Wabunge wamembebesha RC Arusha zigo
Mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Mulongo.
Wabunge hao wanadai kuwa miongoni mwa shughuli ambazo Mulongo
anawatenga zinahusisha ziara za viongozi wa kitaifa na wa kimataifa.
Kwa nyakati tofauti wabunge hao walisema Mulongo amekuwa kikwazo
katika mkoa huo kwani tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha
amekuwa akiwashirikisha wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) peke yao
katika matukio mbalimbali yanayofanyika mkoani humo huku akiwatenga wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wabunge hao wa Chadema walitoa mfano wa ziara ya wiki iliyopita ya
Waziri Mkuu wa Denmark, Helle Schimidt, aliyoifanya katika wilaya za
Arumeru, Arusha Mjini na Monduli kuwa hawakujulisha ujio wa kiongozi
huyo licha ya kwamba wao ni wawakilishi halali wa wananchi katika
majimbo hayo.
“Mimi nilishasahau kabisa mialiko kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Arusha kunapokuwa na ziara kama Rais, Waziri Mkuu au kiongozi yeyote
kutoka nje, huwa naishia kusikia ving’ora kama wananchi wengine na baada
ya kuulizia ndipo naelezwa kuwa kuna kiongozi fulani wa kitaifa,”
alisema Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.
Lema alisema kuwa Isdory Shirima alipokuwa Mkuu wa mkoa huo,
wabunge wa vyama vya upinzani walikuwa wakipata ushirikiano wa kutoka
ofisi ya mkuu wa mkoa, lakini tangu ateuliwe Mulongo kushika wadhifa
huo, hawashirikishi kabisa.
“Ujio wa Waziri Mkuu wa Denmark nilikuwa sifahamu, lakini siku hiyo
wakati amefika Arusha nilimpigia simu Mkuu wa Mkoa wa Arusha kumuomba
‘appointment’ (miadi) ya kuonana naye tujadiliane suala la kufungwa kwa
barabara ya Kanisa ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi ndipo
akanieleza niende uwanja wa ndege nikaonane naye huko kwa sababu alikuwa
anamsubiri Waziri Mkuu wa Denmark,” alisema Lema.
Waziri Mkuu wa Denmark katika ziara yake mjini Arusha, alitembelea
Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) na Makao
Makuu ya Ofisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akiwa katika Jimbo la Arumeru Mashariki, alitembelea Chuo cha
Mafunzo ya Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (TCDC) na wakati wa
ziara ya Jimbo la Monduli alitembelea Boma la kimasai lililoko katika
kijiji cha Nanja.TCDC inaendeshwa kw ushirikiano wa serikali ya Tanzania
na Denmark.
Lema alisema siyo kwamba anang’ang’ania kualikwa katika matukio
muhimu, lakini serikali ya mkoa wa Arusha lazima itambue kuwa yeye ni
mbunge halali ambaye alichaguliwa na maelfu ya wananchi wa Arusha, hivyo
ni lazima utaratibu ufuatwe wa kumwalika kama mwakilishi wa wananchi.
Naye Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse, alisema
hawapewi ushirikiano na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha pamoja na ofisi
za wakuu wa wilaya wakati wao ni wawakilishi wa wananchi kwenye majimbo
yao.
“Ushirikishwaji ni dhaifu sana kwa RC (Mkuu wa Mkoa) na DC (Mkuu wa
Wilaya), viongozi wa kitaifa wanapofanya ziara katika majimbo yetu
hatujulishwi na tukiuliza tunaambiwa hayo ni mambo ya ‘private’
(binafsi),”alisema Mchungaji Natse.
Mchungaji Natse alisema pamoja na mkakati wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa
na Mkuu wa Wilaya wa kuwatenga katika matukio muhimu, wanashukuru kuwa
wananchi katika majimbo yao wanawaamini sana, hivyo mpango huo kama
unalenga kutaka kuwadhoofisha kisiasa, kamwe hautafanikiwa. Kwa upande
wake Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, alisema kama
ilivyo kwa wabunge wenzake wa vyama vya upinzania, naye amekuwa
akitengwa kwa kutojulishwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha
kunapotokea ziara za viongozi wa kitaifa na wa kimataifa.
Baadhi ya matukio ambayo wabunge hao walitengwa ni uzinduzi wa
jengo la Makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Uziduzi wa
Halmashauri ya Jiji la Arusha. Mulongo alipoulizwa na Jamileotz kuhusiana
na malalamiko ya wabunge hao, alisema amekuwa akiwapatia taarifa za
kushiriki katika shughuli mbalimbali kwa kuwapigia simu na siyo kwa
kuwaandikia barua kama wanavyotaka. Mulongo alisema kuwa hata hivyo,
wabunge hao wa upinzani licha ya kujulishwa, wamekuwa wakitoa udhuru
kwamba hawatahudhuria.
“Wanang’ang’ania niwaandikie barua, mambo hayo yalishapitwa na
wakati, mimi kama Mkuu wa Mkoa ninapokupigia simu bado tu huamini
unataka mpaka nikuandikie barua, mbunge hata akinisema hainipunguzii
chochote kwa sababu kwanza kazi yangu siyo kualika wabunge,” alisema
Mulongo. Mulongo alisema baadhi ya wabunge wanataka wapewe mialiko kwa
barua wakati baadhi yao hawakai hata katika ofisi zao. Hata hivyo,
hakuwataka kwa majina.

Comments
Post a Comment