Hatma kama Sheikh Ponda ana kesi ya kujibu au la leo

Sheikh Ponda Issa Ponda
Hatma ya kesi inayomkabili Sheikh Ponda Issa Ponda (54) na wenzake 49 ya kula njama, kuingia, kujimilikisha ardhi kwa jinai, wizi wa mali ya Sh. milioni 59.6 kama wana kesi ya kujibu au la, itajulikana leo.

Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hatua hiyo imefikiwa kufuatia mawakili wa pande zote mbili kutoa hoja za kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya upande wa Jamhuri kuita mashahidi 17 dhidi ya washtakiwa.

Mbali na Ponda, baadhi ya washtakiwa wengine ni Sheikh Mukadam Saleh, Kuluthumu Mohamed, Zaldah Yusuph, Juma Mpanga, Farida Lukoko, Adamu Makilika, Athum Salim, Seleman Wajumbe, Salum Juma, Salum Mkwasu na Ramha Hamza.

Upande wa mashitaka ulidai kuwa katika shitaka la kwanza, Oktoba 12, mwaka huu, eneo la Temeke, washtakiwa wote 50 walikula njama za kutenda makosa.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza, eneo la Chang’ombe Markas, wilaya ya Temeke, washtakiwa wote 50 kwa jinai walivamia   kwa nia ya kutaka kujimilikisha kiwanja mali ya Agritanza Ltd.

Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu, eneo la Chang’ombe Markas, pasipo uhalali na hali ya uvunjifu wa amani, washtakiwa wote kwa pamoja walijimilikisha ardhi ambayo ni mali ya Agritanza Ltd.

Shitaka la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu, Chang’ombe Markas, washtakiwa wote kwa pamoja waliiba vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwemo matofali 1,500, tani 36 za kokoto na nondo vyote vikiwa na thamani ya Sh. 59,650,000 mali ya Agritanza Ltd.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa katika shitaka la tano linamkabili Sheikh Ponda na Mkadam, kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu, eneo la Chang’ombe Markas, wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania, aliwashawishi wafuasi wake kutenda makosa ya jinai.

Washtakiwa wote walikana mashitaka yao kwa nyakati tofauti.

Oktoba 18, mwaka jana, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka yao, lakini Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), aliwasilisha hati ya kiapo cha kupinga dhamana ya Sheik Ponda na Mukadam kwa usalama wake na maslahi ya taifa

Comments

Popular Posts