Polisi yazuia maandamano ya kudai maji Dar

Kamanda wa Polisi mkoa wa kinondoni, Charles Kenyela
Jeshi la Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni limepiga marufuku kufanyika kwa maandamano yaliyopangwakufanywa kesho na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) kushinikiza upatikanaji wa maji katika jimbo hilo na Mkoa wa Dar es Salaam.
 Kamanda wa Polisi mkoa huo, Charles Kenyela, alisema maandamano hayo yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani pamoja na kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.
Alisema maazimio hayo yametolewa baada ya kupokea barua mbili kutoka kwa Mnyika mapema wiki hii  na kukusanya na kubadilishana taarifa na wadau mbalimbali ambao wangeguswa na mkutano pamoja na maandamano hayo.
 
Kenyela alisema walibaini kuwa taarifa ya hoja hiyo tayari Mnyika amekwishaiwasilisha katika Bunge, hivyo Waziri mwenye dhamana alitakiwa kuijibu hoja hiyo katika Bunge na hivyo siyo utaraibu mzuri kwani unaonyesha kuashiria kuchochea fujo kwa kuwa majibu ya suala hilo anayo kupitia Bunge.
 
Sababu nyingine kuwa ni kuwa eneo la Manzese Bkharesa ambalo limekusudiwa kufanyika mkutano huo ni la kuegeshea magari na liko kando ya barabara ambayo kwa sasa iko katika ujenzi hivyo si mahali sahihi pa kufanyia mikutano.
 
Kamanda Kenyela alisema pia Waziri husika ambaye maandamano yanakwenda katika ofisi zake hana taarifa yeyote juu ya maandamano hayo na kwamba kwenda kwa maandamano katika ofisi za serikali bila kutoa taarifa rasmi ni sawa sawa na kuwachochea wananchi dhidi taasisi yao ya Serikali jambo ambalo amesema linaweza kusababisha fujo na kutokea kwa vurugu.
 
Aliitaja sababu nyingine kuwa ni ufinyu wa barabara ya Morogoro ambayo maandamano yanatakiwa kufanyikia. 
 
Aliongeza kuwa eneo la Wizara ya maji ni eneo finyu na limepakana na kituo cha Gridi ya Taifa ya umeme, gesi ya Ubungo na lipo karibu na kituo cha daladala, maeneo ambayo yana watu wengi na wanaweza kudhurika endapo fujo zitatokea.
 
“Jeshi la Polisi limeyabaini hayo ambayo nimeyaeleza na kuamua kuzuia kufanyika kwa maandamano hayo, hivyo yeyote atakayekaidi agizo hili hatua kali za kisheria zitachukuliwa,” alisema Kenyela. Hata hivyo, Mnyika jana hakupatikana kuzungumzia hatua hiyo.

Comments

Popular Posts