KUPOROMOKA GHOROFA:Vigogo kortini
Baadhi ya watuhumiwa wa kesi ya kuua bila
kukusudia kufuatia kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 jijini Dar es
Salaam na kusababisha vifo vya watu 36 wakiwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu jana.
Mbali na Kisoki, mshtakiwa mwengine ni Raza Hussein Ladha ambaye inadaiwa kuwa ndiye mmiliki wa jengo hilo.
Pia wamo Goodluck Mbanga, Willibrod Mugyabuso, Mohamed Abdulkarim
ambaye hati ya mashitaka inamtaja kuwa ni mhandisi, Charles Ogare
(mhandisi), Zonazea Oushoudada (mhandisi mshauri), Vedasto Ruhale (mpima
ardhi), Michael Hema (mjenzi), Albert Mnuo na Joseph Ringo.
Washtakiwa hao walifikishwa katika viunga vya mahakama hiyo jana
saa 7:34 mchana wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi wakiwa
kwenye gari lenye namba za usajili T 220 AMV, T 778 AFG aina ya Toyota
Land Cruiser.
Saa 8:00 walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Devota Kisoka.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na jopo la mawakili wa serikali
waandamizi, Bernad Kongola, Tumaini Kweka na mawakili wa serikali,
Ladslaus Komanya, Mohamed Salum, Mutalemwa Kishenyi na Neema Haule.
Kongola alidai kuwa katika shtaka la kwanza, Machi 29, mwaka huu
mtaa wa Indri Gandh, wilaya ya Ilala, washtakiwa kwa pamoja walimuua
bila kukusudia Yusuph Khari.
Kongola alidai katika shtaka la pili na la tatu, Machi 29, mwaka
huu, washtakiwa waliwaua bila kukusudia Kulwa Alfani na Hamada Musa.
Katika shtaka la nne na la tano, ilidaiwa kuwa Machi 29, mwaka huu
katika mtaa huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua bila kukusudia
Kessy Manjapa na Khamis Mkomwa.
Komanya alidai katika shtaka la sita na la saba, Machi 29, mwaka
huu katika mtaa huo, washtakiwa waliwaua bila kukusudia Boniface Bernad
na Suhail Karim.
Upande huo wa Jamhuri ulidai katika shtaka la nane na la tisa,
Machi 29, mwaka huu katika mtaa huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua
bila kukusudia Salmani Akbar na Selemani Haji.
Wakili wa serikali Haule aliendelea kusoma hati hiyo ya mashtaka
kwa kudai kuwa katika shtaka la 10 na 11, Machi 29, mwaka huu katika
mtaa huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua bila kukusudia Selemani
Mtego na Sikudhani Mohamed.
Ilidaiwa katika shtaka la 12 na 13, Machi 29, mwaka huu katika mtaa
huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua bila kukusudia Ahmed Milambo
na Salum Mapunda.
Shtaka la 14 na 15, ilidaiwa kuwa Machi 29, mwaka huu katika mtaa
huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua bila kukusudia Suleimani Mnyani
na John Majewa.
Shtaka la 16 na 17, ilidaiwa kuwa Machi 29, mwaka huu katika mtaa
huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua bila kukusudia Mussa Mnyamani
na David Herman.
Kweka alidai katika shtaka la 18 na la 19 kwamba Machi 29, mwaka
huu katika mtaa huo, washtakiwa waliwaua bila kukusudia William Joakim
na Abdulrahman Mwiha.
Alidai katika shtaka la 20 na 21 kwamba Machi 29, mwaka huu mtaa wa
huo, washtakiwa wote kwa pamoja waliwaua bila kukusudia Emmanuel
Christian na Mmanyi Ngadula.
Kweka aliendelea kusoma hati hiyo, shtaka la 22 na la 23, kwa kudai
kuwa Machi 29, mwaka huu mtaa huo washtakiwa wote kwa mapoja waliwaua
bila kukusudia Adivai Desiki na Ammanuel Wahai.
