Wakulima na wafugaji wazichapa Pangani
Mapigano
makubwa yameibuka katika vijiji vitatu wilayani Pangani baina ya
wakulima na wafugaji wa kabila la Wamang'ati kutoka mkoani Manyara na
kusababisha baadhi ya wakulima kujeruhiwa na wengine kulazwa
hospitalini.
Mgogoro huo umetokana na madai kuwa
wafugaji walivamia mashamba ya wakulima katika vijiji vya Masaraza,
Mivumo na Kigurusimba Kata ya Bushiri huku wakiwa na mishale kufuatia
hali ya ukame inayoukabili mkoa wa Tanga na mingine ya jirani.
Wakizungumza katika kikao kilichoitishwa
na Mkuu wa mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa, baadhi ya wakulima
wamewashutumu baadhi ya viongozi wa serikali ngazi ya wilaya kwa
kuwakaribisha wafugaji hao kwa makubaliano yao binafsi bila
kuwashirikisha wananchi katika utoaji wa maamuzi.
Walisema kutokana hali hiyo, wafugaji
wamekuwa wakijichukulia sheria mikononi na bila kujali wamekuwa
wakivamia maeneo yao na kulisha mifugo hivyo kuharibu mazao mashambani.
“Wao ni wavamizi lakini wanajiona ndio
wamiliki halali wanaingiza mifugo yao kila mahali na hakuna wa kuwahoji
kimsingi hali hii imetuchosha sana," alisema Saimon Luoga mkulima wa
Kijiji cha Kigurusimba.
Wafugaji hao huharibu pia vyanzo vya maji
hivyo wakazi wa vijiji hivyo wanaiomba serikali kuingilia kati mgogoro
kwani ipo hatari ya kukosa kabisa maji kwa matumizi ya binadamu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
wilaya ya Pangani, Neneka Rashid alisema kuwa wameunda tume ya
kuchunguza tatizo hilo lakini bado wafugaji wamekuwa wakikaidi agizo la
mkuu wa wilaya la kuwataka waondoke katika vyanzo vya maji.
Kufuatia hatua hiyo Mkuu wa mkoa wa Tanga
Chiku Gallawa, amewaagiza wafugaji wote walioingia kinyume cha utaratibu
kuondoka mara moja kabla serikali haijatumia nguvu kuwaondoa

Comments
Post a Comment