SOMA HAPA KUHUSIANA NA TUNDUMA INAVYOGEUKA KUWA DAFUR

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani.
Shughuli za kiuchumi katika mji wa Tunduma uliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia wilayani Momba mkoani Mbeya jana zilisimama kwa zaidi ya saa saba, kufuatia vurugu kubwa zilizoibuka ambazo chanzo chake kinadaiwa kuwa ni mgogoro wa kuchinja ng’ombe kwa ajili ya kitoweo baina ya Wakristo na Waislamu.

Vurugu hizo inadaiwa kuwa zilianza saa 3:00 asubuhi na kudumu hadi jioni huku baadhi ya vijana walijitokeza mitaani na kufunga bararabara kuu ya Tanzania na Zambia na kuchoma magurudumu ya magari pamoja na kurusha mawe hovyo,  hali ambayo ilisababisha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kutumia nguvu ya mabomu ya machozi, risasi za moto na silaha nyingine kuwatawanya.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, alisema kuwa vurugu hizo zilisababisha askari Polisi  mmoja na mwananchi mmoja kujeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Alisema kuwa pamoja na chanzo cha vurugu hizo kuwa mgogoro wa kuchinja baina ya Wakristo na Waislamu, lakini kuna kila dalili za siasa kujipenyeza kutokana na taarifa za kiintelijensia kubaini kuwa wapo wanasiasa waliochoche vurugu hizo.

Kwa mujibu wa Kamanda Diwani, watu 51 wanashikiliwa na Polisi kuhusiana na vurugu hizo na kieleza kuwa hali ya mpaka ilianza kuwa shwari kuanzia saa 11 jioni baada ya Jeshi la Polisi kufanya kazi kubwa ya kurejesha amani katika mji wa Tunduma.

Vurugu hizo zimeibuka ikiwa ni siku moja tu baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa mkoa huo, Abas Kandoro, kutembelea mji wa Tunduma na kukutana na viongozi wa dini za kikristo na Kiislamu na kukubaliana kuwa utaratibu wa kuchinja ng’ombe na mbuzi kwa ajili ya kitoweo cha jumuiya ubaki kama ulivyokuwa zamani ambao uliwaruhusu Waislamu kuchinja kutokana na imani yao

Comments

Popular Posts