Mapya yagundulika majeraha ya Kibanda

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda
Wakati Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetangaza bingo ya Sh. milioni tano kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kuwatia mbaroni watu waliomvamia na kumjeruhi Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, habari mpya kutoka Afrika Kusini anakopatiwa matibabu zinasema madhara mengine mapya yamegundulika mwilini mwake.

Taarifa zilizopatikana kutoka hospitali ya Millpark, Johannesburg alikolazwa zinasema kuwa uchunguzi wa Tscan aliofanyiwa Kibanda umegundua kuwa mfupa wa fizi kati ya mdomo na pua nao umevunjika.

Kuvunjika kwa mfupa huo, mbali ya kumuongezea maumivu na adha kubwa Kibanda, pia unathibitisha nguvu kubwa iliyotumika kulazimisha kung’oa meno yake kwa ukatili mkubwa. 

Kibanda alivamiwa na watu wasiojulikana wakati anajiandaa kufunguliwa lango la kuingia nyumbani kwake Mbezi Beach jijini Dar es Salaam juzi na kumjeruhi sehemu kadhaa za mwili wake na kisha kumng’oa meno, kucha na kuna hisia kwamba jicho lake la kushoto limetobolewa.

Pia Kibanda amejeruhiwa kichwani ambako amshonwa nyuzi kadhaa katika majeraha matatu.

Taarifa kuhusu maendeleo ya afya ya Kibanda ambayo ilisambazwa na Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, ilisama kuwa aliwasili salama Afrika kusini kwa ajili ya matibabu.

Meena alisema kuwa jana Kibanda alifanyiwa vipimo mbalimbali, na kwamba majibu ya vipimo hivyo yamekwishatoka.

Meena alifafanua kuwa kwa mujibu wa taratibu za hospitali hiyo, majibu ya vipimo hivyo yalitakiwa kusomwa na wataalamu wa hospitali hiyo ambao walitarajiwa kuyaangalia kwanza, ili kuamua jinsi ya kutoa tiba.

“Kwa kweli Kibanda anaendelea vizuri, kwani sasa anaweza kuongea ingawa bado anaonekana kuwa anasikia maumivu makali,” alisema Meena akikariri habari kutoka Afrika Kusini.

Meena aliendelea kufafanua kuwa unafanyika utaratibu kati ya TEF na wanafamilia ya Kibanda kuhusiana na jinsi ya kurahisisha mawasiliano  kuhusu maendeleo yake zitakavyokuwa zinatolewa ili wananchi wapate taarifa sahihi.

Aidha, Meena alisema kuwa TEF itakutana leo pamoja na mambo mengine, kuangalia jinsi Jukwaa litakavyoshiriki katika kutoa mchango wake wa matibabu ya Kibanda.

Akizungumzia bingo ya kufanikisha kukamatwa kwa waliotenda unyama dhidi ya Kibanda, Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman  Kova, aliwaomba wananchi kushirikiana na jeshi hilo kutoa taarifa za waliohusika na tukio hilo la kinyama dhidi ya Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New habari (2006 LTD) ili kuharakisha upelelezi.

“Tunaomba ushirikiano wa wananchi kufanikisha upelelezi wa tukio hili, tunataka zoezi la upelelezi lifanyike haraka na ndiyo maana tumeamua kutoa ofa. Hatutamtaja yule atakayetupa taarifa za watu waliohusika,” alisema Kova.

Aidha, Kamanda Kova alisema kuwa tayari timu ya maofisa 12 waliobobea katika upelelezi ambao wameteuliwa kupeleleza tukio hilo, walianza kazi rasmi jana
Wakati huo huo, Chama cha Waandishi wa Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (Misa-tan), kimelaani vikali tukio hilo la kinyama kwa maelezo kwamba ni mwendelezo wa yale yaliyoanza kutokea nyuma kwa lengo la kuzuia uhuru wa habari nchini.

Mkurugenzi wa Misa-tan, Tumaini Mwailenge, alisema hawakubaliani na kitendo hicho kwani ni cha kinyama na kwamba kinalenga kufunga midomo ya waandishi wa nabari ili wasifichue vitendo vya  kifisadi.

“Tunapinga kitendo hiki kwani  hakikubaliki, huu ni mwendelezo wa vitendo vya zamani vinavyolenga kufunga midomo ya waandishi wa habari wasivifichue vitendo vya ufisadi,” alisema na kuongezeza:



Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani vikali tukio hilo na kuitaka serikali kuhakikishia ulinzi wananchi wake, kwani kwa sasa wanaotenda masuala hayo wanaonekana kuwa na nguvu kuliko vyombo vya dola.

Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema tukio la kumshambulia na kumjeruhi Kibanda linafanana na la Mwenyekiti wa Jumuiya ya madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, na kwamba ni jambo linalotia shaka kuwa watendaji ni wale wale waliomtendea unyama daktari huyo.

