Polisi kizimbani kwa tuhuma za kuua raia
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu
Mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Mwanza, Emmanuel Njuu, ilidaiwa na Wakili wa Serikali, Sehewa Mamti, kuwa mtuhumiwa huyo alifanya mauaji hayo Februari 9, mwaka huu katika kituo kidogo cha polisi Igogo jijini Mwanza.
Hata hivyo, mtuhumiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama ya wilaya haina mamlaka kisheria ya kusikiliza kesi za mauaji na chombo chenye mamlaka hiyo ni Mahakama Kuu.
Kesi hiyo iliahirishwa na mtuhumiwa alipelekwa rumande hadi hapo itakapotajwa tena Machi 14, mwaka huu.
Taarifa za mauaji hayo ziliibuliwa kwa mara ya kwanza na mwandishi wa blogu hii Februari 20, mwaka huu baada ya kuwapo kwa usiri mkubwa ndani ya Jeshi la Polisi huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, akikwepa kulizungumzia tukio hilo kwa maelezo kuwa hakuwa na taarifa.
Jana Mwandishi wa blog hii alimtafuta Kamanda Mangu ili azungumzie tukio hilo baada ya askari huyo kusimamishwa kizimbani wiki iliyopita, alithibitisha kuwa mshitakiwa huyo alikamatwa wiki iliyopita.
“Huyo askari unayetaka kujua habari zake ameshafikishwa mahakamani tangu wiki iliyopita. Tulimkamata hapa hapa Mwanza,” alisema Kamanda Mangu kwa ufupi.
Awali \Mwandishi wa blog hii alimkalili baba mzazi wa marehemu mzee Fred Mallya, akidai kuwa mwanaye ambaye alikuwa akifanya kazi kama wakala wa usafiri wa mabasi aliuawa kwa kupigwa na askari wa kituo kidogo cha polisi Igogo bila kumtaja jina.
Akielezea mazingira ya mauaji hayo, Mallya alidai kwamba mwanaye alikuwa katika shughuli zake kwenye stendi ya mabasi ya Nyegezi na kwamba baadaye alifika mwanamke mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja na kumkabidhi (Alfred) kifurushi kilichokuwa na samaki.
Kwa mujibu wa Mzee Mallya, marehemu Alfred alikabidhiwa samaki hao wenye thamani ya Sh. 30,000 ili awasafirishe kwenda Dar es Salaam kama alivyopewa maelekezo na mwanamke huyo.
Alidai kwamba kesho yake mwanamke huyo alirudi katika ofisi ya marehemu Alfred na kumweleza kuwa mzigo aliompatia haujafika, lakini yeye (marehemu) alimsisitiza kuwa aliutuma lakini kama ulipotea alikuwa tayari kulipa kulingana na thamani yake.
Hata hivyo, baada ya kulazimishwa kulipa Sh. 300,000, alisema angelipa Sh. 100,000 ili kuondoa usumbufu usio wa lazima, lakini mwanamke huyo alikataa.
Alidai kwamba suala hilo lilisababisha Alfred kufikishwa kituo kidogo cha polisi cha Nyegezi kabla ya kuhamishiwa kituo cha Igogo ambako kesi yake ilisimamiwa na askari wa upelelezi.
Mzee Mallya alidai kuwa licha ya kumhoji askari huyo alimpiga marehemu kwa kutumia kitu chenye ncha kali na kumsababishia majeraha makubwa sehemu za kichwani na miguuni na kwamba alifariki dunia Februari 17, mwaka huu baada ya kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando

Comments
Post a Comment