Mawakala Redd's Miss TZ kunolewa leo

Mkurugenzi na mratibu wa shindano hilo kutoka katika kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga
Mawakala mbalimbali walioteuliwa kuandaa mashindano ya urembo nchini ya "Redd's Miss Tanzania" leo wanatarajiwa kushiriki katika semina maalum itakayofanyika kuanzia saa 3:00 asubuhi jijini Dar es Salaam.
 
Akizungumza na JAMIILEOTZ jana, mkurugenzi na mratibu wa shindano hilo kutoka katika kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga, alisema kuwa mawakala watakaoshiriki semina hiyo ni wa kuanzia ngazi ya kanda, mikoa na vitongoji vyote vya mkoa wa Dar es Salaam.
 
Lundenga alisema kuwa maandalizi ya semina hiyo yamekamilika na mawakala kutoka mikoani walianza kuwasili jijini tangu jana asubuhi na katika mialiko waliyotumiwa wamesisitizwa kufika bila kukosa ili kupata maelekezo kabla ya kuanza kuandaa mashindano yao ya ngazi husika.
 
Alisema kuwa kila mwaka kamati yake hutoa maelekezo kulingana na kanuni na taratibu zilizopitishwa na kamati hiyo na vilevile kuwapa mwangaza mawakala ni makampuni na taasisi zipi wanazoruhusiwa kuomba udhamini ili wasiende tofauti na mdhamini mkuu wa shindano hilo ngazi ya taifa.
 
"Tunaamini semina itafanyika kama ilivyokusudiwa na mawakala watapewa mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali katika kutekeleza majukumu yao," alisema Lundenga.
 
Mrembo kutoka katika kitongoji cha Sinza, kanda ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Brigitte Alfred, ndiye anayeshikilia taji hilo la taifa aliyelitwaa kutoka kwa Salha Israel wa Ilala.
 
Mwaka jana, kalenda ya mashindano hayo ilibadilika ambapo Kamati ya Miss Tanzania ilieleza kuwa mshindi Brigitte ataiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia mwaka huu na mrembo atakayeshinda taji hilo baadaye mwaka huu ndiye atakayeshiriki fainali hizo mwakani.
 
Lundenga alisema kuwa lengo la mabadiliko hayo ni kumpa mshindi nafasi ya kujiandaa vyema kushiriki fainali hizo zinazoshirikisha warembo kutoka nchi zaidi ya 100.
Rekodi ya mrembo wa mwaka 2005, Nancy Sumary, aliyetwaa taji la Mrembo wa Dunia Kanda ya Afrika haijavunjwa na washiriki wengine waliowahi kuiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo

Comments

Popular Posts