SOMA HAPA KAULI YA SERIKALI KUJENGA NYUMBA 6,000 ZA WANAJESHI
Na Abdalla Wellah
17th May 2013
B-pepe
Chapa
Kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 285 (Sh. bilioni 459) zitatolewa ukiwa ni mkopo na Serikali ya China na dola za Marekani milioni 15 zitachangiwa na Serikali ya Tanzania.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha, alisema hayo katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa nyumba hizo, iliyohudhuriwa pia na Mtaalamu Mkuu wa Mambo ya Kijeshi la China, Kanali Mwandamizi, Wu Xiaoyi, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema nyumba hizo zitajengwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo, utakaokamilika ndani ya miezi 50 katika mikoa 15 nchini, kwa kuanzia na mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Arusha.
Nahodha alisema mradi huo utasaidia kupunguza tatizo la makazi bora ya wanajeshi kwa kati ya asilimia 70 na 80.
Alisema hilo linatokana na ukweli kwamba, kwa muda mrefu serikali imekuwa ikiingia gharama kubwa kulipa kodi za nyumba zinazotumiwa na wanajeshi.
Hivyo, alisema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia pia kuondoa tatizo la wanajeshi kuchanganyika na raia, jambo ambalo limekuwa likipunguza nidhamu kwa wanajeshi.
Aliiambia Kampuni ya Shanghai Construction Group Limited ya nchini China itakayojenga nyumba hizo, kuwa kushindwa kwao kutekeleza makubaliano ya kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa utaalamu, kutafanya kuwa mwisho wa kuacha kufanya nao shughuli nyingine hapa nchini.
Aliwataka wadau wote, ikiwamo wizara na Kitengo cha Ushauri wa Huduma za Majengo cha Taifa kuheshimu makubaliano yaliyopo katika mradi huo.
“Nitatafuta nafasi ya ofisi hapa,” alisema Nahodha, huku akionyesha eneo mojawapo, ambako mradi huo utatekelezwa.
Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema kwa muda mrefu wamekuwa na kilio kuhusu ukosefu wa nyumba za maofisa wa jeshi, hivyo mradi huo umetimiza ndoto yao.
Comments
Post a Comment