepuke kuwajaza watu maneno ya uongo na kusababisha maandamano na kuchukia serikali yao.
Sheikh huyo aliongeza kwamba endapo wanasiasa wakitumia njia hiyo watakuwa wanakwenda kinyume na matakwa ya dini na itasababisha nchi kukosa amani.
Alipongeza hatua ya Sheikh ya mkoa kutetea kwa nguvu zote suala zima la amani, kitendo hicho ni kufuata kwa vitendo mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Hata hivyo, Alhaji Salum ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam, aliwatunuku watu mbalimbali vyeti vya kutambua mchango wao wa kulinda amani nchini.
Waliotunukiwa vyeti hivyo ni Dk. Mengi, Lowassa, Waziri Nahodha, Waziri wa Viwanda, Dk. Abdallah Kigoda na Mkuu wa Mkoa wa Said Meck Sadick

Comments

Popular Posts