MAUAJI YA PADRI:DPP AWAWASHIA MOTO POLISI
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa.
Padri Mushi ambaye alikuwa Paroko wa Kanisa Katoliki Minara Miwili
aliuawa kwa kupigwa risasi Febuari 17, mwaka huu katika eneo la Beitrasi
mjini hapa akiwa ndani ya gari alipokuwa akielekea kuongoza misa ya
Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Theresia, mjini Zanzibar.
Baada ya mauaji hayo, Rais Jakaya Kikwete alitoa kibali cha
kukaribisha maafisa wa FBI kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya
uchunguzi wa mauaji hayo na Machi 17, mwaka huu Jeshi la Polisi
lilimkamata Omar Mussa Makame kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Uchunguzi wa mwandishi wetu umebaini kuwa DPP baada ya kulipitia jalada la
uchunguzi wa mauaji hayo, juzi alitoa mwongozo kwa Jeshi la Polisi
kuendelea kumtafuta muuaji wa Padri Mushi.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, DPP aliliandikia barua Jeshi la Polisi
na kukabidhiwa juzi ikieleza sababu za ofisi yake kutofungua hati ya
mashtaka hadi sasa dhidi ya mtuhumiwa wa mauaji hayo.
Jeshi la Polisi limethibitisha kuipokea barua ya DPP ambayo
inaeleza kuwa ushahidi uliokusanywa katika jalada la kesi hiyo hauna
mashiko na kwamba mtuhumiwa hahusiki na mauaji hayo.
Chanzo cha habari kutoka Jeshi la Polisi kilieleza kuwa DPP
hajaridhishwa na uchunguzi wote uliokusanywa dhidi ya mtuhumiwa pamoja
na watuhumiwa watatu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya askari polisi, Said
Abdulrahman aliyeuawa kwa kupigwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa
wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar Oktoba
17, mwaka jana.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa,
alithibitisha hatua ya DPP kutupa uchunguzi wote wa jalada la mauaji ya
Padri Mushi na kuwataka waandishi wa habari kumtafuta DPP azungumzie
sababu za uamuzi wake wa kutokubaliana na uchunguzi wa Polisi.
Hata hivyo, alisema kwamba Jeshi la Polisi bado linaamini uchunguzi
walioufanya kwa kushirikiana na FBI hauna shaka na kwamba mtuhumiwa
huyo ana kesi ya kujibu mahakamani na wataendelea kumshikilia.
Alisema kwamba kwa mujibu wa sheria, Jeshi la Polisi jukumu lake ni
kuchunguza kesi na ofisi ya DPP jukumu lake ni kufungua hati ya
mashtaka na kutetea kesi mahakamani.
Hata hivyo, mwandishi wetu alipofika katika ofisi ya DPP, Katibu muhtasi
wake alisema amepokea maagizo kutoka kwa bosi wake kuwa waandishi wote
wa habari wanaofuatilia suala hilo, wamuone Kamishna wa Polisi kwa vile
kazi aliyopewa ya kupitia jalada la uchunguzi kabla ya kufungua kesi
ameikamilisha.
“Kamishna ndiye aliyeitisha mkutano na waandishi wa habari kuelezea
hatua iliyofikiwa pamoja na kukamatwa kwa mtuhumiwa, sasa awaite tena
amalizie kazi yake ya kuwaeleza hatua iliyofikiwa baada ya Mkurugenzi
kurejesha jalada la mauaji,” alisema Katibu muhtasi huyo.
Katika hatua nyingine, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya
Jinai, Yusuph Ilembo, jana alifika katika Mahakama Kuu ya Zanzibar,
kufuatia ombi lililofunguliwa mahakamani na wakili anayemtetea mtuhumiwa
wa mauaji, Abdallah Juma Mohamed.
Abdallah Juma amefungua ombi katika Mahakama Kuu kwa kutumia
kifungu cha sheria 390 cha sheria namba 7 ya mwenendo wa makosa ya jinai
ya mwaka 2004, akitaka Jeshi la Polisi litoe maelezo kwa nini mteja
wake hajafikishwa mahakamani ndani ya saa 24 tangu alipokamatwa Machi
17, mwaka huu.
Wakili Abdallah Juma akisaidiwa na mawakili Shaban Juma Bakari na
Shaibu Ibrahim Shaibu waliitaka Mahakama Kuu itoe amri ya kuachiwa kwa
mteja wao kutoka mikononi mwa Jeshi la Polisi. Hata hivyo, Ilembo
alisema kuwa kutokana na uzito wa kesi hiyo, anaomba kupewa muda wa
kutayarisha majibu ya hati ya kiapo kwa maandishi na kuuwasilisha kwa
upande wa utetezi na mbele ya mahakama hiyo kabla ya ombi hilo kuanza
kusikilizwa na kutolewa uamuzi.
“Tunaomba mtuhumiwa aendelee kushikiliwa na Polisi, wakati tukifanya matayarisho ya kujibu hati ya kiapo,” alisema Ilembo.
Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu, Mkusa Isaack Sepetu, alisema
baada ya kusikiliza pande zote mbili, alimtaka Ilembo awe amejibu kwa
maandishi hati ya kiapo ya maombi hayo kabla ya kuanza kusikilizwa kwa
shauri hilo Aprili 8, mwaka huu.
Aidha, Jaji alisema wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo, ametaka
mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani, baada ya hoja za upande wa mawakili
wanaomtetea kutaka dhamana kwa mteja wao, kwa vile bado hajafikishwa
mahakamani kwa tuhuma za mauaji.

Comments
Post a Comment