Polisi wamshikilia kigogo wa Chadema
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare
Lwakatare ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kagera, alitiwa mbaroni jana mchana na maofisa watatu wa polisi waliokwenda katika makao makuu ya chama hicho yaliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akizungumza na mwandishi wa wetu jana alithibitisha kukamatwa na kuhojiwa kwa kiongozi huyo wa Chadema.
Hata hivyo, Kamanda Kova alikataa kuweka wazi sababu za kukamatwa kwake na kuahidi kutoa taarifa rasmi leo baada ya taratibu za kumhoji Lwakatare kumalizika.
“Ni kweli amekamatwa kwa tukio ambalo hatuwezi kulizungumzia, yupo makao makuu ya polisi, kwa taarifa zaidi na sababu za kukamatwa kwake tutawaeleza kesho (leo),”alisema Kamanda Kova.
Kwa upande wake, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, alisema kuwa wamemkamata Lwakatare ili kuchunguza taarifa zilizosambazwa dhidi yake kwenye mitandao zinazohatarisha uvunjifu wa amani nchini.
Senso alipoulizwa kwanini hadi saa 2:00 usiku jana polisi walikuwa wanaendelea kumshikilia Lwakatare, alisema hizo ni taratibu za kisheria ambazo zilikuwa zinaendelea.
Hata hivyo, wakati Jeshi la Polisi likiwa na kigugumizi cha kueleza sababu za kukamatwa kwa Lwakatare, mitandao mbalimbali ya kijamii imeeleza kuwa Lwakatare amekamatwa kutokana na kuhusishwa na tukio la kupanga njama za kumdhuru Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda.
Miongoni mwa mitandao ambayo taarifa hizo zimewekwa ni mtandao wa JamiiForum, ambao umeeleza kuwa Lwakatare amekamatwa kutokana na tukio la Kibanda.
Pia katika tovuti ya Youtube, imewekwa video ambayo inamuonyesha Lwakatale akizungumza mambo mbalimbali ya kupanga njama hizo.
Taarifa zaidi katika mitandao hiyo ya kijamii zimeeleza kuwa, Lwakatare wakati akihojiwa alikuwa na wakili Nyaronyo Kicheere na kwamba baadaye kama atafunguliwa kesi mahakamani, itasimamiwa na wakili mashuhuri nchini na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, akizungumza na mwandishi wa blogu hii, alisema jana majira ya mchana maofisa watatu wa polisi kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi walifika katika makao makuu ya chama hicho.
Alisema baada ya kufika walionana na yeye (Dk. Slaa) na kueleza kuwa wana shida ya kuonana na Lwakatare na kwamba kwa kuwa alikuwa anawafahamu maofisa hao aliwaruhusu kuonana naye.
Dk. Slaa alisema baada ya dakika chache, maofisa hao walirudi tena kwake na kueleza kuwa wanaomba kuondoka na Lwakatare kwenda makao makuu ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
“Walivyozungumza hivyo ikabidi tukafanya utaratibu wakati wa mahojiano awepo na wakili wetu na taratibu kama atafunguliwa jalada taratibu zifanyike kumuwekea dhamana,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa baada ya kumkamata na kuondoka naye, vijana wa Chadema ambao walikwenda makao makuu ya Polisi kufuatilia kinachoendelea, walipofika huko waliambiwa na polisi kwamba hawatakiwi kuonekane makao makuu ya Polisi.
Dk. Slaa alisema mwanasheria wa Chadema, Kicheere ndiye aliyeruhusiwa kuwapo makao makuu ya Polisi na kwamba baadaye Lwakatare alichukuliwa kupelekwa nyumbani kwake kwa ajili ya kufanyiwa upekuzi.
Alisema hadi kufika saa 1:30 usiku, Lwakatare alikuwa bado yupo mikononi mwa polisi na kwamba viongozi wa Chadema walikuwa wanaendelea kufuatilia suala hilo kujua hatma yake.
Dk. Slaa alidai kwamba taarifa zilizosambazwa katika mitandao ya jamii na kumhusisha Lwakatare na tukio la kutekwa na kupigwa Kibanda huo ni mchezo mchafu unaofanywa na watu ambao hakuwataja kwa nia ya kuikandamiza Chadema.
Alisema siku tatu kabla ya kukamatwa kwa Lwakatare, Chadema ilipata taarifa kutoka vyanzo vyake kwamba kuna video feki inaandaliwa ya kuwabambikizia viongozi wa Chadema.
“Kama wamemkamata Lwakatare kwa kumhusisha na tukio la Kibanda sisi Chadema tunafurahi na tunasema sasa ukombozi wa nchi hii upo karibu, tunaomba Watanzania wafungue macho yao ili haki itendeke,” alisema Dk. Slaa na kuongeza:
“Suala la kuwabambikia matukio mbalimbali viongozi na wanachama wa Chadema limekuwa ni utamaduni nchini, lakini jambo lolote linapotokea likahusisha watani zetu (Chama Cha Mapinduzi) halifanyiwi kazi”.
“Wakati wa uchaguzi wa Igunga, Katibu Mkuu wa CCM (wakati huo Willson Mukama), aliituhumu Chadema kwamba wameingiza nchi makomandoo kutoka nje, lakini hakuitwa wala kuhojiwa, Daudi Mwagosi (aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten) aliuawa mbele ya RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) ambaye hadi sasa bado anadunda,” alisema Dk. Slaa akimaanisha RPC wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
Dk. Slaa alitoa mfano mwingine kwamba Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka, alitekwa, kuteswa na kujeruhiwa, lakini hadi sasa vyombo vya usalama havijawahi kumwita kumhoji aeleze kilichotokea kwa sababu vinafahamu siri iliyojificha ndani yake.
Dk. Slaa alisema kuna mchezo mchafu unaochezwa kuiangamiza Chadema na kwamba hata hivyo, chama hicho kitaendelea kuwa imara na kwamba baada ya tukio la Lwakatare, kitajipanga kuibua matukio yote ya mauaji yaliyofanyika nchini.

Comments
Post a Comment