Moto wateketeza maduka Zanzibar
8th April 2013
B-pepe
Chapa
Moto mkubwa umeteketea maduka sita katika mtaa wa kibiashara wa darajani Mkoa wa mjini Magharibi, Zanzibar jana.
Moto huo ulianza kuwaka majira ya saa moja usiku na kusababisha mtafaruku mkubwa mjini humo kabla ya kudhibitiwa na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi visiwani Zanzibar, (KZU).
Mkuu wa Operesheni wa KZU, Simai Haji Simai, alisema chanzo cha moto huo ni cheche za moto zilizokuwa zimebakia baada ya mafundi kukamilisha kazi ya kuchomelea vyuma katika moja ya duka.
Alisema kwamba inaonejkana mafundi baada ya kukamilisha kazi, kuna cheche zilibakia kwa ndani na kusababisha moto katika maduka hayo ya bidhaa mbalimbali zikiwamo nguo na viatu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa mjini Magharibi Unguja, Azizi Juma Mohamed, hakupatikana kuzungumzia tukio hilo baada ya simu yake ya kiganjani kuiita bila kupokelewa.
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amewataka wafanyabiashara kuzingatia umuhimu wa kukata bima katika vitenga uchumi vyao.
Balozi Seif alitoa ushauri huo baada ya kukagua maduka yaliyoungua moto na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabishara wa maduka ya makontena Zanzibar.
Balozi Seif alisema wafanyabiasha wengi wamekuwa wakishindwa kuendelea na biashara zao wakati wanapopatwa na majanga mbalimbali na kushindwa kurejesha mtaji kutokana na vitenga uchumi vyao kutokuwa na huduma za bima.
“Sijui kwa nini wafanyabiashara wetu wamekuwa wagumu katika kukata huduma za bima kwa usalama wa mali zao,”alisema balozi Seif.
Balozi Seif aliwapa pole wafanyabiashara hao na kuwataka kuendelea kuwa na subra wakati huu mgumu wanaoendelea kukabiliana nao kutokana na tukio hilo.
Awali mfanyabiashara aliyeathirika na tukio hilo, Abdulla Hemed Khamis, alikishukuru kikosi cha zimamoto kwa juhudi walizochukua za kuzima moto huo.
Hata hivyo, alisema eneo biashara la darajani limekuwa likikumbwa na wizi wa mara kwa mara unaopelekea kuwavunja moyo wafanyabiashara na kuomba serikali kuimalisha ulinzi wa doria katika mtaa huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Makontena hayo, Suleiman Masuod, aliiomba Serikali kushajiisha wawekezaji kufikiria kujenga majengo makubwa ya biashara (Shooping Maul) kwa lengo la kuwaondolea usumbufu na biashara zao kuwa katika mazingira ya salama.
Suleiman alimueleza Balozi Seif kwamba majengo hayo yanastawisha maeneo ya mji na kutoa haiba inayovutia badala ya mfumo wa makotena kugeuzwa maduka ya biashara visiwani humo.
Matukio ya moto yamekuwa ya kawaida kutokea katika mtaa wa biashara wa darajani na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara kila mwaka visiwani hapa

Comments
Post a Comment