Mawaziri waeleza shule wanazosoma watoto wa

Waziri wa Nchi Ofisi ya rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira
Wakati umma ukiendelea kupiga kelele juu ya matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, huku ikijengwa dhana kuwa viongozi waandamizi serikalini ni wa kulaumiwa kwa kuwa wamekimbizia watoto wao nje ya nchi na kwenye shule binafsi kupata elimu bora huku wakitelekeza zile za umma, baadhi ya viongozi haYo wakiwamo mawaziri wamezungumzia madai hao na kueleza wanakosoma watoto wao.
 
Miongoni mwa waliozungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, wameeleza kwamba watoto wao wanasoma hapa nchini kwenye shule za serikali japokuwa kuna taarifa kwamba watoto wao wanasoma nje ya nchi na kwenye shule binafsi za gharama hapa nchini.
 
Baadhi  ya mawaziri waliozungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti  iliyowauliza kama wana watoto wao wanaosoma au waliowahi kusoma katika shule za kata wamejitetea kuwa wakati shule za Kata zinaanzishwa watoto wao walikuwa wamemaliza kusoma.
 
SOPHIA SIMBA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, alisema watoto wake hawakuwahi kusoma katika shule za kata kwa sababu wakati wanaanza kusoma hazikuwapo.
 
Hata hivyo, Simba alisema anao wajukuu zake ambao wanasoma katika shule za kata na kwamba wanakumbana na kero kadhaa ikiwamo kutofundishwa na walimu.
 
“Kimsingi watoto wangu hawajasoma katika shule za kata, lakini ninao wajukuu zangu wanaosoma shule za kata,  wanapata matatizo kweli, walimu hawafundishi,” alisema Simba.
 
STEVEN WASIRA
 
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira, alisema watoto wake wamesoma katika shule za sekondari za Kilakala, Tanga Ufundi na Forodhani.
 
Wasira alisema: “Suala la matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne hakuna haja ya kutafuta mchawi, kinachotakiwa ni kuangalia ni namna gani tutaweza kuboresha elimu yetu nchini.”
 
“Mimi naungana na hatua ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuunda tume, tume hii itatusaidia kujua mapungufu ni nini na namna ya kuyarekebisha, lakini tukianza kusema watoto wa mtu hawasomi katika shule za kata haitusaidii,” alisema Wasira.
 
Wasira aliongeza kuwa hata baadhi ya wafanyabiashara na wanasiasa watoto wao wengi hawasomi katika shule za kata, lakini hiyo haimaanishi kuwa shule za kata siyo bora.
 
HAWA GHASIA
 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, alisema ana mtoto mmoja ambaye anasoma katika shule ya sekondari ya Mwanga ambayo inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alipoulizwa kama ana watoto wanaosoma katika shule za kata alijibu kwa kifupi kuwa hawezi kujibu swali hilo kwa njia ya simu hadi afuatwe ofisini. 
 
WILLIAM LUKUVI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema suala la kama mawaziri wana watoto wao wanaosoma shule za sekondari za kata aulizwe Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
 
“Mimi ni Coordinator (mratibu) wa serikali siwezi kuzungumzia suala la kama mawaziri wana watoto wao wanaosoma shule za kata muulize Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,” alisema Lukuvi.
 
DK. ABDALLAH KIGODA
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, alipoulizwa kama ana watoto wake wanaosoma shule za kata au walisoma katika shule hizo alisema watoto wake wote ni wakubwa walishamaliza kusoma zamani.
 
Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge, alisema ana watoto wawili ambao walisoma shule ya sekondari ya Igwachanya ambayo ni ya kata na kwamba hivi sasa wanasoma chuo kikuu.
 
Lwenge alisema baadhi ya shule walimu hawafundishi. Alisema tatizo lingine ni kwamba wanafunzi hivi sasa wanasomea mitihani na walimu wanawafundisha kwa ajili ya mtihani tu.
 
