Wanafunzi waliofukuzwa vyuo vikuu waomba msaada wa JK
Rais Jakaya Kikwete
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Philipo Mwakibinga, mmoja kati ya wanafunzi waliofukuzwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), alisema wameamua kumwomba Rais Kikwete kuingilia kati baada ya kuona jitihada zao zikikwamishwa na baadhi ya viongozi wa serikali.
Mwakibinga alisema kitendo cha kuwafukuza na kuwazuia wanafunzi zaidi ya 145 wasidahiliwe na chuo chochote nchini ni cha uonevu ambacho licha ya kuwanyima haki yao ya msingi, kitapoteza idadi kubwa ya rasilimali watu ambayo itapelekea upungufu wa wataalam kama madaktari, wahandisi, wachumi, wahasibu, wahadhiri pamoja na wanasayansi.
“Tunamuomba Rais Kikwete alichukulie jambo hili kwa uzito unaostahili, huku akiangalia mustakabali wetu na wa Taifa kwa ujumla,” alisema Mwakibinga.
Aliongeza kuwa tabia ya kuwafukuza wanafunzi imekuwa ni janga la kitaifa katika vyuo vikuu nchini na kwambaikiwa litafumbiwa macho, taifa idadi kubwa ya wanafunzi watafukuzwa vyuoni kila uchao.
Mwakibinga alisema wanafunzi waliofukuzwa kuanzia 2011 mpaka sasa ni 145, ambao walikuwa mstari wa mbele kudai haki yao ya kupewa mafunzo kwa vitendo, kudai vifaa pamoja na mazingira bora ya kujifunzia, kudai kurejeshwa kwa serikali ya wanafunzi iliyofutwa na watawala wa chuo. Mengine ni kudai mikopo ambayo inawasaidia kulipa ada na kujikimu wanapokuwa vyuoni.
Umoja huo unaundwa na wanafunzi waliofukuzwa kutoka UDSM, Chuo Kikuu cha Doddoma (Udom), Chuo Kikuu Kishiriki Muhimbili (Muhas), Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu Kishiriki cha Biashara na Ushirika Moshi (Muccobs), Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo Kikuu cha Mtakatifu John (STJN).

Comments
Post a Comment