Majambazi wateka Hiace,wawavua nguo abiria

IGP Said Mwema, Mkuu wa jeshi la Polisi.
Majambazi yasiyojulikana yamevamia basi dogo la abiria aina ya Hiace katika kijiji cha Kishanga, wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma na kuwavua nguo abiria kisha kupora simu, fedha na mabegi.
 
Majambazi hao pia walimjeruhi kondakta wa Hiace hiyo, George Athoni (37) kwa kumpiga risasi katika miguu yote na kutokomea kusikojulikana.
 
Tukio hilo lilitokea jana saa moja asubuhi katika pori lililoko katika kijiji cha Kishanga wakati gari hilo likisafiri kuelekea mjini Kigoma.
Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kigoma, Dismas Kisusi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa gari hilo lilikuwa linaendeshwa na Nuru Juma likiwa na abiria 16.
 
Alisema gari hilo lilipofika katika pori  katikati ya vijiji vya  Kishanga na Kalera, ghafla kulitokea mlio wa risasi na kupiga kwenye mlango wa kuingilia abiria.
 
Alisema kutokana na hali hiyo, dereva alisimamamisha gari na majambazi hao wakaingia na kuanza kuwavua nguo abiria kisha kupora mabegi, simu, fedha na kutokomea kusikojulikana.
 
Mkuu huyo wa upelelezi alisema polisi wanaendelea na msako wa kuwasaka majambazi hao ili sheria ichukue mkondo wake.
 
Akizungumza na Jamiileotz akiwa amelazwa wodi namba saba katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Mawemi, kondakta Athoni, alisema walipakia abiria 16 katika gari hilo kutoka kijiji cha Kashanga kuelekea mjini Kigoma majira ya asubuhi.
 
 “Tulipofika katika pori lililopo katikati ya vijiji vya Kashanga na Kalera ghafla tulisikia mlio wa risasi na risasi kupiga mlango wa kuingilia abiria na dereva akasimamisha gari,” alisema.
 
Athoni alisema kuwa baada ya dereva kusimamisha gari,  ghafla majambazi watatu waliokuwa wamevalia majaketi meusi kama ninja wakiwa na bunduki waliingia kwenye gari na kuamuru abiria wote wavue nguo zote na kuanza kukusanya mabegi, nguo walizovua, simu na fedha.
 
Alisema kuwa majambazi hao walimpiga risasi kutokana na kukaidi amri ya kuvua nguo na kwamba baada ya kumpiga risasi katika miguu yote miwili, walimpora Sh. 250,000 alizokuwa nazo kwenye bukta aliyokuwa amevalia ndani ya suruali yake.
 
Aliendelea kusimiliwa kuwa, wakati anapigwa risasi na kuvuliwa nguo, abiria wote walikuwa wamelazwa kifudifudi.
 
Kondakta huyo alisema baada ya muda, majambazi hao waliwaamsha abiria na kuwaamuru waingie ndani ya gari na baadaye kumuamuru dereva aendeshe kuendelea na safari huku wakiwa uchi wa mnyama. 
 
Athoni alisema kuwa majambazi waliacha ndani ya gari nguo zilizochakaa na abiria kuamua kuzivaa na walipofika katika kijiji cha Kalera ndipo walipokutana na polisi na kuwaeleza kuwa walikuwa wamevamiwa na kuporwa.
 
 Kwa mujibu wa kondakta huyo, polisi walielekea katika eneo la tukio na abiria kuendelea na safari hadi kituo cha polisi kati.
 
Alisema kuwa baada ya kufika kituo cha polisi alipewa fomu ya PF3 na kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa Maweni kwa matibabu.
 
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk. Leonard Subi, alithibitisha kupokea majeruhi huyo ambaye alipigwa risasi miguu yote miwili na kwamba amelezwa katika wodi namba saba

Comments

Popular Posts