LITA 29 ZA TINDIKALI ZAKAMATWA HUKO ZANZIBAR.... AL-SHABAB WAHUSISHWA..!

!


SIKU chache baada ya Padri wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Machui, Anselm Mwang’amba kumwagiwa tindikali Zanzibar, Polisi visiwani hapa imekamata lita 29 za tindikali kwenye magaloni ya ujazo tofauti. Kamishna Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Jeshi hilo, Kilimani mjini hapa. “Jeshi la Polisi limekamata watu 15 kwa matukio mbalimbali...wapo tunaowahoji kuhusu mtandao wa kundi la Al-Shabaab, lakini wapo wanaohusishwa na matukio ya tindikali, hawa tunataka kujua wameipata wapi na nani amewauzia,” alisema. Akizungumzia tukio la mwishoni mwa wiki la Padri Mwang’amba kumwagiwa tindikali alisema:“Hivi sasa tunazungumza tukio la kumwagiwa tindikali Padri Mwang’amba Mlandege …upelelezi unaendelea na watu kadhaa tumewakamata ingawa ni mapema mno kutaja majina yao, lakini wakati ukifika tutawafikisha mahakamani.” Akifafanua, Kamanda Mussa alisema Polisi inakabiliwa na changamoto kubwa ya vitendo vya hujuma kwa kutumia tindikali dhidi ya watu mbalimbali Zanzibar. Kuhusu matukio mawili ya kumwagiwa tindikali kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa, Rashid Ali Juma na Katibu wa Mufti, Shekhe Fadhil Soraga, alisema upelelezi wa shauri hilo umekamilika na jalada lipo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka na Makosa ya Jinai (DPP).


