Watu tisa wafa, 53 wajeruhiwa ajalini
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman
Katika tukio la kwanza, watu sita walikufa papo hapo na wengine 25 kujeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Lilongwe nchini Malawi kwenda jijini Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka katika kijiji cha Igawa wilayani Mbarali, mkoa wa Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, jana alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 3:30 usiku ikihusisha basi la kampuni ya Easy lenye namba za usajili Y 405 AJQ aina ya Scania.
Alisema miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo, watano kati yao ni raia wa Malawi na mmoja ni Mtanzania.
Kamanda Diwani aliwataja waliokufa kwenye ajali hiyo ambao wametambuliwa kwa jina moja moja kuwa ni Asam, mkazi wa wilaya ya Baraka nchini Malawi, Bonzo, Maria, Adam Sakwati na mtoto mdogo wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja wote wakazi wa Zingwangwa- Blantyre, Malawi.
Alisema mtu wa sita aliyeafariki ni Mtanzania Rajabu Hassan (35) ambaye alikuwa kondakta wa basi hilo aliyefariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ilembula mkoani Njombe.
Kamanda Diwani alisema majeruhi ni 25, kati yao wanaume ni 14 na wanawake ni 11 na kuwa wote wamelazwa katika Hospitali ya Ilembula.
Alisema miili ya marehemu watano raia wa Malawi imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, ikisubiri ndugu na jamaa kufika kuichukua kwa ajili ya shughuli za mazishi.
Kwa mujibu wa Kamanda Diwani, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi lenye namba za usajili T 491 BBJ aina ya Nissan, mali ya kampuni ya Taqwa, Keneth Thomas (48), mkazi wa Kabwe jijini Mbeya ambaye alijaribu kulipita basi la Easy, lakini kwa mbele alikutana na gari lingine, hivyo aliamua kurudi ghafla upande wake na kusababisha basi la Easy kupoteza uelekeo na kuacha njia.
Alisema dereva Thomas amekamatwa na Polisi kuhusiana na ajali hiyo, lakini dereva wa basi la Easy, Ajali Mohamed, alikimbia baada ya kutokea kwa ajali hiyo.
Kamanda Diwani alisema kuwa hivi sasa taratibu za kumfikisha mahakamani mtuhumiwa Thomas zinafanyika na kuwa zitakapokamilika atasimamishwa kizimbani.
Kamanda Diwani ametoa wito kwa madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
WATATU WAFA, 28 WAJERUHIWA MWANZA
Katika tukio la pili, watu watatu wamekufa papo hapo na wengine 28 wamejeruhiwa baada ya basi lililokuwa likisafiri kutoka Musoma kuelekea Mwanza kugongana uso kwa uso na lori la mchanga katika eneo la Nyamhongolo nje kidogo ya jijini la Mwanza.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ernest Mangu, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa, ajali hiyo ilitokea jana saa 4:30 asubuhi kwa kuhusisha basi la kampuni ya Marquis lenye namba za usajili T 961 AGP na lori aina ya Fuso lenye namba za usajili T 671 ABY, mali ya Salum Transport.
Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Hamis Musa, Shija Musa na dereva wa Fuso aliyetambuliwa kwa jina la Andrew Omela na kwamba miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Kamanda Mangu alisema majeruhi 28 wa ajali hiyo walipelekwa katika hospitali hiyo kwa matibabu na kwamba kati yao wanaume ni 18 na wanawake ni 10.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa basi ambaye alijeruhiwa vibaya baada ya kukatika miguu yake yote miwili.
Awali mashuhuda wa ajali hiyo walisema kwamba, ilitokea baada ya askari waliokuwa katika operesheni ya kukamata magari yanayosafirisha mchanga wa ujenzi kusimamisha lori la mchanga bila kuchukua tahadhari.
Walidai kwamba mmoja wa askari hao akiwa na maofisa wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) Kanda ya Ziwa, alisimamisha lori moja lililokuwa limebeba mchanga ndipo lori lingine lililokuwa nyuma yake likagongana uso kwa uso na basi ambalo pia lilikuwa kwenye mwendo kasi.
Comments
Post a Comment