Wabunge Chadema waanza sokomoko Jipya
Tundu Lissu mbunge wa Singida Mashariki.
Wabunge wanne wa Chadema waliotiwa hatiani na kamati hiyo kuhusiana
na vurugu zilizotokea bungeni Februari 4, mwaka huu, ni pamoja Joshua
Nassari (Arumeru Mashariki), Tundu Lissu (Singida Mashariki), John
Mnyika (Ubungo) na Pauline Gekul (Viti Maalum).
Msimamo wa wabunge hao ulitangazwa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alipozungumza na NIPASHE, saa chache
baada ya kukutana na kamati hiyo na kugoma kuhojiwa nayo jana.
Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alisema
aligoma kuhojiwa kutokana na kamati hiyo kumpa tuhuma jana ikiwa ni siku
rasmi ya mahojiano, kinyume cha kanuni za Bunge, ambazo zinataka mbunge
anapotuhumiwa apewe siku tatu za kujiandaa kabla ya kwenda kuhojiwa.
“Kwa hiyo, nimewaeleza kuwa mahojiano hayataanza mpaka kwanza
nitakapojiandaa,” alisema Lissu, aliyetajwa na Bunge katika orodha ya
wabunge wanne wa Chadema kwamba, ni vinara wa vurugu bungeni.
Alisema alikutana na kamati hiyo jana saa 4 asubuhi, lakini baada
ya dakika 15 aliondoka baada ya kuitolea hoja kadhaa kuhusu utaratibu
huo.
Lissu alisema sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa, ni kwa vile
kamati hiyo ilikaa Februaria 5 kujadili jambo hilo na Februari 8, mwaka
huu, ikatoa hukumu yake mbele ya Bunge kwamba, katika uchunguzi wao
wabunge wanne au watano walisababisha vurugu bungeni.
Hivyo, akasema kamati hiyo, ambayo kwa sasa inafanya shughuli zake kimahakama, haiwezi kukaa tena kwa jambo hilo.
“Mahakama ikishakamilisha hukumu, mamlaka yake yanaisha. Jambo hilo
limeshaisha, haina mamlaka ya kusikiliza. Ni makosa kutushitaki tena
sababu tulishashitakiwa na kuadhibiwa kwa kuitwa vinara wa vurugu na
watovu wa nidhamu,” alisema Lissu.
Alisema hoja hiyo inatiwa nguvu na kifungu cha 280 cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai.
Lissu alisema kifungu hicho kinamlinda kwa kuwa tayari
alishaachiwa huru na ‘mahakama’, hivyo hawezi kushitakiwa tena kwa kosa
hilo hilo moja.
“Nilishaitwa kinara wa vurugu, nilishaadhibiwa,” alisema Lissu.
Alisema sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa, ni kwamba, kamati hiyo
ilikiuka Katiba ya nchi ilipokaa Februari 5,6 na 7, kwani
haikuwapelekea hati ya mashtaka, pia haikuwapa fursa ya kujitetea.
Badala yake, alisema kamati hiyo iliwahukumu bila kuwaonyesha
makosa yao ni yepi, kinyume cha Ibara ya 12 (6) na (7) ya Katiba ya
nchi, ambayo inazuia haki na wajibu wa mtu kuamuliwa bila mwenyewe
kusikilizwa kwa ukamilifu.
“Sisi haki na wajibu wetu vimeamuliwa (na kamati hiyo) bila kutupa
haki ya kusikilizwa kabisa. Hivyo, kamati hii ni ya uvunjaji wa katiba,”
alisema Lissu.
Alisema sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa, ni ukiukwaji wa sheria
ya haki, kinga na madaraka ya Bunge, uliofanywa na Bunge kutokana na
kuwaita kwa kutumia ujumbe wa polisi, badala ya hati ya wito ya Bunge.
Lissu alisema ujumbe huo ulitumwa na Bunge kwa Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP, ambaye naye akausambaza kwa
makamanda wa polisi wote wa mikoa.