“Kimsingi tatizo la matokeo mabaya pamoja na mambo mengine linachangiwa na wanafunzi wenyewe kusoma kwa ajili ya mtihani tu wanakuwa na mitihani ya nyuma, pia walimu hawafundishi na wanafunzi wanatumia jitihada zao kujisomea,” alisema Lwenge.
 
SOSPETER MUHONGO
 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema kwa umri alionao hawezi kuwa na mtoto anayesoma katika shule za kata.
 
“Mimi nipo Uingereza, unaniuliza masuala ya elimu wakati ya kwangu tu yananitosha, kwanza umri wangu sina mtoto anayesoma shule za kata,” alisema Profesa Muhongo.
 
PROFESA MARK MWANDOSYA
 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi maalum), Profesa Mark Mwandosya, alisema kwa sasa hana mtoto anayesoma sekondari.
 
Profesa Mwandosya ambaye alikuwa akizungumza na NIPASHE akiwa nje ya nchi alisema suala la kuzorota kwa elimu lisichukuliwe kisiasa, kinachotakiwa ni kujipanga upya kutafuta mbinu za kuboresha elimu nchini.
 
“Tukianza kutafuta mchawi tutaanza kurudi nyuma, hii ni karne ya sayansi na teknolojia, tunatakiwa tujipange ili ifikapo 2025 nchi yetu iwe ya watu wenye uelewa mzuri na kujiamini,” alisema Profesa Mwandosya.
 
Profesa Mwandosya alisema changamoto kubwa iliyopo ni kuboresha shule za sekondari zilizopo badala ya kuanza kuulizana mtoto wa fulani anasoma katika shule gani jambo ambalo halitasaidia.
 
CELINA KOMBANI
 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, alisema ana watoto wanne, ambao hakuna hata mmoja aliyesoma nje ya nchi.
 
Alisema mwanaye wa kwanza, ambaye hakumtaja jina, alisoma hadi kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Pugu, iliyoko jijini Dar es Salaam.
 
Waziri Kombani alisema baadaye mwanaye huyo alisoma Shule ya Alfa (Father Pekupeku) kidato cha tano na sita, iliyoko mkoani Morogoro na kwamba, elimu ya juu alisoma katika Chuo Kikuu Mzumbe, kilichopo mkoani humo.
 
Alisema mwanaye wa pili, ambaye pia hakumtaja jina, alisoma sekondari ya Kizuka, iliyoko mkoani humo na kwamba, elimu ya juu alisoma katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
 
Waziri Kombani alisema mwanaye wa tatu, ambaye vilevile hakumtaja jina, alisoma kidato cha kwanza hadi sita katika Shule ya Sekondari Morogoro, wakati Shahada ya Kwanza aliipata katika Chuo Kikuu cha Tumaini na Shahada ya Pili aliipata Chuo Kikuu Mzumbe.
 
Alisema mwanaye wa nne, ambaye pia hakumtaja jina, hivi sasa yuko mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu Mzumbe.
 
“Hakuna mtoto wangu aliyesoma nje. Wakitaka wafanye uchunguzi,” alisema Kombani.
 
Alisema tatizo la kufaulu na kufeli, liko kwa mtoto mwenyewe na siyo shule anayosoma, licha ya shule za hapa nchini kukabiliwa na tatizo la vitendea kazi, ambavyo alisema serikali imekuwa ikilishughulikia.
 
GAUDENSIA KABAKA
 
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema watoto wote ambao hakutaja idadi yao, akiwamo wa mwisho, ambaye kwa sasa ni marehemu, walisoma katika shule za kawaida hapa nchini.
 
Alisema mwanaye wa kwanza, ambaye hakumtaja jina elimu ya msingi alisoma katika Shule Msingi Bunge, iliyoko jijini Dar es Salaam na kwamba, walipohamia mkoani Mwanza, aliendelea na elimu hiyo katika Shule ya Msingi Nyanza.
 
