Mwanamke auawa kwa kukatwa mapanga

IGP Saidy Mwema
Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Wanawake duniani, vitendo vya kikatili kwa wanawake vimeendelea kushika kasi katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo mkoani Pwani, mwanamke mmoja Fatuma Shaban, amefariki dunia baada ya kukatwa  kwa mapanga na mume wake eneo la Kidimu, wilayani Kibaha.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ulrich Matei, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, mwanamke huyo, ameuawa kikatili na mumewe, Petter Ndala, maarufu kama Kasheba, ambaye alikimbia baada ya mauaji hayo yaliyotokea juzi, majira ya saa 1:30 usiku.

Kamanda Matei alisema chanzo cha mauaji hayo kimedaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi na Polisi wanaendelea na jitihada za kumtafuta mtuhumiwa huyo, aweze kufikishwa kwenye vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria.

Katika tukio Lingine mwili wa mtoto mwenye umri wa miaka miwili, Alikama Saidi, umehifadhiwa katika hospitali Teule ya Tumbi, Kibaha kwa uchunguzi, baada ya kuzama kwenye karo la kuhifadhi maji, huko eneo la Kidimu, wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Ilidaiwa kabla ya kifo hicho, mtoto huyo alikuwa akicheza nyumbani kwao, lakini mkazi jirani,  Agness Mufyanga, alipita eneo hilo, na mtoto huyo kumfuata kwa nyuma akiendelea kucheza, hadi alipoangukia katika karo hilo ambalo lilikuwa halijafunikwa, akazama na kupoteza maisha.

Katika tukio jingine, mtoto mmoja mtembea kwa miguu, mwenye umri wa miaka mitano, Laiza Said mkazi wa Makole, wilayani Bagamoyo, alipoteza maisha baada ya kugongwa na  basi  lenye namba za usajili T 546 AWS aina ya Fuso, mali ya kampuni ya Super Jatco.

Kamanda huyo wa polisi alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 7:45 mchana, katika barabara ya Chalinze Segera, ambapo basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Nurdin Abas, aliyekuwa akitokea Dar es Salaam kuelekea Lushoto Tanga, ambaye amekamatwa na anahojiwa na Polisi

Comments

Popular Posts