Mtoto ateswa na ugonjwa wa ajabu kwa miaka 17


13th October 2013
Chapa
Mtoto Selemani Rajabu
Ni mateso makubwa aliyoyabeba kwa miaka 17 sasa akiwa hawezi kutembea wala kupanda kwenye gari kutokana na ugonjwa wa ajabu uliosababisha uvimbe mkubwa kwenye miguu yake unaomlazimu ashindwe kufanya shughuli yoyote isipokuwa kwa msaada wa watu wengine.

Selemani Rajabu, alizaliwa mwaka 1996, na kukua na maradhi hayo ambayo kadri umri unavyokua ndivyo uvimbe unavyozidi kuongezeka.
Uvimbe huo ulianza kidogo kwenye nyayo za miguu yake ambao hata hivyo, wazazi wake waliona ni wa kawaida.
Selemani anasema baada ya kufika umri wa kukaa ndipo wazazi wake waliposhtuka na kugundua kuwa lilikuwa tatizo kubwa baada ya uvimbe huo kuongezeka kila siku na kuamua kumpeleka hospitali.
“Mateso ninayopata siwezi kusimulia na sijui nini hatma ya maisha yangu kwani naishi katika mazingira magumu kutokana na maumivu katika miguu yangu,” anasema kwa masikitiko.
Ukikutana na Selemani lazima utatokwa na machozi jinsi anavyoishi kwa mateso. Amekuwa mtu wa kubebwa na kutolewa nje na kurudishwa ndani.
Selemani ni mkazi wa kwa Butu eneo la Bomba Mbili kwa Chela kata ya Kivule, Wilaya ya Ilala mkoa wa Dar es Salaam ambako anaishi na mzazi wake.
Akizungumza na mwandishi wa blogu hii Jumapili baada ya kumtembelea nyumbani kwao, anasema kuwa kutokana na uvimbe huo anashindwa kutembea na kadri miaka inavyokwenda ndivyo miguu hiyo inavyozidi kuvimba na wakati mwingine 
kumsababishia maumivu makali.
"
Tangu nikiwa mdogo niliambiwa sijawahi kutembea hadi nilivyofikia hapa ninateseka," anasema.
Selemani anasema kutokana na hali yake inambidi ajisaidie hapo hapo kwa kuwa hawezi kwenda 
chooni.

Hata anapotolewa nje kupata hewa inambidi abebwe na watu wawili kutokana na uzito wa uvimbe wa miguu yake.
"Natamani miguu yangu ipungue uvimbe ili niweze kuwa kama watoto wenzangu na kazi nyingine nifanye mwenyewe na mimi niweze kuishi kwa raha kama walivyo watoto wengine,” anasema.

Anatamani aende shule lakini hali aliyonayo haimruhusu na hivyo kumkosesha haki zake za msingi.
Wakati anapoumwa hupata shida zaidi kwa kuwa inabidi wazazi wake wawe na zaidi ya Sh. 20,000 kwa ajili ya kukodi gari aina ya pick up kwa kuwa magari mengine hawezi kuenea.

Selemani anaeleza kuwa wakati akiwa anaishi Manzese aliumwa malaria hivyo ndugu zake walilazimika kumuomba daktari aende nyumbani kumfanyia vipimo.

Hata hivyo, anasema daktari huyo aligoma na kuwataka ndugu zake wampandishe kwenye teksi au bajaji.
Kutokana na tatizo hilo, ndugu zake huamua kumnunulia dawa za kutuliza maumivu kutokana na kukosa uwezo wa kukodi gari, dawa ambazo hutumia mpaka sasa kila anapojisikia vibaya.

Selemani anawaomba wasamaria wema walioguswa na tatizo lake wamsaidie kwa hali na mali ili aweze kwenda India kufanyiwa upasuaji.
Anasema wazazi wake wamehangaika katika hospitali mbalimbali ikiwamo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili bila mafanikio.
Aidha, walipoenda hospitali ya CCBRT, waliambiwa kuwa tatizo hilo hawawezi kulihudumiwa na kutakiwa kurudi nyumbani.
“Natamani ningepata mfadhili akanisaidia nikatibiwe huko India maana huwa nasikia watu wakipelekwa kutibiwa angalau huu mguu unywee niweze kutembea kama wenzangu ninapata shida sana hilo tu ndiyo linanisumbua,” anasema.
Baba wa mtoto huyo Rajabu Yusuph, anasema kuwa mtoto wake alianzwa na tatizo hilo kwa uvimbe katika miguu yote miwili ambapo hawakuweza kugundua kwa haraka kama ni tatizo kwani walidhani ni unene.
Anasema wakati alipofika umri wa kutambaa waliona tatizo hilo linaongezeka na kumpeleka hospitali lakini alipewa dawa ambazo hazikuweza kutatua ugonjwa huo.
Yusuph anasema huwa anaumia jinsi mwanawe anavyoendelea kuteseka kwani hana uwezo wa kumpeleka nje ya nchi aweze kupatiwa matibabu angalau uvimbe huo uweze kupungua.
Anasema anawaomba wasamaria wema na hata upande wa serikali waweze kumsaidia hata kama atashindwa kutembea basi uvimbe huo uweze kupungua aweze kuwa kama watoto wengine.
Kwa upande wa majirani ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema wamekuwa wakiishi na familia hiyo kwa ukaribu pamoja na kumfariji mtoto huyo.
“Hata mimi naingiwa na imani na kwamba kila nikimuona jinsi alivyo huwa naumia sana na sina uwezo wa kumsaidia zaidi ya kumuombea kwa Mungu aweze kumponya,” alisema jirani huyo
Alisema serikali inatakiwa kumuangalia mtoto huyo kwa jicho la huruma ili waweze kumsaidia katika kumpatia matibabu ya kumpeleka nje ya nchi.
Mtu yoyote atakayeguswa na tatizo la mtoto huyu kwa hali na mali ili apatiwe matibabu awasiliane na baba yake mzazi Rajab Yusuph kwa simu 0718355563 pia Mhariri wa gazeti hili 0715268581

Comments