Alisema mwanaye huyo alisoma hadi kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Wasichana, iliyoko mkoani Tabora na baadaye alisoma elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
 
Hata hivyo, Waziri Kabaka alisema hakubaliani na dhana iliyotawala vichwani mwa watu wengi kwamba, wazazi wanaowapeleka watoto wao kusoma kwenye shule za binafsi, ni watu wenye uwezo pekee kifedha.
 
Alisema hata wazazi wasiokuwa na uwezo nao pia huwapeleka watoto wao kwenda kusoma kwenye shule hizo kwa kujibana kimatumizi.
 
“Huo utafiti mnaoufanya hautasaidia. Wazazi wanaowapeleka watoto wao (kusoma) private schools (shule za watu binafsi) siyo wenye hela tu, hata wasiokuwa na hela pia wanawapeleka,” alisema Waziri Kabaka.
 
BENEDICT NANGORO
 
Naibu Waziri  wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi,  Benedict Ole Nangoro, alisema hana watoto wanaosoma nje ya nchi.
 
“Hakuna mtoto wangu hata mmoja anayesoma nje ya nchi, wote wanasoma hapa nchini tena katika shule za serikali mkoani Arusha,” alisema Nangoro.
 
JENISTA MUHAGAMA
 
Mwenyekiti wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Peramiho (CCM), Jenista Muhagama, alisema watoto wake wote wanasoma katika vyuo na shule zilizopo hapa nchini.
 
Alisema mmoja wa watoto wake amemaliza shule ya Sekondari Matogoro iliyoko Songea na hivi sasa ni mwalimu.
 
Alisema katika shule hiyo pia wapo watoto wake wawili wanaoendelea na masomo ambao bado hawajamaliza.
 
SUZAN LYIMO
Waziri kivuli wa Elimu na Mbunge Viti Maalumu (Chadema), Suzan Lyimo, alisema watoto wake wote wanasoma katika shule za hapa nchini, mmoja anasoma shule ya Sekondari Ilboru iliyopo jijini Arusha.
 
Alisema wengine wawili wanasoma katika shule ya msingi Mlimani iliyopo jijini Dar es Salaam, na mwingine anasoma katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas).
 
MAGDALENA SAKAYA
 
Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Tabora (CUF), Magdalena Sakaya, alisema hana mtoto yeyote anayesoma katika shule za gharama kubwa bali ana mtoto mdogo wa miaka mitano anayesoma katika shule ya misheni.
 
KASIMU MAJALIWA
 
Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi –Elimu), Kasimu Majaliwa, alisema hana imani kwamba elimu imezorota kwa sababu watoto wa viongozi wanasoma nje ya nchi na badala yake matokeo mabaya ya kidato cha nne yamesababishwa na mambo mengi. 
 
“Sisi tumepewa dhamana, tutahakikisha tunatekeleza kikamilifu kusimamia majukumu yetu. ziko sababu nyingi za watoto kutofanya vizuri, wapo ambao wamefeli kwa kutosoma kikamilifu, wapo waliokosa vifaa, walimu au miundombinu mibovu; siyo sababu moja tu ya kusomesha watoto nje ya nchi,” alisema.
 
Alisema hakuna Waziri au Mtendaji Mkuu wa Wizara ambaye anakwenda kazini na kuishia tu kusoma magazeti kwa sababu mtoto wake anakuwa anasoma nje ya nchi. 
 
“Tuko makini kuona elimu inapata mafanikio, ndiyo maana utaona serikali inaimarisha miundombinu, inaweka vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuzalisha walimu wengi kila mwaka.”
 
Alisema pamoja na mambo mengine, tume iliyoundwa na Waziri Mkuu itaangalia mitihani iliyopita ilivyotungwa hadi usahihishaji ili kuona kasoro na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike.
 
