BINTIA APIGWA KICHAPO CHA MBWA MWIZI NA KUMWAGIWA MKOJO NA MAMA YAKE CHANZO KUGOMA KUZIMA TAA YA CHUMBANI KWAKE USIKU..!!



Vitendo vya kikatili vimekuwa vikikithiri katika jamii yetu, jambo ambalo linakemewa na taasisi mbalimbali bila mafanikio.

Hilo limejitokeza kwa mwanafunzi anayesoma Chuo cha Polisi Ufundi Kilwa Road, Temeke, Yunia Manyama (pichani) aliyelazwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi la Polisi, jijini Dar akiuguza majeraha yaliyotokana na kipigo kutoka kwa mama yake mdogo aliyemtaja kwa jina la Sikitu Shirati.

Tukio hilo la kikatili lilitokea usiku wa kuamkia Jumanne wiki iliyopita saa saba usiku kwa kile kinachodaiwa kuwa hakuzima taa chumbani kwake wakati wa kulala.

Mbali na kupata kipigo hicho kwa kutumia waya wa umeme, majeruhi huyo alidai mama yake huyo alimwagia mkojo wa mwanaye uliokuwa kwenye kopo .
 

 “Nikiwa nimelala na wenzangu watano  nilishitukia nikipigwa kwa waya wa umeme miguuni na mikononi na mama mdogo, nilipomuuliza kwa nini ananipiga alinijibu kuwa sababu sikuzima taa ya chumbani wakati mimi nililala mapema kabla ya wenzangu,” alidai mwanafunzi huyo.

Aliongeza kuwa alimpiga hadi aliishiwa nguvu, baadaye alijikokota hadi kwa baba yake mkubwa ambaye anaishi karibu na maeneo hayo, aligonga na kufunguliwa mlango na alipomuona mwili  umetapakaa damu alitokwa na machozi.

Yunia alieleza kisa cha kupigwa na mama yake mdogo ambapo wote waliokisikia walisema ni cha kipuuzi. Kulingana na hali yake ilivyokuwa, ililazimika kupelekwa hospitali hiyo usiku baada ya kupata PF3, katika Kituo cha Polisi Kilwa Road. 

Baada ya kupata matibabu alienda kituo cha polisi na kufungua jalada lenye kumbukumbu namba KLR/RB/4905/2013 shambulio la kudhuru mwili.

Alidai kuwa polisi baada ya kujua kwamba Sikitu ni mke wa askari polisi hawakuweza kuchukuwa hatua. Kwa sasa hivi mwanafunzi huyo baada ya kuruhusiwa hospitali anajiuguza kwa baba yake mkubwa.

Kwa upande wake Sikitu alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema kwamba alikuwa akimwadhibu kama mwanaye. “Alifanya kosa ndiyo maana niliamua kumuadhibu,” alisema Sikitu.

Comments