Katika shtaka la 24, ilidai kuwa Machi 29, mwaka huu katika mtaa
huo, washtakiwa wote kwa pamoja walimuua bila kukusudia Agustino Chuma.
Baada ya washtakiwa kusomewa mashitaka yao, hawakutakiwa kujibu
chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo
hadi upelelezi utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda
ya Dar es Salaam.
Upande wa utetezi uliongozwa na jopo la mawakili wa kujitegemea,
Jerome Msemwa, Joram Msemwa, Henry Mataba, Martin Rwehumbiza na George
Ogunde.
Jerome aliwaelekeza washtakiwa hao kwamba hawatakiwi kujibu
chochote kwa sababu kesi hiyo itasikilizwa Mahakama Kuu na kwamba kwa
sasa iko kwenye usikilizwaji wa awali.
Wakili Jamhuri, Salum alidai kuwa mashtaka yanayowakabili
washtakiwa ni kuua bila kukusudia na yamefunguliwa chini ya kifungu cha
195 cha sheria ya kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002
na mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana.
“Kwa mujibu wa mashitaka hayo hii siyo mahakama itakayosikiliza
kesi hii, washtakiwa mnatakiwa kuwa kimya kwa sababu mko kizimbani kwa
ajili ya kujulishwa kwa nini mnashikiliwa na kutuhumiwa,” alisema Hakimu
Kisoka.
Hata hivyo, Jerome alidai kuwa mashitaka yanayowakabili washtakiwa
yana dhamana na kwamba mahakama ya Kisutu ina mamlaka ya kusikiliza
maombi na kutoa dhamana kwa washtakiwa.
“Kwa mujibu wa sheria namba 148 kifungu cha 5 (a) cha Mwenendo wa
Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), kinaeleza wazi mashitaka ambayo hayana
dhamana, lakini kosa la kuua bila kukusudia halipo kwenye sheria hiyo
inayozuia dhamana,” alidai Jerome.
Wakili wa Jamhuri, Kongola alidai kuwa hoja za utetezi hazina
mashiko kwa sababu kesi hiyo imefikishwa mahakamani hapo kwa mara ya
kwanza na kwamba hakuna sababu ya kutoa malalamiko.
Aidha, upande wa Jamhuri uliomba mahakama iwapo itaona kwamba ina
mamlaka ya kutoa dhamana kwa washtakiwa ijielekeze kwenye mazingira ya
tukio la kesi inayowakabili washtakiwa na usalama wao.
Hakimu Kisoka alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili,
mahakama itatoa uamuzi Aprili 16, mwaka huu na kuamuru washtakiwa
wapelekwe mahabusu.
TIBAIJUKA ATANGAZA KIAMA
SERIKALI imetangaza kiama kwa wa miliki wa majengo ya ghorofa
kuanzia 11 na kuendelea katika eneo la Indra Ghandhi, jirani na
lilipoporomoka ghorofa hilo na kuua watu 36, kwa maelezo yamekiuka
sheria za mipango miji.
Kutokana na tukio hilo, serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amesema Wizara yake jana imetoa kibali cha kubomolewa kwa jengo pacha.
Alisema zoezi la ubomaji wa maghorofa hayo hauhitaji uchunguzi,
majadiliano, kamati wala tume yoyote bali kutekeleza kazi ya kubomoa inayopaswa kufanywa na mmiliki wa jengo husika.
Alisema kwenye eneo hilo kwa mujibu wa mipango miji ngazi ya Wizara
haitakiwi kujengwa ghorofa zaidi ya kumi kwa kuwa maeneo yake ni madogo
na hayawezi kustahimili majengo makubwa, lakini wapo wamiliki wamejenga
zaidi ya idadi hiyo.
“Hivi sasa ninavyozungumza nanyi, naelekea ofisini kusaini kibali
cha kubomoa jengo hilo kesho (leo), nitatoa tamko rasmi, sheria inamtaka
mmiliki kubomoa kwa gharama zake,” alisema.
