Mbunge Chadema kizimbani

Mbunge wa jimbo la Ukerewe, Mwanza kwa tiketi ya Chadema, Salvatory Machemli
Mbunge wa jimbo la Ukerewe, Mwanza kwa tiketi  ya  Chadema,  Salvatory  Machemli   amefikishwa  mahakamani  kujibu shitaka la uchochezi.

Machemli  (39)  amesomewa  shitaka  hilo  jana  mbele ya  Hakimu  Mkazi  Mfawidhi  wa mahakama ya wilaya  hiyo, Rouben  Luhasha.

Hata hivyo, Machemli  amekana  shitaka hilo na yupo nje  kwa dhamana ya Sh. milioni 2 na ahadi ya  Sh. 150,000.

Mwendesha  mashitaka wa  polisi  ASP, Denis  Rwiza, alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa  huyo alitenda kosa hilo  Oktoba  23,  2011 majira  ya saa za  alasili  katika  kijiji cha Nyamanga  kisiwani Ukara.

Rwiza ambaye pia ni Afisa Upepelezi wa wilaya hiyo, alisema mbunge  huyo alitenda kosa hilo wakati  akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chadema.

Alisema mshitakiwa kwa makusudi aliwachochea  wananchi kutenda kosa hilo kwa kuwaelekeza wachukue uamuzi mgumu ikiwa ni pamoja na kuzuia na kushambulia  maafisa wa polisi wakati wa kufanya kazi zao kisiwani hapo.

Imedaiwa kuwa  kupitia mkutano huo aliwataka  wananchi wazuie na wamshambulie kwa silaha za jadi ikiwemo marungu, mapanga na fimbo afisa wa polisi atakayekwenda kutafuta washitakiwa nyakati za usiku.

Mwendesha mashitaka huyo wa polisi alisema  kipindi hicho ulikuwepo msako wa watuhumiwa wa mauaji ya watu wanne waliouawa na wananchi   Desemba 10,  2010  mbele ya maafisa wa polisi   kwa tuhuma za ujambazi.

Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na imeahailishwa hadi Machi 21, itakapotajwa tena

Comments

Popular Posts