Kesi ya kina Ponda yaibua mapya

Sheikh Ponda Issa Ponda
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imeambiwa na Shahidi wa 21, Salma Abdulraatifu (34), katika kesi inayowakabili Sheikh Ponda Issa Ponda (54) na wenzake 49, kwamba askari waliwatukana matusi na kumnyima kwenda kuchukua pochi yake  iliyokuwa na Sh. 780,000.
 
Shahidi huyo alitoa madai hayo jana alipokuwa anatoa utetezi wake mbele ya Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Victoria Nongwa.
 
Salma alidai kuwa askari hao walivunja mlango mkubwa na kuingia msikitini na kuwakuta wanaume wanaswali, mmoja akasema ndani kuna watu wengine ambao walikuwa wanawake wakaamriwa kutoka.
 
Alidai watu hao walijitambulisha kuwa ni askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) wakawaamuru kunyoosha mikono juu.
 
‘’Walitutukana matusi pamoja na kutukebehi, nikawaomba kwenda kuchukua pochi yangu niliyokuwa nimeisahau ndani ambayo iliyokuwa na Shilingi 780,000 wakaniambia hakuna ruhusa,” alidai.
 
Naye shahidi wa 22, Said Rashid alidai kuwa siku ya tukio alikuwa kwenye Msikiti uliopo kiwanja cha Marcus Chang’ombe na hatambui shtaka linalomkabili wala halifahamu Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata).
 
 
Mashahidi kumi walitoa utetezi wao mahakamani hapo na kufanya jumla ya washahidi waliotoa ushahidi kufika 27.
Ushahidi unaendelea leo.
 
Upande wa wa mashtaka ulidai kuwa katika shtaka la kwanza, Oktoba 12, mwaka huu huko Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 50 walikula njama ya kutenda makosa.
 
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza katika eneo la Chang’ombe Markas, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 50 kwa jinai walivamia   kwa nia ya kutaka kujimilikisha kiwanja mali ya Agritanza Ltd.
 
Katika shtaka la pili, Ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka jana eneo la Chang’ombe Markas pasipo uhalali na hali ya uvunjifu wa amani washtakiwa wote kwa pamoja walijimilikisha ardhi ambayo ni mali ya Agritanza Ltd.
 
Shtaka la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka jana katika eneo hilo, washtakiwa waliiba vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwemo matofali 1,500, tani 36 za kokoto na nondo vyote vikiwa na thamani ya Sh. 59,650,000 mali ya Agritanza Ltd. Wote walikana mashitaka hayo.

Comments

Popular Posts