Kanisa Moravian lalaani kushambuliwa Kibanda
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda
Mwenyekiti wa Jimbo hilo, Mchungaji Clement Mwaitebele, alitoa msimamo huo alipozungumza na Jamiileotz kwa njia ya simu kutoka Dodoma ambako viongozi makanisa yaliyo chini ya CCT, wanaendelea na vikao vyao vya maamuzi
.
Alisema Kanisa limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hiyo, lakini pia likaona vyema jamii kupewa msimamo badala ya kukaa kimya kana kwamba kanisa hilo nalo limefurahishwa na jambo hilo la kinyama.
Mchungaji Mwaitebele, alisema Kanisa limelazimika kuchukua hatua hiyo ya kulaani, lakini pia kuvishauri vyombo vya ulinzi kuacha kufumbia macho dalili za aina yeyote ya uovu unaoanzishwa na makundi ya watu ndani ya makanisa au nyumba nyingine za ibada.
“Kibanda ni Mwenyekiti wa Jukwaa huru la waandishi wa habari Tanzania, lakini unyama aliotendewa ni mbaya na haustahili kutufanya tubaki kimya kwa sababu zozote, hivyo ni vyema kutumia nafasi hii kutuma salamu kwa waliohusika kwa namna moja na ufadhili wa jambo hilo,” alisema Mchungaji Mwaitebele.
Alisema waumini wa kanisa hilo nchini kote wanamtakia Kibanda matibabu mema na apone haraka na kuendelea na wajibu wake katika kipindi hiki ambacho Taifa linabakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii.
“Tumeamua kutenga siku maalum kwa ajili ya kumuombea kijana wetu, maana haya yaliyotokea ni majaribu na ambayo msingi wake ni uwajibikaji, lakini tunawatia nguvu na kuwaomba wamuachie Mungu ajibu kilio chenu,” alisema.

Comments
Post a Comment