HALI NI TETE MBEYA WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI LUPATA WACHOMA BWENI HABARI KAMILI IKO HAPA




Bweni moja la wanafunzi wa kiume katika Shule ya Sekondari Lupata inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi Wilayani Rungwe limeteketea kwa kuchomwa moto na baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakipinga kitendo cha uongozi wa shule hiyo kuwasimamisha masomo wenzao watatu kwa utovu wa nidhamu. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman (pichani), jana alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 2:00 usiku, baada ya wanafunzi waliosimamishwa masomo ku.....wahamasisha wenzao kupinga adhabu hiyo na kufanya vurugu.


Alisema tukio hilo limesababisha uharibifu mkubwa wa mali za shule hiyo ingawa moto huo haukusababisha madhara yoyote kwa binadamu.

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Diwani alisema chanzo ni wanafunzi watatu wa shule hiyo kusimamishwa masomo utokana na utovu wa nidhamu.

Alisema wanafunzi hao baada ya kusimamishwa masomo walianza kuwahamasisha wenzao kuwaunga mkono katika kupinga adhabu hiyo, jambo lililopelekea kufanyika kwa vurugu kubwa shuleni hapo.

Alisema bweni lilichomwa moto lilikuwa ni la wanafunzi zaidi ya 50 ambao hawakuwa tayari kuwaunga mkono wanafunzi hao, hali iliyosababisha wenzao kulichoma bweni walilokuwa wakilala.

Kamanda Diwani alisema jumla ya wanafunzi 15 wakiwemo waliokuwa wamesimamishwa masomo wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Rungwe kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na vurugu hizo.

Alisema tathimini ya uharibifu wa mali bado inaendelea kufanywa ili kujua thamani ya mali iliyoharibiwa na moto huo.

Comments