SOMA HAPA WEZI WALIVYOINGIA IKULU NA KUIBA KUKU,WALINZI WASHINDWA KUWABAIN IWAALIFU
Ikulu ndogo anayoishi Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga, imevamiwa na watu wasiofahamika ambao waliiba kuku waliokuwa bandani.Tukio hilo limetokea usiku wa Oktoba 2 mwaka huu, ambapo kuku hao walikuwa kwenye banda lililojengwa kwa matofali.
Wizi huo umetokea baada ya wezi hao kutoboa ukuta wa banda hilo mbali ya kuwepo ulinzi wa kutosha.
Chanzo chetu cha habari kutoka Jeshi la Polisi wilayani humo, kilisema askari waliokuwa zamu siku hiyo katika nyumba hiyo
hawakuweza kuwabaini wezi hao.
"Ni tukio ambalo linatuumiza kichwa, eneo kama hili kuvamiwa na kuvunjwa, uchunguzi wa kina ufanyike kubaini kwanini wahalifu hawakubainika mapema na kukamatwa," kilisema chanzo hicho.Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa Mbinga walisema ni jambo la kushangaza eneo hilo lenye ulinzi mkali kuvamiwa na wezi hao kufanikiwa kuiba kuku.
"Mkuu wa Wilaya ni mwakilishi wa Rais wetu, inakuwaje eneo la Ikulu ndogo analoishi kuvamiwa na wezi wakati vyombo vya usalama vipo," walihoji wananchi hao.Kamanda wa Polisi mkoani humo, Deusdedith Nsimeki, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa;
"Ni kweli taarifa juu ya kuvamiwa na kuvunjwa banda la kuku katika Ikulu ndogo nimezipata hivi punde...kuku kadhaa wameibwa. "Idadi yake sijaipata lakini uchunguzi bado unaendelea ili tuweze kubaini ni nani aliyehusika na uhalifu huo, hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusika na tukio hili," alisema
Comments
Post a Comment