MWAKYEMBE.......UFISADI MPYA BANDARINI

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Mawakala wa Forodha wameibua ufisadi mpya katika Bandari ya Dar es Salaam baada ya kubainisha kuwa vizuizi vyote vilivyowekwa katika bandari hiyo vipo kwa ajili ya maslahi ya baadhi ya vigogo.
 
Madai hayo yameibuka baada ya kila wanapotaka kupitisha mizigo yao kulazimishwa kutoa rushwa.
 
Walimweleza hayo juzi Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, wakati wa mkutano wa dharura wa wakurugenzi wa makampuni ya mawakala wa Forodha kueleza changamoto zinazowakabili katika Bandari ya Dar es Salaam.
 
Mmoja wa mawakala hao, Teddy Mwakibete, alisema katika kero wanazokumbana nazo katika bandari hiyo ni pamoja na  kuombwa rushwa wanapotaka kupitisha mizigo ambayo imekamilishwa taratibu zote za kisheria.
 
“Geti zote zilizowekwa bandari zimewekwa kwa ajili ya kunufaisha baadhi ya watu hasa geti la kuingilia Kampuni ya Kupakua na Kupakia Makontena (TICS), tunalazimishwa kutoa rushwa ndipo tupite,” alisema Mwakibete.
 
Mwakibete alimweleza Dk. Mwakembe kero nyingine wanayokumbana nayo mawakala wa forodha ni kulazimishwa kuwa na rundo la vitambulisho ili waruhusiwe kufanya kazi zao vinavyowagharimu zaidi ya Sh. 64,000.
 
Mfano wa vitambulisho hivyo ni cha TICS, TPA (Mamlaka ya Bandari), ICD na cha uwanja wa ndege ambavyo vinawagharimu pesa nyingi na hutakiwa kuvivaa kwa wakati mmoja.
Wakala mwingine, Otieno Igogo, alisema serikali isadie kuweka ushindani mzuri wa kibiashara kwa mawakala kwa sababu mawakala wakubwa wanawaonea wadogo na kuwachongea kwamba ni wezi na matapeli.
 
Igogo alisema kero nyingine inayowakabili ni upatikanaji wa leseni ya wakala wa forodha ambayo ni ngumu kuipata kutokana na sheria zilizowekwa.
 
"Mheshimiwa waziri kuna tatizo la makampuni makubwa kukusanya fedha ambazo ni za tozo na kuzipeleka nje, hili suala lazima serikali iliangalie linaathiri uchumi wan nchi,” alisema Igogo.
 
Akijibu malalamiko hayo, Dk. Mwakyembe alisema suala la mawakala kutakiwa kuwa na vitambulisho vingi atalifanyia kazi kwa kuhakikisha kunakuwa na kitambulisho kimoja tu au viwili.
 
Dk. Mwakyembe alisema kero nyingine amezichukua na kuahidi kuzifanyia kazi ili kuboresha utendaji kazi wa mawakala wa forodha ambao wana mchango mkubwa katika uchumi wa nchi

Comments

Popular Posts