Hofu ya ufisadi yatanda hospitali ya wilaya Manyoni
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, ubadhirifu huo ni wa muda
mrefu, jambo linalosababisha hospitali hiyo kukosa hadhi ya ngazi ya
wilaya.
Taarifa zaidi zinadai kuwa, madaktari na manesi katika hospitali
hiyo, wameshakutana mwishoni mwa mwaka uliopita, kujadili changamoto
zinazowakabili, ikiwemo upotevu wa fedha zinazotolewa kwa ajili ya
uboreshai huduma za afya.
Ilidaiwa kuwa ufisadi unaofanyika hospitalini hapo umesababisha upungufu kadhaa ikiwemo ukosefu wa vitendea kazi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya gazeti hili, kiasi cha Shilingi milioni 26
kutoka serikalini, zinatolewa kila mwezi hospitalini hapo, lakini
‘zinaishia’ mifukoni mwa watumishi wasiokuwa waminifu.
Mmoja wa madaktari (jina limehifadhiwa) alisema miongoni mwa vifaa
muhimu vinavyokosekana hospitalini hapo ni mashine ya oxygen, hivyo
kusababisha wagonjwa wengi wakiwemo watoto wanaozaliwa kabla ya muda
wao, kupoteza maisha.
Alivitaja vifaa vingine ni vipimo vya shinikizo la damu, joto la
mwili na ultrasound, hivyo kusababisha wagonjwa kwenda katika hospitali
ya mkoa wa Dodoma.
Chanzo chetu kilienza kuwa hospitali hiyo haina daktari bingwa wala
utaratibu kupima wagonjwa wodini unaotakiwa kufanywa mara mbili au tatu
kwa siku, kulingana na afya ya mgonjwa.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Jackson Kitundu, alithibitisha kuwepo upungufu huo ikiwemo kutokuwepo ultrasound.
Pia alisema mashine nyingine kama ya oxgen, wanasubiri mgawo kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Dk Kitundu alisema madai ya Shilingi milioni 26 zinazodaiwa
kufanyiwa ufisadi hospitalini hayana ukweli, kwa vile fedha
zinazotambulika ni Shilingi milioni 13.

Comments
Post a Comment