Wasomali wanatafuta kazi serikalini bila ya kuiogopa al-Shabaab




Wasomali vijana wenye elimu ya vyuo vikuu wameanza kutafuta ajira katika mashirika ya serikali, wakiwa huru kutokana na woga uliodumu kwa muda mrefu baada ya wanachama wa al-Shabaab kufukuzwa mjini Mogadishu mwezi Agosti 2011.



Wanafunzi wakihudhuria masomo katika shule ya sekondari kwenye mji wa Somaliland wa Sheikh. Serikali kwa sasa inaajiri wahitimu wa vyuo vikuu kujaza nafasi katika wizara. [Na Tony Karumba/AFP]

Mohamed Adam Ahmed, mwenye umri wa miaka 30 na mhitimu wa Chuo Kikuu cha Mogadishu kwenye kitivo cha Biashara na Uendeshaji, alianza kufanya kazi katika wizara ya Masuala ya Umma kwenye idara ya uhusiano wa kanda miezi mitatu iliyopita. Hivi sasa, anasema anashangazwa kuwa hajakumbana na hatari yoyote ambayo alikuwa anatarajia.

"Nilikuwa nikiamini kuwa usalama wangu ungekuwa hatarini kama ningeanza kufanya kazi seriklalini kwa sababu nilikuwa ninasikia kuwa waajiriwa wa serikali wanauliwa," aliiambaia Sabahi, na kuongeza kuwa alikuwa anaogopa kutembelea ofisi za serikali.

Akiwa na fursa chache za ajira, Ahmed aliomba kazi bila kujali hatari. Bado, alisema kuwa hakuwa na imani kuwa angeweza kuajiriwa, kwa vile kazi nyingi zilitolewa kwa uaminifu wa ukoo siku za nyuma. Lakini mambo yamebadilika.

Nafasi nyingi za kazi katika mashirika ya serikali zinatangazwa katika mtandao wa Redio Mogadishu inayosimamiwa na serikali.

"Nina furaha kwa sababu kila mtu anayefikiriwa kwa kazi serikalini lazima afanyiwe jaribio la sifa zake. Nahisi hili linakuza elimu na utawala wa sheria," alisema.

Deqa Abdi Omar, mwenye umri wa miaka 27 ambaye alikuwa mwajiriwa wa Wizara ya Wanawake na Masuala ya Familia katika Serikali ya Mpito ya Shirikisho, sasa anafanya kazi kama mkuu wa jarida katika Wizara ya Masuala ya Umma.

Alisema kuwa maisha yake kama mfanyakazi wa serikali yameimarika sana tangu mwaka uliopita.

"Mwanzo nilikuwa ninapokea vitisho vya kifo kutoka kwa al-Shabaab kwa njia ya simu mpaka nilipobadilisha nambari yangu," aliiambia Sabahi. "Lakini sasa, namshukuru Mwenyezi Mungu, ninaweza kwenda wilaya yoyote ya Mogadishu kama mwajiriwa wa serikali, hata huko Suqa Holaha," alisema, akimaanisha iliyokuwa ngome imara ya al-Shabaab.

Khadar Ali, mwenye umri wa miaka 35, alisomea sayansi ya kompyuta katika Chuo Kikuu cha Nairobi, ambako alisema alikuwa na ndoto ya siku moja kurejea Somalia bila ya woga.

"Leo nina furaha kwamba nimereja katika nchi yenye amani na elimu ambayo itaniwezesha kuwanufaisha watu wangu," aliiambia Sabahi.

"Nilipeleka maombi mengi katika wizara za serikali ya shirikisho ya Somalia," alisema. "Nina matumaini makubwa kuwa marafiki znagu na mimi tutaanza kazi katika Wizara ya Habari, Posta na Mawasiliano ya Simu hivi karibuni kwa sababu tulifuzu mtihani."

"Wakati nilipokuwa nje ya nchi, niliamini kuwa maamuzi ya ajira yalihusika na wale waaminifu kwa koo tu, lakini sasa ni kitu cha kufurahia ikiwa watu wanatathminiwa kwa mujibu wa elimu yao," alisema na kuwataka Wasomali wanaoishi nje kurejea nyumbani na kugawana ujuzi na elimu yao ili kuijenga upya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Vijana na Michezo Aweys Sheikh Hadaad alisema kuwa serikali ya shirikisho inafanya kazi ngumu ya kujenga upya asasi kwa misingi ya usawa wa fursa na kuajiri na kuwaendeleza watu kwa misingi ya sifa. Serikali pia inafanyia kazi mipango ya kukuza ukuaji kwa ubia na sekta binafsi, katika juhudi za kuwapa vijana wa Somalia mbadala ulio bora kuliko itikadi kali na uharamia, aliimbia blogu hii.

Comments

Popular Posts