Alisema kitendo hicho ni cha kinyama na hakikustahili kutendewa binadamu yeyote hata kama ana makosa na hakikustahili kutendwa na binadamu yeyote mwenye kuheshimu utu wa mwingine.

“Katika nchi huru kama Tanzania, sasa inaonekana matukio haya ni ya kawaida, tunaitaka serikali kuwahakikishia usalama wananchi wake…Kibanda alikuwa na maadui wengi kutokana na kazi yake, anafichua maovu ya vigogo mbalimbali bila woga,” alisema.

Aidha, alisema kama serikali haihusiki kwa namna yeyote ni vyema ikafanya uchunguzi wa haki na kuchukua hatua stahili na siyo kupiga danadana kama ilivyokuwa kwenye tukio la Dk. Ulimboka.

 “Hali ni tete sana, kitakachoondoa hofu za wananchi ni serikali kufanya uchunguzi wa haki, ni lazima ifanye wananchi waishi kwa amani, mfanano wa matukio haya unaendelea kutia shaka kuwa watendaji wana nguvu na wataendelea kufanya watakavyo pale maslahi yao yanapogushwa,” alisema.


Katibu wa Klabu ya  Waandishi wa Habari Kanda ya Kati (CPC), Habel Chidawali, alisema tukio hilo linawajengea mazingira ya hofu waandishi wa habari hata kwa wale watu ambao wanawafahamu.

“Tukio hilo linajenga mazingira hofu kwa waandishi wa habari hata kwa watu…lakini tunahitaji kutenda kazi kwa uangalifu mkubwa,” alisema Chidawali.

Alisema waandishi wa habari hawatakiwi kurudi nyuma kwa sababu kufanya hivyo ni kuwasaliti wale ambao damu zao zimemwagika wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kawaida.

Naye Wakili wa kujitegemea mjini Dodoma, Elias Machibya, alisema anaamini kuwa tukio hilo lilipangwa na watu kutokana na utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.

Alisema kitendo hicho ni kinyume cha Katiba ambayo inatamka kila mtu ana uhuru wa kutoa na kupata habari.

 “Haki ya kupata habari ni ya Kikatiba, serikali ichukue hatua itakayokomesha matukio haya ili wananchi wawe na imani,” alisema
Viongozi wakuu wa vyama vya siasa vyenye wabunge bungeni, wamelaani vikali imelaani kitendo hicho.

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia, alisema viongozi hao walipokea kwa mshtuko mkubwa taarifa hizo.

Mbatia alisema viongozi hao walivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka wa tukio hilo ili wahusika wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.

Pia alisema wameitaka serikali kuwa makini zaidi kukomesha matukio ya namna hiyo ambayo yameanza kushamiri nchini kwa kuwa yanajenga wasiwasi, chuki, uhasama na hasira miongoni mwa raia ikiwamo kuhatarisha usalama na amani ya nchi.

Chama cha Wananchi (CUF), Kimelaani vikali kitendo alichofanyiwa Kibanda, na kulitaka Jeshi la Polisi na serikali kuhakikisha waliohusika na kitendo hicho wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema tukio hilo halikuwagusa waandishi wa habari tu bali Watanzania wote wanaoitakia nchi yao iwe na amani na mshikamano.
Profesa Lipumba alisema taarifa za kuwapo kwa dhamira ya watesaji kutaka kumdhuru kwa kumfyatulia risasi Kibanda ili kumwangamiza kabisa ni za kushtua zaidi na kuiweka tasnia ya habari katika mashaka makubwa.

Aliongeza kuwa kuvamiwa kwa Kibanda na kuteswa na watu wasiojulikana ni mfululizo wa matukio mabaya ya utesaji na ya kikatili ambayo yanaendelea kukithiri nchini na hayapaswi kuvumiliwa.

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, kuanzia mwishoni mwa mwaka jana mpaka sasa matukio kadhaa yanayofanana na alilofanyiwa Kibanda yamekuwa yakitokea huku serikali ikiendelea kutoa ahadi ya ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao kwa kauli pekee.

Alifafanua kuwa pamoja na vitisho vya kuteswa na kuuawa kwa waandishi wa habari vinavyoonekana kutamalaki nchini vinarudisha nyuma uhuru wa wananchi kupata habari, jambo ambalo lina athari kubwa  kwa mustakabali wa  taifa.

 “Kutokana na matukio mengi ya kikatili, serikali pamoja na Jeshi la Polisi lifanye jitihada za kurejesha matumaini kwa wananchi kuwa ulinzi wa raia utaimarishwa na wahalifu kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema na kuongeza:

“Serikali sasa itoke usingizini na Jeshi la Polisi liongezewe uwezo wa kiintelijensia na upelelezi wa matukio ya uhalifu ili kuepusha raia kuendelea kuteketea

Comments

Popular Posts