Kibanda afanyiwa upasuaji Madaktari washindwa kuokoa jicho
Mwenyekiti
wa TEF, Absalom Kibanda amefanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini na
taarifa kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006)
Ltd, Hussein Bashe inasema Kibanda ameshatoka kwenye chumba cha
upasuaji.
Hata hivyo, taarifa mbaya ni kwamba Madaktari wameshindwa kuokoa jicho lake la kushoto na kuamua kuling’oa.
"Wamechukua hatua hiyo ya kitatibu baada
ya kuwa tayari jicho hilo lilikuwa limepondeka kwa ndani hivyo
lisingeweza tena kuona. Atawekewa jicho la bandia la plastiki ambalo
hata hivyo halitakuwa likiona," ilisema taarifa hiyo
.
Upasuaji huo uliochukua saa 5 na dakika 30
umefanyika kwa ufanisi mkubwa na ulikuwa ukiongozwa na madaktari bingwa
watatu. Wawili kati yao ni wataalamu wa kichwa na mmoja ni mtaalamu wa
macho.
Taarifa imeongeza kuwa katika upasuaji
huo, hakukuwa na madhara ya ndani katika kichwa chake, hivyo kichwa kiko
salama. Sura yake imejengwa upya kutokana na majeraha ambayo yalikuwa
yametapakaa baada ya kupigwa.
Changamoto kubwa waliyokutana nayo
madaktari waliomfanyia upasuaji ni kurejesha katika sehemu yake baadhi
mifumo midogo inayozunguka jicho pia kurejesha taya la kushoto ambalo
lilikuwa limeathiriwa na tukio la kupigwa kwake jambo ambalo
limefanikiwa.
Ripoti kamili kuhusu upasuaji huo inatarajiwa kutolewa leo na madaktari hao.

Comments
Post a Comment