SOMA HAPA KAULI YA KALAJEREMIAH KUKABIDHI TUNZO KWA MAMA YAKE MAREHEMU MANGWEA
MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Kala Jeremiah ameamua kumuenzi aliyekuwa msanii wa hip hop, Albert Mangwea 'Ngwair' aliyefariki Mei 28 mwaka huu nchini Afrika Kusini kwa kutoa tuzo yake aliyoipata mwishoni mwa wiki iliyopita na kuiwakilisha kwa familia ya msanii huyo mkoani Morogoro.
Msanii huyo amepokea tuzo za Kilimanjaro Music 2012-2013. ikiwemo ya msanii bora wa hip hop mwaka huu ameiwasilisha tuzo hiyo juzi mchana kwa familia ya msanii pamoja na kwenye kaburi la msanii huyo ikiwa ni ishara ya kumuenzi kwa vitendo.
Akizungumza na mwandishi wa habari wa jamiileo tz.blogspot.com katika msafara wa kwenda Morogoro, Kala aliweka wazi kuwa ameamua kumpa tuzo hiyo kutokana na heshima aliyokuwa nayo katika suala la muziki hususani wa hip hop na kuipelekea kwa familia yake ili itambue mchango wake katika swala la muziki .
Alisema ameamua kumpa tuzo hiyo kutokana na uwezo aliyekuwa nayo na ni hali ambayo imemtokea mwenyewe bila ya kushawishiwa na mtu yeyote yule anastahili, huku akiamini kuwa kufika kwake katika familia ya marehemu ni moja ya kuitia nguvu familia hiyo na kuonyesha kujali na kuwa pamoja nayo katika kipidni hiki kigumu
"Mimi kama msanii bora wa hip hop kwa mwaka huu, nimeamua kumkabidhi tuzo hii ya msanii bora wa hip hop marehemu Ngwair kwa sababu alikuwa anafanya kazi hiyo ya muziki, ambao na mimi sasa nafanya na isitoshe yeye alikuwa ni mwalimu wangu kwa kile alichokuwa anaimba," alisema Kala.
Wakati huo huo msanii wa muziki wa kizazi kipya Seleman Msindi 'Afande Sele' mwenyeji wa Morogoro alimpokea Kala alipofika mkoani hapo kwa ajili ya kuipeleka tuzo hiyo kwa familia ya Ngwair.
Afande Sele alisema kuwa kitendo alichoamua kukifanya Kala kwa kuamua kutoa tuzo hiyo ni kitendo cha kipekee kinachoonyesha faraja kwa wasanii wa muziki kwa ujumla pamoja na familia ya marehemu.
Alisema kuwa Kala ameanza kazi ya muziki muda mfupi na amejalibu kuonyesha thamani kwa wasanii walioanza muziki kabla yake hivyo kitendo alichokifanya ni cha kuigwa.
"Kala anastahili pongezi kwani kitendo alichokifanya ni cha kiungwana na kinastahili kuigwa kutoa tuzo uliyopewa na haujawahi kupewa hapo mwanzo ni kitendo cha ujasiri na kuonyesha unathamini michango iliyopita " alisema Afande Sele.
Mbali na kuikabidhi tuzo hiyo kwa familia pia Kala aliweza kutoa rambirambi zake kwa familia ya marehemu ikiwa ni sehemu ya kuikamilisha ziara yake.
Comments
Post a Comment