Alisema ana watoto wawili na mmoja anasoma Ruangwa wakati mwingine bado hajaanza shule. 
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, alisema matokeo mabaya ya wanafunzi katika mtihani huo yametokana na sababu nyingi zikiwamo za wanafunzi, wazazi na serikali kwa upande mwingine.
 
Alisema suala la kusingizia viongozi wa serikali kuwa ndiyo sababu ya kufeli kwa wanafunzi kwa kuwa hawasomeshi watoto wao kwenye shule za kata, siyo la kweli kwa kuwa wapo baadhi ya viongozi akiwamo yeye ambaye wadogo zake wawili aliowasomesha, wamemaliza katika shule za sekondari za kata huko Mtibwa.
 
“Kwanza ukisema viongozi wa serikali unakuwa unabagua kwa sababu utakuwa unaongelea mawaziri, makatibu wakuu na ukaacha wengine kama wabunge na wafanyakazi wengine serikalini. La msingi hapa ni kuona tulipokosea na kuparekebisha,” alisema.
 
Alisema suala la kufeli kwa wanafunzi linatokana na mazingira ya baadhi ya shule zenyewe kama miundombinu inayohitajika, wanafunzi na wazazi kwa upande mwingine.
 
Alisema kwa mfano mwanaye aliyemaliza mwaka jana na ambaye amepata daraja la nne, hakusoma katika shule za kata kwa sababu hakuchaguliwa baada ya kumaliza darasa la saba, na badala yake alimpeleka kwenye shule iliyokuwa na kila kitu; walimu, maabara na maktaba lakini bado alipata daraja la nne.
 
Alisema wanafunzi wengi wamefeli kutokana na kutojibidiisha katika masomo na badala yake wakatumia muda mwingi kwenye ‘facebook’ wakichati usiku kucha badala ya kusoma.
“Hapa unajiuliza mtoto huyu amepata wapi simu, moja kwa moja amepewa na mzazi wake. Kwa hiyo nasema, ni vizuri tukaboresha mazingira ya shule, tukawapa maslahi mazuri walimu, tukaweka maabara, maktaba, tukaboresha mitaala yetu, lakini pia tukawasimamia watoto wasome, kwa kuwa unaweza ukampeleka ng’ombe mtoni, lakini huwezi ukamlazimisha kunywa maji,” alisema.
 
Wakati mawaziri na baadhi ya wabunge wakieleza hivyo, tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameunda tume maalum itakayofanya uchunguzi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ambayo yalitangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa Februari 18, mwaka huu.
 
Katika matokeo hayo, asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne Oktoba, 2012 walifeli kwa kupata daraja sifuri. 
 
Juzi Pinda alitangaza majina ya wajumbe tume hiyo ambao ni Mwenyekiti wa Tume ni Profesa Sifuni Mchome kutoka tume ya vyuo vikuu, Makamu mwenyekiti wa tume hiyo ni mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Bernadeta Mshashu.
 
Wajumbe wa tume hiyo ni pamoja na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia (NCCR Mageuzi), mbunge wa Kibiti (CCM), Abdul Marombwa, Profesa Mwajabu Possi (Profesa Mshiriki wa Elimu toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), Honoratha Chitanda (Makamu wa Rais Chama cha Waalimu – CWT), Daina Matemu (Katibu wa Tahossa), Juma  Mringo (Mwenyekiti Tamongsco).
 
Wengine ni Rajan Rakheshi, (Katibu Mtendaji Twaweza), Peter Maduki (Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii), Nurdin Mohamed, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Alharamain, (Mjumbe toka Bakwata),  Suleiman Hemedi Khamis (Mwakilishi-Baraza la Wawakilishi), Abdallah Hemed Mohamedi (Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar), Mbarouk Jabu Makame (Baraza la Elimu Zanzibar), na Kizito Lawa, Mratibu wa Mitaala (Taasisi ya kukuza Mitaala)

Comments

Popular Posts