Shekhe Soraga alimwagiwa tindikali mwishoni mwa mwaka jana akiwa eneo la Magogoni Msumbiji, Mkoa wa Mjini Magharibi, wakati akiwa mazoezini. Wakati akifanya mazoezi hayo, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Yusuf Ilembo, Shekhe Soraga alimwona mtu mwingine akifanya mazoezi mbele yake kabla ya kumgeukia na kummwagia tindikali iliyomjeruhi usoni na kifuani. Baadaye mtu aliyefanya unyama huo, alitoweka na kuelekea kusikojulikana. Mbali na Shekhe Soraga, mwanzoni mwa Agosti, walimu wawili wa kujitolea raia wa Uingereza, Kate Gee (18) na Krisdtie Trup (18), walijeruhiwa kwa tindikali, wakati wakienda kula usiku. Akizungumzia upelelezi wa tukio hilo, Kamanda Mussa alisema upelelezi uko hatua za mwisho kukamilika. Kutokana na uhalifu huo, walimu hao walikimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam kupewa huduma na baadaye walirudishwa kwao kwa matibabu zaidi, na mmoja wao anatarajiwa kupandikizwa ngozi. Msako Kuongezeka kwa matukio hayo, kumesababisha Polisi Zanzibar kuanza operesheni kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kwa lengo la kupunguza matumizi holela ya tindikali.Kamanda Mussa alisema operesheni hiyo ilianza Jumamosi na inalenga waagizaji, wasambazaji na watumiaji wa tindikali kwa ujumla. Kwa usimamizi wake, Kamanda Mussa alisema msako maalumu umeanza katika maduka yanayouza tindikali ili kujua kama wanamiliki vibali halali vya biashara hiyo. “Msako wa tindikali umeanza na sasa tumeanza ukaguzi wa maduka ya biashara hiyo kujua kama wana leseni ya kuiendesha,” alisema. Pia Polisi imeanza kukutana na wadau kuangalia sheria ya kumiliki tindikali na matumizi yake ikiwamo kudhibiti tatizo hilo. Al-Shabaab Kati ya watuhumiwa 15 wa kikundi cha kigaidi cha al Shabaab wanaoshikiliwa Polisi, Kamanda Mussa alisema baadhi yao ambao hakuwataja majina, wanatuhumiwa kuhusika na kikundi hicho na itikadi za imani kali za kidini. Al-Shabaab, yenye asili yake Somalia, ina lengo la kutafsiri Sheria za Kiislamu katika namna ya imani kali ya kidini. Kikundi hicho kinadaiwa kupewa mahitaji ya kifedha kutoka vikundi vya kimataifa vya kigaidi, baadhi ya nchi na wananchi wa Somalia wanaoishi nje ya nchi yao. Wanazuoni Taarifa ya wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay-atul Ulamaa), iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, ilitaka Watanzania kurejea kwenye utamaduni wa karne nyingi zilizopita, wa kuvumiliana na kushirikiana kulinda amani nchini. Mwenyekiti wa wanazuoni hao nchini, Shekhe Sulaiman Kilemile, alieleza katika taarifa hiyo, kwamba kitendo cha Padri Mwang`amba kumwagiwa tindikali, hakikubaliki na ni wajibu wao kukilaani kwa nguvu zote. “Hivi ni vitendo vinavyoashiria chuki baina ya Watanzania wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vikiachwa viendelee vitasababisha amani, utulivu na busara kutoweka nchini,” alieleza Shekhe Kilemile katika taarifa hiyo. Taarifa hiyo pia ilikemea matumizi ya silaha za moto kama ilivyotumika kumwua Padri Evarist Mushi, na kumjeruhi Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Ponda Issa Ponda.“Matukio kama hayo yote ni hatari ambayo yanaweza kubadili sura nzuri ya Tanzania…tunachukua nafasi kuwahadharisha viongozi wa dini na wengineo wasikurupuke kuelekeza tuhuma kwa kikundi kimoja dhidi ya kingine. “Hivyo si halali tukio kama hilo kuhusishwa na udini, uzanzibari na utanganyika kabla ya kufanya uchunguzi na kupata dalili sahihi za kutosheleza,” alisema Shekhe Kilemile. Askofu Shao Katika hatua nyingine, Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao, amesema usalama wa viongozi wa dini umekuwa mdogo Zanzibar kutokana na kuendelea kupokea vitisho. Askofu Shao alisema hayo Dar es Salaam, alipokwenda kumjulia hali Padri Mwang’amba, ambaye amelazwa Muhimbili. Padri Mwang’amba alisema Julai alipokea vitisho kutoka kwa vijana ambao hufanya mazoezi katika njia ambayo yeye hupita kwenda kuona wazee, lakini hana uhakika kama ni vijana hao ndio wameshiriki uhalifu huo.“Siwezi kusema moja kwa moja kama ni hao vijana, maana walinitolea vitisho kuwa ipo siku watanifanyia kitu kibaya kwa kuwa nawasumbua wakati wanafanya mazoezi. “Siwezi kusema moja kwa moja kuwa ni wao ama ni mwendelezo wa matukio ya watu wanaofanya uhalifu kwa kuwamwagia wenzao tindikali,” alisema Padri Mwang’amba. Aliongeza kuwa baada ya kupokea vitisho hivyo alitoa taarifa Polisi na hali ikaendelea kuwa shwari, kwani hakupokea tena vitisho mpaka alipomwagiwa tindikali. Aliziomba mamlaka husika kuhakikisha wahusika wanatafutwa na kuchukuliwa hatua, pia kudhibiti matukio ya aina hiyo ambayo yamekuwa yakijitokeza visiwani humo. Askofu Shao alisema vitisho wanavyopata ni vingi zaidi, pia hawawezi kujua madhumuni na makusudi ya matukio hayo, kutokana na kuwepo kwa migongano tofauti ya kisiasa, kidini na mingineyo.Alisema asilimia kubwa ya matukio yanayotokea yamekuwa yakilenga dini moja na kufanya viongozi wa dini kuhofia usalama wao. “Kwa tukio hili hii ni ishara tosha kwamba usalama wetu ni mdogo sana, sasa hivi tunaogopa hata kutembea,” alisema

Comments