“Hapo kuna ukiukwaji wa sheria. Kwani huo siyo wito kwa wabunge,
bali ni police massage (ujumbe wa polisi). Kanuni za Bunge zinasema
mbunge atapelekewa summons (hati ya wito). Utaratibu wa kutuita
haukufuatwa,” alisema Lissu na kuongeza:
“Summons anakabidhiwa mbunge. Wana namba zetu za simu, tunapoishi wanapajua. Hawakuwa na sababu ya kututumia police massage.”
Alisema kinyume cha utaratibu huo wa kanuni za Bunge, wamekuta kuna
barua iliyoandikwa na Katibu wa Bunge, ambayo siyo hati ya wito.
Lissu alisema sheria inataka hati ya wito kwa mbunge iandikwe na
Katibu wa Bunge kwa maelekezo ya Spika, hivyo hawajui barua hiyo
iliandikwa na nani, badala yake wanachoamini ni kwamba, haijaelekezwa na
Spika.
Alisema sababu nyingine ya kukataa kuhojiwa, ni kwamba wanaamini
kamati hiyo kisheria haipo kwa kuwa ilishavunjwa na kanuni za Bunge.
Lissu alisema kwa mujibu wa kanuni hizo, katika Mkutano wa 10 wa Bunge, kamati zote za kudumu za Bunge zinatakiwa zivunjwe.
“Kwa hiyo, uenyekiti wa Ngwilizi kwenye kamati hiyo, haupo, ujumbe
wa Vita Kawawa haupo, ujumbe wa Ndesamburo haupo na wajumbe wengine
wote wa kamati ujumbe wao haupo. Uliisha tangu tarehe 8/2/2013,” alisema
Lissu na kuongeza:
Alisema kutokana na kanuni za Bunge, Spika hana mamlaka ya kuvunja kamati moja peke yake, bali anatakiwa kuzivunja zote.
“Sasa hii kamati ya Ngwilizi inatoka wapi, kwa kanuni ipi, kwa sheria ipi?,” alihoji Lissu.
Alisema Februari 8, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliunda na kutaja
kamati mpya 18 na siku hiyo hiyo akasema agawe fomu kwa wabunge ili
wajiunge kwenye kamati hizo, ikiwamo ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge.
“Kwa hiyo, kamati ya Brigedia Ngwilizi ilishaisha. Wasubiri spika aunde upya,” alisema Lissu.
Alisema pia kanuni ya 113 (10) inazungumzia nafasi ya mwenyekiti na
uenyekiti wa kamati ya Bunge kwamba, unakoma katika Mkutano wa 10.
Hivyo, akasema uhai wa Ngwilizi kama mwenyekiti wa kamati hiyo
uliisha tangu Mkutano wa 10 wa Bunge ulipoahirishwa Februari 8, mwaka
huu.
“Kwa hiyo, hatuna kamati, hatuna mashtaka, bali ni ukiukwaji wa
kanuni uleule, ambao umekuwa ukifanywa na Bunge hili. Kwa sababu hizo,
hatuwezi kuendelea kwenda kwenye chombo, ambacho hakipo kisheria,”
alisema Lissu.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema suala hapa si wabunge
wa Chadema, bali wawakilishi wa wananchi, hivyo hawatakwenda kuhojiwa
kwenye kamati hiyo na kwamba, kama ni kuwafukuza ubunge, wako tayari na
Spika ajaribu kufanya hivyo.
Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na
Mbunge wa Hai, alisema kanuni ya Bunge namba 113 (7) inazungumzia ukomo
wa uhai wa kamati za Bunge, kwamba unaishia Mkutano wa 10 wa Bunge,
ambao unakuwa nusu ya kwanza ya uhai wa Bunge lenyewe.
Hivyo, akasema kamati hiyo inayowaita wabunge wa Chadema uhai wake
uliisha siku Bunge la 10 lilipoahirishwa Februari 8, mwaka huu.
“Hivyo, kwa mujibu wa kanuni za Bunge kamati hiyo haipo na mwenyekiti wake alishamaliza muda wake,” alisema Mbowe.
