KAMA ULISIKIA MWANAFUNZI WA CHUO KIKUU DSM AMEPIGWA RISASI HABARI KAMILI IKO HAPA
22nd June 2013
B-pepe
Chapa
Mwanafunzi huyo anayechukua masomo ya sheria katika chuo hicho akiwa mwaka nne ambaye hivi sasa amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili chini ya uangalizi maalum, alikuwa na wenzake Joseph Hansi, Robert Alex, Lunura Masalu na Kitojo Karani wakati wa tukio.
Taarifa zinaeleza kuwa watu wanne wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevamia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kumshambulia mwanafunzi huyo kwa kumpiga risasi mwilini na kupora kompyuta mpakato na simu za kiganjani.
Mwanafunzi huyo alikuwa anamalizia mitihani yake ya mwisho ya kuhitimu elimu hiyo, jana.
Tukio hilo lilitokea wakati mwanafunzi huyo akijisomea na wenzake hao watatu majira ya saa 9:00 usiku wakijiandaa kwa mtihani ambapo ghafla walivamiwa na majambazi hao na kutakiwa walale chini.
Wanafunzi hao walipotii amri hiyo, majambazi hao waliwapora kompyuta mpakato tatu, simu tatu na pochi ndogo.
Wakati majambazi hao wanaondoka, Alex alinyanyuka na kuwafuata majambazi kwa kuwaomba wampe kitambulisho chake ili aweze kuingia kwenye mtihani.
Kitendo hicho kilisababisha mmoja wa majambazi hao kumyatulia risasi mwanafunzi huyo.
Kufuatia tukio hilo, wanafunzi wa chuo hicho waliandamana majira ya saa 10 alfajiri kuelekea ofisi ya kituo cha polisi chuoni hapo kulalamikia kutokuwepo kwa ulinzi wa kutosha kwenye mabweni yao.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Utawala (UDSM), Profesa Yunus Mgaya, ilieleza kuwa uongozi wa chuo unasikitika kutokea kwa tukio la ujambazi katika ukumbi wa mihadhara wa Yombo 1 majira ya saa 9 usiku kuamkia Ijumaa.
Taarifa ilisema tukio hilo lilijiri wakati wanafunzi wakiwa wanajisomea kwa maandalizi ya mitihani inayoendelea chuoni hapo.
"Majambazi waliwavamia wanafunzi hao na kuwapora mali walizokuwa nazo, zikiwemo kompyuta mpakato na simu za mkononi," ilisema taarifa yake.
Baada ya tukio hilo wanafunzi waliokuwa kwenye eneo la tukio walimchukua mwanafunzi aliyejeruhiwa kwa risasi na kumpeleka kituo cha afya chuoni hapo na baadaye kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Ofisa Habari wa Hospitali ya Muhimbili, Aminieli Aligaeshi, alisema kuwa mwanafunzi huyo tayari ameshafanyiwa upasuaji wa kutolewa risasi hizo.
Alisema kwa sasa hali yake inaendelea vizuri na amewekwa kwenye chumba maalumu (ICU) kwa ajili ya uangalizi wa karibu.
Uongozi wa Chuo umewaomba wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na hasa wanafunzi, kuendelea kuwa watulivu, wakati vyombo vya usalama vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemain Kova, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo majira ya saa 9.00 usiku na kwamba bado wahusika hawajafahamika.
Alisema majambazi hao walikuwa na mapanga na visu na baada ya kuwavamia waliwataka wanafunzi hao kulala chini na kupora mali zao.
Kova alisema kitendo cha mwanafunzi huyo kuwafuata majambazi hao kiliwaudhi na kuanza kumpiga kwa risasi.
Akizungumzia maandamano yaliyofanywa na wanafunzi hao alisema yalikuwa na lengo la kushinikiza kuboreshewa kwa ulinzi. Aidha, alisema jeshi la polisi linaendelea na msako mkali ili kuwanasa majambazi waliohusika katika tukio hilo.
CHANZO: NIPASHE
Comments
Post a Comment