Wafanyakazi 50 A TO Z waacha kazi
Wafanyakazi
zaidi ya 50 kutoka mkoani Tanga wa kiwanda cha kutengeneza vyandarua
cha A TO Z, jijini hapa wameacha kazi kwa madai ya kupunjwa posho zao.
Wakizungumza na mwandishi wa blogu hii, wafanyakazi hao ambao ni sehemu ya 250
waliotoka mkoani Tanga na kuajiriwa kwenye kiwanda hicho, walisema
wameamua kuacha kazi na kurudi nyumbani kwao baada ya mwajiri wao
kuwahadaa kwamba angewalipa mshahara mnono na kuwapatia malazi na
chakula bure kitendo ambacho hakikuwa hivyo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wafanyakazi hao, Raymond
Erasto, alisema kilichowafanya waamue kuacha kazi katika kiwanda hiyo
ni pamoja na manyanyaso ambayo wamekuwa wakiyapata ikiwemo kupewa
chakula kisichofaa ambacho ni ugali na mchuzi wa maharage yenye wadudu.
‘’Wakati wanakuja kutuchukua mkoani Tanga walituahidi mshahara
mnono wa Sh. 250,000 kwa mwezi, kulala bure, lakini cha ajabu chumba
tunacholala watu wanne tunakatwa kila mmoja sh. 30,000 kila mwisho wa
mwezi,’’ alisema Erasto.
Alisema kilichobainika ni kwamba malipo hayo yalikuwa na makato
mengi kiasi cha kujikuta baadhi yao wakiambulia Sh. 30,000 kwa mwezi.
Mfanyakazi mwingine Athumani Salimu aliutuhumu uongozi wa kiwanda
hicho kwa kushindwa kujali maslahi ya wafanyakazi hao kwani kazi
wanayoifanya ni ngumu na haiendani na malipo wanayopewa na kukitaka
kiwanda hicho kuwatendea haki wafanyakazi wake kwani ipo hatari ya
kukimbiwa na wengine iwapo hawatajirekebisha.
Naye Afisa mwajiri wa A TO Z,Godwin Obed akizungumza kwa njia ya
simu kutoka mkoani Tanga alikanusha wafanyakazi hao kulipwa Sh 30,000
kwa mwezi na kufafanua kuwa baadhi yao hawaingii kazini na taratibu za
kiwanda ni lazima wakatwe sehemu ya malipo yao.
Aliongeza kuwa wafanyakazi hao hulipwa vizuri stahili zao kama
makubaliano yalivyokuwa, ila kuna makato ya kisheria kama NSSF na
mengine ambayo ni lazima yakatwe, hivyo kitendo cha kudai kwamba
wanalipwa kidogo na kupewa chakula kibovu hayana ukweli wowote.
''Sisi tumechukua wafanyakazi 250 kutoka Tanga kwa hiyo hao 50
unaosema wameachakazi hawatusumbui wao waende watakuja wengine,''alisema
Obed kwa njia ya simu.

Comments
Post a Comment