Alisema shughuli hiyo itakwenda sambamba na kubomoa majengo mengine
yaliyo zaidi ya ghorofa kumi kwenye eneo hilo na kwamba eneo la
Kariokoo wamebaini kuwapo kwa majengo yaliyokiuka taratibu za ujenzi.
Prof. Tibaijuka alisema Wizara inasimamia mipango na halmashauri
zinahusika katika kusimamia ujenzi, hivyo kulikuwapo na udhaifu katika usimamizi ya ujenzi wa maghorofa hayo.
Alisema Wizara itafanya upembuzi wa kitaalamu kwenye maghorofa
mbalimbali jijini Dar es Salaam ili kubaini kama yalijengwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia
Mchechu, alisema iwapo mmiliki wa jengo hilo atashindwa kubomoa na
serikali kufanya kazi hiyo atatakiwa kulipa gharama zote za kubomoa.
“Tulikuwa na mkataba wa makubaliano baina ya mmiliki, na alikubali,
anatakiwa kubomoa iwapo itatokea sheria za ujenzi zimekiukwa,” alisema.
IET YAUNDA TIMU KUCHUNGUZA
Katika hatua nyingine, Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET) imeunda
timu ya watalaamu saba kuchunguza mfumo mzima katika sekta ya ujenzi
nchini pamoja na ripoti ya tume ya Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa,
aliyoiunda mwaka 2006 ili kuona kilichopendekezwa wakati huo kama
kimetekelezwa.
Lowassa aliunda timu hiyo baada ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa eneo la Chang’ombe, jijini Dar es Salaam.
Kadhalika, watalaam hao wameitaka serikali kuweka kando masuala ya
siasa inapopewa ushauri wa kitalaamu ili kuepuka majanga zaidi kwa taifa
yakiwamo kuanguka kwa maghorofa.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Rais wa IET, Dk. Malima Bundala, alipozungumza na waandishi wa habari.
Timu hiyo ambayo itaanza kazi yake leo, itaongozwa na Ladslaus
Salem na wajumbe wake watatoka vyama vya makandarasi, wahandisi,
wafanyabiashara na wabunifu wa majengo na itakamilika ndani ya siku 14.
Dk. Bundala alisema ingawa serikali imeunda tume kuchunguza chanzo
cha kuanguka kwa jengo la ghorofa 16 jijini Dar es Salaam wiki
iliyopita, na wao kama wataalamu katika taasisi binafsi wameunda timu
hiyo ili kujikita kuangalia mfumo mzima katika sekta ya ujenzi nchini.
Alitaja mambo watakayochunguza kuwa ni kuangalia taasisi zenye
majukumu ya kisheria katika kusimamia ujenzi hususani wa maghorofa,
viwango vya ubora wa vifaa vinavyotumika katika ujenzi ikiwamo nondo,
saruji na vyumba vinavyotumika na kama taratibu za kazi zinafuatwa.
Dk. Bundala alisema timu hiyo itaangalia suala la usanifu na
usimamizi wa majengo na kwamba mapendekezo yao watayawasilisha
serikalini kwa kuwa ndiyo yenye mamlaka ya kufanya maamuzi.
Alisema watalaamu wanaounda timu hiyo wamebobea katika masuala ya
ujenzi na kwamba wao hawataki kutibu matokeo ya tatizo bali wanataka
kujua chanzo cha tatizo zima katika sekta ya ujenzi.
“Kila mwaka tunafanya mikutano yetu ya mwaka na kila mara huwa
tunatoa mapendekezo ya kitalaamu kwa serikali na itafika mahali tutaenda
sambamba na itaona umuhimu wetu,” alisema.
Kuhusu kuchunguza mapendekezo ya timu iliyoundwa na Lowassa, Dk.
Bundala alisema wataipitia ili kuona kilichopendekezwa kwa serikali na
utekelezaji wake umefikia wapi mpaka sasa.
Wiki iliyopita jengo la ghorofa 16 lililoporomoka liliporomoka
wakati likiendelea kujengwa kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na
Indira Gandhi jijini Dar es Salaam na kuua watu 36.

Comments
Post a Comment