Chadema waenda Dodoma kuwawinda Makinda, Ndugai
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alipozungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema Kamati Kuu imewaagiza wabunge wote wa chama hicho kujipanga na kuhakikisha Spika na Naibu wanang'olewa kutokana na kushindwa kufuata kanuni za Bunge.
Mkutano wa 11 wa Bunge unaanza kesho mjini Dodoma kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali pamoja na kupitisha bajeti ya serikali kwa mwaka 2013/14.
Mnyika alisema Kamati Kuu ilipokea taarifa ya masuala yaliyotokea katika vikao vya Bunge lililopita, zikiwamo vurugu zilizotokea kwa wabunge kusimama na kuimba.
Alisema kikao hicho kilijadili na kuazimia kuwa hali hiyo ya kuyumba kwa uendeshaji wa mhimili wa Bunge na yote yanayotokea bungeni ni kwa sababu ya ukiukwaji wa kanuni unaofanywa na Spika na Naibu wake.
"Kamati Kuu imebariki hatua zote zilizochukuliwa awali kuhusu masuala yaliyojitokeza bungeni, ikiwamo kuwataka wabunge wasiende kwenye Kamati ya Ngwilizi (Kamati ya Haki na Madaraka ya Bunge)," alisema.
Alisema Kamati Kuu imeazimia na kuagiza Kambi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chadema ichukue hatua za kibunge juu ya Spika na Naibu wake. Mapema mwaka huu baada ya vikao vya Bunge, kambi ya upinzani ilitoa maelekezo kwa wabunge wake wote kutafuta njia za kibunge za kumwajibisha Spika Makinda na Naibu wake kwa madai kwamba wameshindwa kumudu uendeshaji wa Bunge hasa katika matumizi ya kanuni.
Habari za ndani kutoka Chadema zinasema tangu kumalizika mkutano wa Bunge uliopita, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, amekuwa akiandaa 'muundo' ambao wabunge mbalimbali wa chama hicho wataweza kuutumia kumwajibisha Spika na Naibu Spika.
Akizungumza na jamiileotz kwa njia ya simu jana jioni, Lissu alikiri kwamba wabunge wa Chadema wamepania kumng'oa Spika na Naibu wake kwa kutumia mbunge mmoja mmoja kuwasilisisha hoja ya kutokuwa na imani na viongozi hao.
Alisema kanuni za Bunge zinamruhusu mbunge yeyote kuwasilisha hoja binafsi bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na wabunge na kisha kupiga kura za kumng'oa Spika na Naibu wake.
Kanuni ya Bunge namba 134 (1) inasema mbunge yeyote anayetaka kumwondoa Spika madarakani chini ya Ibara ya 84 kifungu cha 7 (d) ya Katiba atawasilisha taarifa ya maandishi kwa Katibu wa Bunge akielezea sababu za kutaka kupeleka hoja hiyo bungeni.
Pia kanuni hiyo hiyo kifungu cha (5) inasema ili hoja hiyo iweze kujadiliwa ni lazima iungwe mkono na theluthi mbili ya wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katibu wa Bunge atawasilisha hoja hiyo kwa Kamati ya Bunge Haki, Maadili na Madaraka kwa ajili ya kujadiliwa; kama kamati ikiridhika kuna tuhuma mahususi zinazimhusu Spika, hoja hiyo itawasilishwa bungeni.
Kuhusu Bunge kukataa kupokea hoja za namna hiyo, Lissu alisema hata kama ikitokea hivyo haiwazuii kuwasilisha hoja hiyo bungeni kama walivyopanga.
Wakati huo huo, Kamati Kuu ya chama hicho imeshangazwa na danadana inayofanywa na vyombo vya dola nchini, hususan Jeshi la Polisi nchini katika matukio kadhaa yanayotishia usalama wa raia na mali zao.
Mnyika alisema chama hicho kinasikitishwa na ukimya wa Rais Jakaya Kikwete na kushindwa kutumia mamlaka yake kikatiba kuunda chombo huru kuchunguza matukio ili ukweli ubainike. Aidha, chama hicho kimehoji mazingira ya uhusiano baina ya matukio mawili ya kinyama yaliyohusisha kiongozi wa madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka na lile la Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, waliotekwa na kisha kupigwa usiku.
Alisema chama hicho kinayaona matukio hayo ni makubwa na mazito, lakini serikali na chama tawala wamekuwa wakitumia matukio hayo kufanya propaganda na kuficha ukweli.

Comments
Post a Comment