KUWA WA KWANZA KUMFAHAMU GAIDI ANAYESUMBUA ULIMWENGUNI ALIYEKAMATWA NA POLISI WA TANZANIA
Mtu huyo aliyekamatwa wilayani Kyela, pia anatuhumiwa kuhusika na vitendo vya ugaidi nchini Uingereza.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, alisema mtuhumiwa huyo alikuwa anatumia majina mawili tofauti kwenye hati za kusafiria na alikuwa akijaribu kuvuka mpaka wa Tanzania kuelekea Malawi.
Alisema mtuhumiwa huyo alitumia hati ya Tanzania yenye namba AB 651926 yenye jina la Adil Ally Patel na hati ya Uingereza yenye namba NO 51555382 yenye jina la Iqbal Hassan Ally.
Manumba alisema hati ya Tanzania aliyokamatwa nayo ni kati ya hati 26 zilizoibiwa kwenye Ofisi za Uhamiaji mwaka mmoja uliopita.
Alisema mshukiwa wa ugaidi alikuwa akisaidiwa na Mtanzania mmoja ambaye hakumtaja jina na baada ya kukaguliwa kompyuta mpakato (laptop) yake ilikuwa na maneno ya uchochezi ya kidini kuhusu imani tofauti.
Manumba alisema aliwasiliana na Serikali ya Uingereza kuhusu hati ya mtuhumiwa huyo na kuelezwa kuwa ni halali na kufahamishwa kuwa mtu huyo wanamtafuta kwa tukio la ugaidi nchini Uingereza.
Alisema kuna Mtanzania mwingine ambaye hakumtaja jina, alikamatwa kwa kuhisiwa kujihusisha na mtuhumiwa huyo wa ugaidi ambaye baada ya kukaguliwa pia alikutwa na kompyuta yenye maneno ya uchochezi dhidi ya dini isiyomhusu.
Alisema mtuhumiwa huyo alijitambulisa kuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo kimoja kilichopo nchini Sudan.
Manumba aliwataka wazazi kuwa waangalifu na vijana wao wanaokwenda kusoma nje ya nchi kwa kuwa baadhi yao hurubuniwa na kujiingiza katika mambo yanayohusiana na ugaidi.
Aliongeza kuwa polisi wana uhakika kwamba kuna baadhi ya vikundi vya kigaidi ndani ya nchi ambavyo vina mipango ya siri ya kutekeleza ugadi nchini.
Aliwataka Watanzania kuwa waangalifu wakati polisi ikifanya kazi yake ya uchunguzi na kuonyesha kuwa hali ya usalama si nzuri nchini kutokana na matukio ya kihalifu yanayoendelea.
Aidha, alisema polisi inaendelea na uchunguzi dhidi ya matukio ya mlipuko miwili ya mabomu iliyotokea mkoani Arusha na lile la kuuawa kwa Padri Evarist Mushi, Zanzibar.
Alisema matukio hayo yameonyesha sura mbaya kwa Tanzania ya kuwepo kwa tishio la ugaidi.
Alisema uchunguzi utakapokamilika washitakiwa watafikishwa kwemnye mikono ya sheria kuhukumiwa kwa makosa ya jinai.
Aliongeza kuwa taarifa zitakazokuwa zikitolewa na raia wema zitasaidia polisi kurahisisha uchunguzi na kuwakamata wahusika kwa wakati.
Manumba ametahadharisha kuwa ongezeko la uhalifu nchini limekuwa likihusisha baadhi ya wananchi kutumika vibaya na wavunjifu wa amani.
Alisema kufuatia matukio hayo, baadhi ya watuhumiwa wanashikiliwa na baada ya uchunguzi kukamilika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Hii ni sifa mbaya Watanzania wanapaswa kujiepusha na vishawishi vya aina yoyote vitakavyopelekea kuvunjika kwa amani iliyopo tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanzania,” alisema.
Katika matukio ya kigaidi yaliyotokea siku za hivi karibuni watu watatu walikufa na zaidi ya 70 kujeruhiwa baada ya kurushwa bomu kanisani na mtu asiyefahamika katika kanisa la Katoliki Jimbo Kuu la Arusha wakiwa wamejumuika katika uzinduzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Olasiti.
Katika tukio jingine jijini humo, bomu lilipuka kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) eneo la Soweto kata ya Kaloleni mkoani Arusha.
Katika tukio hilo watu watatu walifariki dunia kutokana na mlipuko wa bomu wakati chama hicho kikiwa kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa madiwani.
Wakati huo huo Manumba alisema polisi jijini Dar es Salaam limekamata meno ya tembo 347 katika eneo la Kimara ambayo yanaamika yamepatikana kwa njia za kijangili katika mbuga za Tanzania.
Alisema mbali na nyara hizo, kuna meno mengine ya tembo 788 yalikamatwa nchini Malawi katika mji wa Mzuzu na kwamba inaamika kuwa yalisafirishwa kutoka Tanzania kama mzigo wa saruji kutoka katika kiwanda cha Saruji Mbeya.
Manumba alisema polisi nchini wanafanyakazi kwa kushirikiana na polisi wa kimataifa kuhakikisha kuwa ukweli wa matukio yanakuwa wazi na uchunguzi ukikamilika wahusika watafikishwa katika vyombo vya sheria.
Comments
Post a Comment