WAZIRI MAGUFULI ATAMANI KUWA RAIS WA TANZANIA......ANADAI KWAMBA YUPO TAYARI KUGOMBEA MWAKA 2015 ENDAPO ATAKIDHI MASHARTI

 Katika hali inayoonyesha kuwa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, anautamani urais, amesema anaweza kutangaza nia hiyo kama atakidhi masharti yatakayowekwa kwenye Katiba mpya.

Alisema iwapo Katiba ijayo itakuja na sifa ambazo atakidhi vigezo kuna uwezekano mkubwa wa kuwania nafasi hiyo na kwamba iwapo atapungukiwa sifa zinazohitajika kwa mujibu wa Katiba hataingia kwenye kinyang’anyiro hicho.

Dk. Magufuli ambaye pia ni Mbunge wa Chato alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wazee wa wilaya hiyo kwenye ukumbi wa ‘Mshikamano Saccos’, muda mfupi baada ya mzee Paschal Nyambibo (87) kumsihi agombee nafasi hiyo mwaka 2015 kutokana na sifa zake za uchapakazi ndani ya serikali.

Nyambibo alisema kutokana na uwajibikaji mzuri aliouonyesha Dk. Magufuli tangu mwaka 2000 akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi na katika wizara mbalimbali, Watanzania wamekuwa na imani kubwa na uwajibikaji wake na kwamba anastahili kupeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ifikapo mwaka 2015.

Licha ya kauli hiyo kusababisha minong’ono mingi kwa wazee waliohudhuria kikao hicho, Dk. Magufuli alionekana kutuliza hali hiyo kwa kusema isubiriwe Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano iwapo itakuwa na masharti ambayo yatamfanya kujitathimini iwapo ana sifa za kugombea au vinginevyo.

Hata hivyo, Dk. Magufuli hakusita kuonyesha hisia zake za kukerwa na baadhi ya wananchi wanaobeza maendeleo aliyotekeleza katika jimbo lake tangu alipochaguliwa kuwa Mbunge.


Alimshutumu hadharani aliyekuwa Katibu wa CCM wilaya ya Chato kabla ya kuhamishiwa wilayani Mbogwe, Gervas Stephano, kuwa hana shukrani.

Dk. Magufuli alimwelezea katibu huyo kuwa hana fadhila kutokana na mambo mengi aliyomtendea tangu akiwa katibu wa ofisi yake ya jimbo ambapo alimsaidia kupanda ngazi na kuwa Katibu wa CCM wilaya Chato, Kwimba, Kasulu, Kilosa na kurejea tena Chato kabla ya kuhamishiwa wilaya ya Mbogwe mkoani Geita  kuendelea na wadhifa huo.

“Tatizo lenu watu wa Chato hamna shukrani…mambo mengi nimefanya hapa Chato, lakini yote mnaona ziro…hata niliowasaidia kama Gervas naye sasa hivi ananiponda…lakini nawashukuru sana wazee wangu kwa kunikumbusha niliyoyafanya kwenye jimbo letu kupitia risala yenu nzuri,
” alisema Dk. Magufuli.

“Kutokana na hali hiyo ninawazawadia Sh. 1,000,000 mfanye sherehe ya kujipongeza kwa kuwa natambua mmejitesa sana mpaka kufanikisha kikao hiki cha leo…na kwa kuwa hamna mradi wowote wa kuwaingizia kipato kama wazee, ninaahidi kuwapa Sh.   3,000,000 kutoka mfuko wa jimbo, ili muanzishe walau saccos ya kukopeshana,” alisema.

Baadhi ya viongozi na wananchi wamekuwa wakilitaja mara kwa mara jina la Waziri Magufuli miongoni mwa watu wanaodhaniwa kutaka kugombea nafasi ya urais wa Tanzania mwaka 2015, ingawa mwenyewe amekuwa akikanusha uvumi huo.

Mbali na Dk. Magufuli, wengine ndani ya CCM wanaotajwa  ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa; Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye anajiita mtaji wa urais; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Ushirikiano wa Kimataifa –CCM, Dk. Asha-Rose Migiro na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Mambo ya Nje, Bernard Membe, ambaye alipata kusema anasubiri kuiteshwa na Mungu kuwania nafasi hiyo.


Comments