Vijana watwangana ngumi kufuatia kuvuliwa madaraka kwa mbunge wa kazkazini Zitto Kabwe

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe
Uamuzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kuwavua nafasi za uongozi vigogo wake watatu akiwamo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, umepokelewa vibaya na baadhi ya wafuasi wao ambao wameamua kupigana ngumi.

Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alivuliwa nyadhifa zake sambamba na aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Mkumbo Kitila na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha,Samson Mwigamba.

Kamati Kuu ya chama hicho ilichukua hatua hiyo Ijumaa iliyopita, baada ya kubaini waraka wa usaliti waliouandaa ukiibua tuhuma mbalimbali dhidi ya chama na viongozi wake ngazi ya taifa.

NGUMI ZAPIGWA MBEYA

Kundi la vijana wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Zitto jijini Mbeya wanadaiwa kurushiana makonde na viongozi wa Chadema katika ofisi ya chama hicho Wilaya ya Mbeya Mjini kwa madai ya kutofautiana msimamo kuhusiana na uamuzi wa Kamati Kuu.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, David Mwambigija maarufu kwa jina la ‘Mzee wa Upako’, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo juzi mchana.
Mwambigija alisema kuwa chanzo cha vurugu hizo ni vijana zaidi ya 18 wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Zitto kuanza kufanya vikao vya siri mjini Mbeya kwa nia ya kukihujumu chama.


Alisema uongozi wa chama ngazi ya wilaya ulipopata taarifa hizo alizodai kuwa ni za kiintelijensia na kuwa yeye (Mwambigija) ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya chama hicho wilaya, aliamua kuaandikia barua ya kuwaita ofisini kwa lengo la kuwahoji.

Alisema vijana hao walipofika ofisini kwake huku wajumbe wa Kamati Tendaji wakiwa tayari wameketi kwa ajili ya kuwahoji, waliingia ndani ya ofisi na kulazimisha wahojiwe kwa pamoja badala ya kuhojiwa mmoja mmoja.

Alisema walipotakiwa watoke nje ili kila mmoja ahojiwe kwa wakati wake, waligona na kukataa kutoka ofisini na ndipo yeye kama Mwenyekiti alipoamuru kikosi cha ulinzi wa chama hicho maarufu kwa jina la Red Bridged kuwatoa nje kwa nguvu na ndipo vurugu hizo zilipoanza.

“Ni kweli kumetokea vurugu kubwa ofisini kwetu wakati kikao cha kamati ya utendaji kikihitaji kuwahoji vijana wanaoendesha vikao vya siri kutaka kukihujumu chama kutokana na uamuzi wa Kamati Kuu kumvua Zitto madaraka, tumepata taarifa hizi kwa njia zetu za kiintelijensia kuwa vijana hawa wapo kwenye kundi la Zitto,” alisema Mwambigija.

Hata hivyo, Mwambigija alipotakiwa na gazeti hili kuonyesha uthibitisho juu ya tuhuma dhidi ya vijana hao, alisema kuwa ushahidi bado ni siri kwa vile wametumia njia zao za kiintelijensia kubaini mtandao wa vijana hao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Mkoa wa Mbeya, Joseph Kasambala ambaye ni mmoja wa vijana walioitwa kuhojiwa na kamati ya utendaji alikanusha madai hayo na kusema kuwa vurugu hizo hazikuwa na uhusiano hata kidogo na sakata la Zitto kuvuliwa madaraka.

Alisema chanzo cha vurugu hizo ni Kamati hiyo kumuita na kutaka kumuhoji kinyume cha katiba ya Chadema yeye (Kasambala) ambaye ni kiongozi wa mkoa, hivyo hawezi kuhojiwa wala kuwajibishwa na kamati hiyo ambayo ni ngazi ya wilaya.

Alisema kuwa Katiba ya Chadema inaeleza wazi kuwa kingozi wa mkoa mamlaka yake ya nidhamu ni Kamati Kuu ya Chadema Taifa, hivyo kitendo cha ngazi ya wilaya kumuita na kutaka kumuhoji ni ukiukwaji wa Katiba.

“Mimi baada ya kupata barua ya kuitwa na Kamati hiyo ikinieleza kuwa nina tuhuma ambazo hazikuandikwa kwenye barua waliyoniletea, nilikwenda ofisini ili nipewe tuhuma zangu kwa maandishi kama ambavyo Katiba inaelekeza, lakini nikashangaa eti wanataka wanihoji, nikakataa walipotaka kunishinikiza vijana wakawajia juu wakipinga nisidhalilishwe na ndipo vurugu zile zilipoanza,” alisema Kasambala.

KATIBU TANGA AHOJI

Baadhi ya viongozi wa Chadema mkoa wa Tanga, wamehoji maamuzi ya kumvua madaraka Zitto na wenzake.

Katibu wa Chadema Wilaya ya Tanga, Harid Rashid, alisema jana kuwa hakubaliani na maamuzi hayo.

Rashid ambaye aliongozana na  mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Hussein Baruti na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Wilaya ya Tanga, Mohamed  Aufi, alisema  kuwavua nyadhifa viongozi hao ni uonevu kwa kuwa hawaoni kosa walilolifanya.

Alisema  kuwa Kamati Kuu ilikuwa na njia nyingi za kulipatia ufumbuzi jambo hilo badala ya kuwavua uongozi.

 Alisema kuwa wameamua kuwa wazi kuhusiana na tukio hilo kutokana na ukweli kuwa Zitto ni mtu muhimu katika uongozi wa chama.

KATIBU DAR KUHOJIWA NA POLISI

Katibu wa Chadema Wilaya ya Kinondoni na Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Henry Kilewo, jana aliitwa makao makuu ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuhojiwa kwa tuhuma ambazo zinadaiwa kuwa hazijulikana hadi sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya wito huo, Kilewo alisema kuwa jana alipigiwa simu na ofisa wa polisi (bila kumtaja jina) ili aende mara moja makao makuu ya jeshi hilo kwa ajili ya mahojiano zaidi, lakini haikuwezekana kutokana na wakili wake kuchelewa kufika eneo hilo kwa muda mwafaka.

Hata hivyo, Kilewo alisema kuwa hagopi chochote kwani yuko tayari kwa lolote kwa ajili ya kupigania haki za Watanzania.

Wakili wake, Peter Kibatara, alisema kuwa jana mteja wake alishindwa kuhojiwa kutokana na yeye (Kibatara) kuchelewa kufika muda uliotakiwa kwa sababu alikuwa na majukumu mengine ya kimahakama.

Kutokanana na sababu hizo, polisi walimtaka Kilewo na wakili wake kufika leo asubuhi kwa ajili ya mahojiano hayo.
Mwandishi wa jamiileo tz.blogspot.com alipomtaka msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, kueleza sababu za Kilewo kuitwa kuhojiwa, alisema kuwa kutaja sababu  siyo utaratibu wa kipolisi.  

Hata hivyo, ziko taarifa kuwa mmoja wa viongozi wa Chadema waliovuliwa madaraka alifungua kesi kwa madai ya kukashifiwa katika mitandao ya kijamii. Imeandikwa na Emmanuel Lengwa, Mbeya; Dege Masoli, Tanga na Isaya Kisimbilu, Enles Mbegalo, Dar.

Comments