Alisema wabunge wa Chadema wameitwa kwa sababu ya vurugu
zilizotokea bungeni Februari 4, mwaka huu, wakati wanajua kuwa kamati
hiyo hiyo tayari ilishalifanyia kazi jambo hilo.
Zaidi hivyo, alisema kamati hiyo ilitengeneza tuhuma, ikaendesha
mashtaka, ikatoa hukumu, ikiwataja hata wahusika kuwa ni Lissu, Mnyika,
Paulina Gekul (Viti Maalum) na Nassar.
Kutokana na hilo, aliwataka kutambua kuwa kamati hiyo inapokaa huwa
ni sawa na mahakama, ambayo kwa kawaida kisheria na kikanuni,
mahakama/kamati hiyo inapokuwa imeshaamua jambo haiwezi tena kukaa na
kulifanyia kazi jambo hilo hilo.
“Mbele ya Watanzania wote, Tanzania nzima na dunia nzima ikasikia.
Kamati ile iliwahukumu wabunge wa Chadema bila hata kuwasikiliza. Dunia
nzima inajua hivyo. Sasa wanataka kusikiliza nini tena? Wakosaji
wanajulikana. Walihukumiwa bila hata kufuata taratibu,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Brigedia Jenerali (mstaafu), Hassan
Ngwilizi, akizungumza na JAMIILEOTZ alisema hawezi kuzungumzia chochote juu
ya hilo bali atafutwe Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah.
Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza na JAMIILEOTZ alisema ni kweli kuna wabunge ambao wangetarajiwa kuhojiwa na
Kamati hiyo lakini hawezi kulizungumzia kwa mapana sana kwa kuwa siyo
msemaji wa kamati hiyo.
Alisema katika Kikao kilichopita cha Bunge kiliipa jukumu Kamati
hiyo kuchunguza vurugu zilizotokea bungeni hapo, na kueleza kuwa Kamati
hiyo ilianza kufanya kazi ya kuchunguza wakati vikao vya bunge
vikiendelea mjini Dodoma.
Alisema baada ya kukamilisha kufanya kazi ya kuchunguza vurugu
zilizotokea bungeni hapo, Kamati hiyo ili kabidhi orodha ya baadhi ya
wabunge waliowabaini kuwa ni chanzo cha vurugu hizo na ikawataja katika
kikao cha bunge kilichopita.
Aliongeza kuwa baada ya Kamati kumaliza kazi ya kuchunguza na
kuwataja wahusika hao kikabaki kipengele cha kutoa adhabu kwa wahusika
waliobainika kuwa chanzo cha vurugu.
Ndugai alisema bunge baada ya kupata majina hayo ikaona ni vyema
wabunge hao wahojiwe na kujitetea mbele ya kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge kabla ya adhabu kutolewa dhidi yao.
Alisema kuna uwezekano mkubwa kwa wabunge hao kuanza kuhojiwa na
Kamati hiyo kwa sasa kwa kuwa vikao vya bunge vinakaribia kuanza na
adhabu inatakiwa kutolewa katika vikao vitakavyoanza hivi karibuni.
Mwisho.
Wakati huo huo, Mbowe ametangaza tamko la Musoma kwamba Machi 25,
mwaka huu, katika majiji manne; Arusha, Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam,
yatafanyika maandamano makubwa yakihusisha kila raia mwema mwenye
kuitakia elimu mema nchi hii, kuandamana ili Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, na Naibu wake, Philip Mulugo, wang’oke
madarakan kutokana na matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka
jana.
Katika matokeo yaliyotangazwa mwaka huu na Kawambwa Februari 8
mwaka huu, yalionyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6
wamepata sifuri, huku 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo
waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wamepata daraja la
nne.
Dk. Kawambwa alisema watahiniwa walikuwa 456,137, wa shule wakiwa 397,136 huku wa kujitegemea wakiwa 68,806.

Comments
Post a Comment